Dar imehamia Tabata

Muktasari:

  • Siku za nyuma burudani nyingi za Jiji la Dar es Salaam ilizoeleka kwamba, zipo mitaa ya Kinondoni na Sinza. Huko imezoeleka kwamba muda wowote ndani ya saa 24 watu hawalali na chochote kile ambacho unakitaka unakipata.

KAMA hujawahi kufika Dar es Salaam kwa takribani mwaka mmoja uliopita, ukiingia sasa unaweza kuonekana mshamba. Achana na miundombinu ambayo imebadilika kwa kasi katika siku za hivi karibuni, ishu ya viwanja vya starehe kwa wapenda bata na yenyewe ina mabadiliko makubwa.

Siku za nyuma burudani nyingi za Jiji la Dar es Salaam ilizoeleka kwamba, zipo mitaa ya Kinondoni na Sinza. Huko imezoeleka kwamba muda wowote ndani ya saa 24 watu hawalali na chochote kile ambacho unakitaka unakipata.

Ndio maana yakaibuka maneno kama Sinza kwa wajanja, Kinondoni chuo kikuu. Lakini, tathimini na uhalisia wa hivi karibuni, vinaonyesha upepo umebadilika na kwamba, Kinondoni na Sinza licha ya kuwa bado zina sehemu za kujirusha lakini zimepoteza umaarufu na mpango mzima wa starehe za Dar es Salaam zimehamia Tabata.

Tabata ama Tbt ipo umbali wa dakika 30 kutoka kwenye stendi kuu ya mabasi Ubungo kama unaelekea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere na kwa sasa imekuwa zaidi ya eneo lolote la Dar es Salaam.

Zile nyama choma, ndizi choma, michemsho, makange, nyama pori na marostirosti pamoja na vinywaji vya kila aina ikiambatana na bendi za muziki wa dansi, klabu za disko kwa sasa zimehamia nyumbani, Tabata.

Kuna viwanja maarufu kama Forty Forty, Kwetu Pazuri, Toroka Uje, The Great Party, Mikasa, Casavega na Nay Pub pale maeneo ya Savanna. Ni baadhi ya maeneo ambayo yamekuwa na utitiri wa watu kutoka maeneo mengi ambayo hauwezi kulinganishwa na maeneo mengine ya Dar es Salaam kwa sasa.

Bendi kama Twanga Pepeta, FM Academia, Mapacha Watatu, Msondo Ngoma, Sikinde na nyingine zimehamishia burudani zao Tabata kutokana na ukweli kwamba, vijana wengi na wapenzi wa burudani wamehamia huko.

SABABU NI NINI?

Baadhi ya wadau wanasema aina ya vijana ambao miaka mitatu mpaka minne iliyopita walikuwa wakizichangamsha Sinza na Kinondoni na ambao, hawakuwa na majukumu sasa umri umewatupa mkono na wamelazimika kuhamishia makazi Tabata ambalo ni eneo tulivu zaidi kuishi na familia zao.

Lakini, wengine wanaeleza kuwa hata gharama za maisha kwa Tabata ni tofauti na maeneo yaliyoko karibu na mji kwani, Tabata ni rahisi kupata chumba au nyumba kwa bei rahisi na hata makazi yake ni tulivu na huduma za vyakula na mzunguko wa pesa ni mkubwa kama Sinza na Kinondoni ama Temeke.

Wengine wameeleza kuwa wanaojaza viwanja hivyo vya starehe vya Tabata ni wale wanaotoka maeneo ya jirani na huja kula bata. Lakini, uwekezaji wa wamiliki wa viwanja hivyo nao umetajwa kama kivutio kwani, wameajiri mabinti wenye mvuto na wanawalipa vizuri ambao, wanatambua kazi yao ya kutoa huduma bora.

