Duh! Msama sasa anatia timu hadi uswazi

Muktasari:

Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Alex Msama, amewaambia waandishi wa habari kwamba Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ametoa Sh10 Milioni ili kusaidia juhudi za kupambana na watu wanaojishughulisha na wizi wa kazi za wasanii.

KAMPUNI ya udalali ya Msama, imekiri kupata mafanikio makubwa katika zoezi la kuwakamata watu wanaouza nakala feki za kazi za wasanii jijini Dar es Salaam, huku ikisisitiza kwamba itakatiza kila kona ya jiji na ikimaliza itahamia mikoani.

Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Alex Msama, amewaambia waandishi wa habari kwamba Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ametoa Sh10 Milioni ili kusaidia juhudi za kupambana na watu wanaojishughulisha na wizi wa kazi za wasanii.

“Wale wanaofanya biashara ya wizi wa kazi za wasanii waache na watafute kazi nyingine za kufanya kwani zoezi hili si kwa Mkoa wa Dar es Salaam tu, ni zoezi la nchi nzima na lazima watu wajifunze kulipa kodi kwani pesa za kodi zinaleta maendeleo katika nchi yetu,” alisema Msama na kusisitiza kwamba zoezi hilo litakuwa la aina yake kwani wataingia katika mitaa yote ya Dar ili kuwasambaratisha wafanyabiashara haramu.

“Tutaingia katika vichochoro vyote vya mkoa wa Dar es Salaam hasa katika maeneo yaliyokithiri kwa biashara hiyo yakiwemo Ubungo, Kimara, Manzese, Kariakoo, Mbagala, Temeke, Kigamboni kabla ya kuhamia mikoani,” alisisitiza Msama.