Spurs, Arsenal waipasua Wembley

Muktasari:

Macho katika mchezo huo yatakuwa kwa Harry Kane wa Spurs na Aubameyang wa Arsenal

London, England. Jiji la London litasimama kwa dakika 90 wakati Tottenham Spurs watakapoikaribish Arsenal ‘kitu cha London derby’  kitapigwa kesho mchana Jumamosi kwenye Uwanja wa Wembley.

Arsenal itakwenda kumenyana na mahasimu wao Tottenham, ambao kiungo wao kutoka Kenya, Victor Wanyama yupo kwenye kiwango bora kweli kweli.

Ni mwendo wa kutishana tu, lakini wengi wanaamini London derby ya safari hii vita itakuwa kwenye kiungo, ambapo upande wa Arsenal kutakuwa na Jack Wilshere, Granit Xhaka, Mesut Ozil na Henrikh Mkhitaryan, wakati kwa wenyeji wa Wembley, Spurs watakuwa na Wanyama, Mousa Dembele, Dele Alli na Christian Eriksen.

Kocha, Arsene Wenger anayetamba na staa wake mpya, Pierre-Emerick Aubameyang, ambaye amepiga Spurs Bao Nne katika mechi nne alizocheza dhidi yao, itakuwa mechi yake ya kwanza kwenye London derby, lakini kocha huyo Mfaransa amewapiga vijembe wachezaji wa Spurs kwamba, wanaongoza kwa kujiangusha.

 Mkhitaryan juzi Alhamisi alibaki mazoezini kivyake alipokuwa akijifua kuhakikisha anakwenda kuweka muunganiko mzuri na Aubameyang kuendeleza mambo matamu baada ya mechi moja tu walioyocheza pamoja Arsenal kupiga mtu 5-1, walipoipiga Everton wikiendi iliyopita.

Lakini, Spurs inayotambia uwezo wa straika wao Harry Kane watashuka Wembley wakiwa na kumbukumbu ya kushinda mechi yao iliyopita kwenye ligi dhidi ya kigogo, walipoizabua Man United 2-0.

Kocha Mauricio Pochettino hawana wasiwasi hasa ukizingatia kwamba, anaamini kikosi chake kipo fiti hasa baada ya kurejea kwenye kikosi Wanyama, ambaye kwenye mechi dhidi ya Liverpool alipiga bonge la bao, ambalo limekuwa gumzo kwa wiki nzima katika kuelekea London derby.

Vinara wa Ligi Kuu England, Man City wao watakuwa nyumbani kuwakaribisha Leicester City, wakati Manchester United watasubiri hadi Jumapili watakapomenyana na Newcastle United ugenini.

Mechi nyingine za kesho Jumamosi, Huddersfield watacheza na Bournemouth wakati Southampton watakuwa wenyeji wa Liverpool.

Chelsea watasubiri hadi Jumatatu watakapokipiga na West Brom huko Stamford Bridge, wakati Jumamosi nyingine itakuwa Everton na Crystal Palace, Stoke City na Brighton, Swansea City na Burnley na West Ham watakipiga na Watford.