Tulieni, mambo mazuri yanakuja Simba

Muktasari:

  • Mashabiki hao wamenuna kutokana na kuishuhudia timu yao ikilitema taji la FA ililokuwa ikilishikilia tangu Mei, mwaka jana, kisha kufurushwa mapema katika Kombe la Mapinduzi.

SIMBA asubuhi ya jana imelikimbia Jiji la Dar es Salaam na kujichimbia Morogoro kuweka kambi ya maandalizi ya mechi yao ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Singida United, lakini huku mashabiki wake wamenuna.

Mashabiki hao wamenuna kutokana na kuishuhudia timu yao ikilitema taji la FA ililokuwa ikilishikilia tangu Mei, mwaka jana, kisha kufurushwa mapema katika Kombe la Mapinduzi.

Kinachowatia hofu zaidi ni sintofahamu ya wachezaji na benchi la ufundi kwa jinsi walivyochuniana Uwanja wa Amaan, Unguja na hata walipotua jijini kutoka visiwani, lakini kumbe Kocha Masudi Djuma, ameshtukia mchezo.

Djuma amenong’onezwa namna mashabiki wa klabu hiyo walivyopaniki na kisha kwa kujiamini akatamka; ‘Wana Simba watulie, mambo mazuri yanakuja’.

Djuma alisema kuwa, hali ndani ya kikosi chake ni shwari na kusisitiza kuwa kuna jambo moja tu likamilike Simba kabla ya kuanza kusherehekea mafanikio na hasa kutupia nyavuni katika mechi watakazocheza.

MSIKIENI WENYEWE

Akizungumza na Mwanaspoti muda mchache kabla ya kusepa zao Morogoro, Djuma alisema kwa sasa timu yake inacheza soka tamu kinoma na kutengeneza nafasi za kufunga. Hata hivyo, amesema tatizo ni utulivu wa vijana wake wanapokuwa mbele ya lango na ameanza kulipatia ufumbuzi ili wakirejea wafanye makubwa kuwapa raha mashabiki wa Msimbazi.

“Napenda mfumo wa kushambulia zaidi na ndio mfumo wangu na hauwezi kuwa sawa kwa wiki mbili nilizokaa na timu kwani, unachukua muda kuuzoea.

“Mwanzo tulicheza ila hatupati nafasi nafasi za kufunga tofauti na sasa, tunatengeneza nafasi nyingi ila tatizo ni utulivu katika kumalizia na hili litaisha hivi karibuni,” alisema Djuma.

Djumba (40) aliyetoka kuipa Rayon Sports ubingwa wa Rwanda, alisema;

“Ukipanga wachezaji ambao, hawakuwa wakipata nafasi ya kucheza basi hutaka kuonyesha mambo mengi ili kutambulisha uwezo wao hivyo kukosa utulivu, ila hili litaisha tu.”

NIDHAMU

Kuhusu nidhamu alisema baada ya kuwepo kwa madai ya baadhi ya nyota walionyesha utovu katika Kombe la Mapinduzi na Simba kutolewa hatua ya makundi, kwa sasa kila kitu kipo sawa baada ya kukaa na kuzungumza na vijana wake.

“Kwanza mawasiliano ndani ya timu ni mazuri tofauti na hali nilivyoikuta wakati nafika hapa, kulikuwa na makundi kikosini, wapo waliojiona zaidi ya wengine kiasi cha kuchagua wachezaji wa kucheza nao. Nimejitahidi kuliondoa hilo kwa kuweka usawa katika kutumia mifumo mipya ya upangaji kikosi ili kila mmoja acheze.

“Napenda zaidi majadiliano nikiona jambo haliendi sawa, ila linapojirudia ndipo huchukua hatua kali kwani, tayari tumejadiliano hapo awali na kukubaliana wote.”

Ufanunuzi wa Djuma umekuja kutokana na mjadala uliozuka kwa kile kilichoonyeshwa na Shiza Kichuya, Jonas Mkude na Nicholous Gyan kususa kukaa benchi walipotolewa na kuwenda jukwaani walipolala bao 1-0 dhidi ya URA ya Uganda.

Kaimu Rais wa Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ alikaririwa juu ya suala hilo la utovu wa nidhamu kwa kusema; “Taratibu zipo za kuchukua dhidi ya wachezaji wasiokuwa na nidhamu, hivyo, tunalifanyia kazi ili kujua zaidi ndipo tutachukua hatua stahiki.”