Ramadhani Pentagone, huyu ni mwanamuziki wa bendi ya Ivory yenye makazi yake Mwananyamala anasema: “Sababu kubwa kabisa Kinondoni kukosa kumbi za burudani na watu wamezoea kumbi zilizolazimishwa toka zamani bendi kupiga, lakini hizo sio kumbi bali ni bar maarufu.

“Pia baa nyingi kwa sasa ni za viwango, ambapo Tabata inaongoza kwa bar nzuri na kumbi. Kinondoni hakuna kumbi zaidi ya vijisehemu maarufu na hii ni kutokana na kukosa maeneo,” alisema.

Naye Shomary Athumani alisema kwa mtazamo wake Kinondoni yote ni kama imepoteza ladha za kumbi.

“Kiukweli kwa sasa watu wengi wapenda burudani wako nje ya mji na Tabata au Temeke na Yombo, ni sehemu ambazo watu wengi walihamasika kupanga au kujenga nyumba zao.

“Kwa hiyo kwa wafanyabiashara hasa wa burudani waliona fursa ya kuwapelekea baa na kumbi nzuri za burudani ndiyo maana Tabata pako juu sana. Wamiliki wamejenga utaratibu wa wateja waliopo kuendelea kuwavuta wengine waishio mbali ili kuendeleza shangwe,” anasema Paschal Kinuka na kuongeza pia kwamba, jiji la Dar es Salaam limepanuka kwa kasi.

Cephas Martin, ambaye ni mdau wa muziki wa dansi anasema; “Huku kwingine watu wameshazoea burudani ni zile zile hata idadi ya kwenye hayo maeneo inazidi kuwa hafifu na jinsi mpangilio wa mji ulivyo maeneo ya Tabata, Yombo, Gongo la Mboto, Temeke yana ruhusu ujenzi wa sehemu mpya za burudani hata makazi hivyo watu wengi wamehamia sehemu hizo.”

ZAMANI ILIKUWAJE?

Kumbi kama Lang’ata (FM Club) na baadaye kuitwa Club Aset ni moja ya klabu zilizokuwa na umaarufu mkubwa tangu enzi za bendi kama Maquis Du Zaire, na vijana wote wa zamani walikuwa wanakutana hapo kufanya yao.

Pia, kumbi kama Vijana Social hall uliokuwa ukitumiwa na Vijana Jazz, Ukumbi wa Safari Resort wa Kimara uliokuwa uwanja wa nyumbani wa Orchestra Safari Sound (OSS) chini ya gwiji, Ndala Kasheba na akina King Kikii, ukumbi wa Muleba Bar Mabibo ambao bendi kama MCA International maarufu kwa mtindo wa Munisa Ndesa.

Kulikuwa na ukumbi wa Hotel 92 uliokuwa chini ya bendi ya Watunjatanjata na Motel Jasmina uliopo Kijitonyama ambao, ulikuwa nyumbani kwa bendi ya Bantu Group chini ya Mzee Hamza Kalala.

Kuna kumbi nyingi maarufu kama Mango Garden, Msasani Club, Gogo Hotel, Msasani Bay Villa, Tiger Motel, Bahari Beach Hotel, DDC Magomeni Kondoa, DDC Mlimani Social, Lango la Jiji, Friends Corner Hotel na Texas zote zimepoteza mvuto kabisa.

Ilala kulikuwa na kumbi maarufu kama Amana Club, Max Bar, Y2k, Afri Center, Mbowe, Ushirika, na DDC Kariakoo wakati Temeke kulikuwa na Imasco, Harbours Club, Highway Park za Kurasini, Omax Keko, Wapiwapi Chang’ombe, Temeke Stereo, Sugar Ray, Kisuma baa na DDC Keko ambazo zilikuwa zinatamba kwelikweli. Kinondoni pia imeongoza kwa kuwa na bendi nyingi za muziki wa dansi, taarab na disko kulinganisha na maeneo mengine ya jiji. Sinza katika siku za hivi karibuni kumekuwa baa maarufu ambazo zimepoteza mvuto wake kwa kasi na kubaki na majina tu.