Dimpoz alivyonusurika kifo Afrika Kusini - 1

KATIKA nyumba za ghorofa za Weom, eneo la Morning Side, Barabara la Shannon Ln kwenye Kitongoji cha mji wa kifahari wa Sand ton jijini Johannesburg, Afrika Kusini nakutana na msanii maarufu wa Bongo Flava, Omary Nyembo au Ommy Dimpoz.

Dimpoz hayupo vilevile kama unavyojaribu kutengeneza picha. Anaumwa. Hauhitaji akwambie kama anaumwa. Hapana. Anaumwa. Unamuona tu kwamba anaumwa. Sio Dimpoz yule ambaye unamfahamu. Mchangamfu na mwenye mambo mengi ya utani.

Wakati ukiendelea kuburudika na wimbo wake wa Yanje ambao, unatamba Tanzania na Afrika Mashariki na kati kwa jumla, fahamu kwamba mpaka sasa hali ya staa huyu aliyewahi kutamba na nyimbo za Nai Nai, Baadaye, sio nzuri.

Najua unamfahamu Dimpoz wa jukwaani, wa katika video, lakini zaidi wa mitandaoni, hasa Instagram. Dimpoz mwenye mbwembwe nyingi na picha zake za kitanashati. Huyu niliyekutana naye Sandton, Johannesburg alikuwa anachechemea akiwa ameinamisha kichwa chake chini.

Sauti yake inatoka kwa shida na wakati mwingine unalazimika kusubiri apumzike kidogo ili aendelee na mazungumzo naye. Wakati mwingine anatamani kucheka au kupumua kwa nguvu, lakini inashindikana. Anakumbana na maumivu makali.

Amevaa jaketi linaloziba kichwa chake kwa sababu mbili. Kwanza ni kwa sababu amekonda sana. Lakini, pili ni kwa sababu anaziba kidonda kirefu katika eneo la shingo ambacho kilitokana na operesheni kubwa iliyomlaza hospitalini akiwa ICU kwa siku tisa.

Nini Kilimsibu? Mara ya mwisho Dimpoz alionekana katika harusi ya Ali Kiba akiwa katika afya njema kabisa.

Hata hivyo, ndani yake kulikuwa na kitu kilichokuwa kinamsumbua kwa muda mrefu. Hakuna aliyefahamu sana zaidi ya rafiki yake Ali Kiba.

“Unajua brother Edo kwa muda mrefu nilikuwa nikila chakula sometimes kuna kitu kinakuja kinakwama hakiendi. Najaribu kutumia nguvu sana kumeza, lakini inashindikana. Mara tatu nimekwenda Muhimbili eti kisa nimekwamwa na kinyama kidogo tu wakati nakula,” anaanza kusimulia Dimpoz.

“Katika harusi ya Kiba pale Dar es Salaam ilinitokea asubuhi wakati nimeandaliwa chai. Tulikuwa mimi, Kiba na Gavana Joho (Hassan Joho, Gavana wa Jiji la Mombasa ambaye ni rafiki mkubwa wa Dimpoz na Kiba). Wakati nakunywa chai nikawa napata wakati mgumu sana. Gavana Joho akashtuka. Akauliza ni kitu gani kinanitokea. Kiba akamwambia ni tatizo fulani kubwa na linanitesa.”

“Gavana akasema kama ni hivyo basi kuna umuhimu niende Mombasa kwa madaktari anaowafahamu ambao, ni wataalamu sana wa masuala ya mwili wa binadamu. Ndani ya siku chache nikaenda Mombasa. Pale ndipo tatizo kubwa lilipoonekana.”

Wakati Dimpoz akiamini kwamba tatizo lake lilikuwa limefika mwisho katika mikono ya wataalamu zaidi pengine kuliko nyumbani alikotokea, hali haikuwa hivyo kabisa.

“Baada ya uchunguzi madaktari waligundua kwamba, tatizo langu ni kubwa na nilipaswa kwenda Afrika Kusini kwa wataalamu zaidi. Iligundulilka kuwa ndani ya koo langu mishipa imetanuka kiasi kwamba, haiwezi kupitisha kitu chochote kwa urahisi.”

“Hicho ndio kilikuwa chanzo cha kuja hapa Afrika Kusini. Nilikuja hapa nikionekana kama nina afya njema brother, lakini badaye kilichonitokea nilichungulia kifo. Namshukuru sana Mungu aisee. Nilipitia vipimo mbalimbali kabla ya operesheni, lakini madaktari walinishtua zaidi baada ya kuniambia kwamba operesheni yangu ilikuwa ngumu na nusu ilikuwa uhai huku nusu nyingine ikiwa ni kifo,” anasimulia Dimpoz.

Kwanini ilikuwa ngumu? Namuuliza Dimpoz ambaye amekuwa Afrika Kusini kwa mwezi mzima sasa na hajawahi kutoka nje zaidi ya kushinda ndani kutazama runinga na kunywa lundo la dawa alizoweka mezani karibu na kochi analokaa.

“Kilichotakikiwa katika operesheni ile madaktari waliniambia kwamba, kulikuwa na njia mbili za kunifanya nirudi katika hali ya kawaida. Kwanza ni kurekebisha mishipa ileile ya koo, lakini wakanionya kwamba baadaye hali ile ingeweza kujirudia.”

“Pili, wakaniambia njia nyingine ilikuwa ni kuhamisha njia ambayo ninaitumia katika kupitisha chakula. Hii ilionekana kuwa salama zaidi. Hata hivyo, ilikuwa operesheni ndefu sana. Awali, madaktari waliniambia ingechukua saa saba, lakini ikaja kuchukua saa 10.”

Dimpoz ananionyesha kidonda kikubwa kilichotokana na kuchanwa kwa tumbo lake kuanzia chini ya kifua hadi chini ya kitovu. Usitegemee kumuona Dimpoz aliye tumbo wazi kwa miaka mingi ijayo.

“Licha ya kunichana shingoni, lakini pia waliniachana sehemu kubwa ya tumbo kwa ajili ya kurekebisha. Kilichokuwa kinatakiwa kwanza ni kuhakikisha inapatikana njia ya muda ya kupitisha chakula wakati njia halisi inaondolewa. Lakini pia kuhakikisha njia mpya ya chakula inafanya kazi vema.”

Operesheni hii ilifanikiwa. Hata hivyo, kitu cha hatari zaidi ambacho kilimtokea Dimpoz ni kwamba alilazimika kukaa ICU (Chumba cha uangalizi maalumu) akiwa hajitambui kwa siku zaidi ya saba. Hakujua yupo ulimwengu gani. Anaamini kwamba ni Mungu ndio amemuokoa.

“Sikujitambua kwa zaidi ya siku saba. Nilikuwa nimewekewa nyaya katika kila kiungo changu. Nilikuwa napumulia mashine kusaidia mapafu yangu. Kila kitu kilitibuka na nilikuwa katika hali ya hatari,” anasimulia Dimpoz kwa sauti ya chini.

“Nilipozinduka sikujua nilikuwa wapi. Kwa jinsi ambavyo nilikuwa dhaifu sana, nilihisi kifo aisee. Jinsi ambavyo madaktari walivyonishughulikia nilikuwa naona kabisa , maisha yangu yapo hatarini sana,” anasema Dimpoz.

Je, Operesheni ya Ommy Dimpoz ilifanywa na daktari gani? Unafahamu kuwa iligharimu kiasi kikubwa cha pesa? ataendelea kuwa Afrika Kusini mpaka lini? Fuatana na kisa hiki cha kusikitisha katika Mwanaspoti kesho Jumanne.