Vodacom kuijaza manoti Yanga

Meneja uhusiano wa kampuni ya Vodacom, Matina Nkurlu.

Muktasari:

Meneja uhusiano wa kampuni ya Vodacom, Matina Nkurlu alisema wanayofurahi ligi ukimalizika kwa ushindani mkubwa.

Dar es Salaam. Mabingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara, Yanga watakabidhiwa zawadi zao Jumatano hii jijini Dar es Salaam.

Yanga imetwaa ubingwa wake wa 27 msimu huu baada ya kufikisha pointi 68, sawa na Simba lakini wakitofautiana kwa mabao ya kufunga na kufungwa.

Wadhamini wa ligi hiyo Kampuni ya mawasiliano ya Vodacom Tanzania PLC inatarajia kutoa zawadi kwa washindi mbalimbali ya Ligi Kuu Bara kwa msimu huu.

Meneja uhusiano wa kampuni ya Vodacom, Matina Nkurlu alisema wanayofurahi ligi ukimalizika kwa ushindani mkubwa.

“Tunaipongeza Yanga pamoja na mshindi wa pili Simba na Kagera Sugar iliyomaliza na ya tatu, ligi ilikuwa na msisimko pamoja na ushindani mkubwa.”

Nkurlu aliongeza, “Waswahili husema chanda chema huvishwa pete, tunapenda kuwatangazia wadau wa soka na timu zilizoshiriki ligi kuu kuwa tarehe 24, Jumatano tutakuwa na sherehe kubwa itakayofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Mlimani City ya kukabidhi zawadi yao mabingwa.

"Pamoja na mabingwa, timu nyingine zilizoshiriki zitazawadiwa zawadi mbalimbali kwa kuwa zawadi zao zipo tayari pia kamati Maalum iliyoundwa kusimamia tuzo hizi imefanya mabadiliko kiasi kwa kuongeza baadhi ya tuzo ambazo hazikuwepo msimu uliopita lengo ikiwa ni kuboresha tuzo hizi."

Tuzo zilizoongezwa ni: Tuzo ya Heshima (ambayo itatolewa kwa mwanasoka nguli wa zamani mwenye historia nzuri kwa soka la Tanzania).

Alisema Vodacom Tanzania mwaka huu imetoa zawadi mapema kwa kuwa ni utaratibu wa kawaida kwa kampuni hiyo kukabidhi zawadi mara tu baada ya msimu wa ligi kwisha.

“Uchelewaji wa kutoa zawadi hutokana na sababu mbali mbali ambazo zinakuwaga nje ya uwezo wao ikiwamo baadhi ya timu kuwa zinashiriki mashindano mengine kama Kombe la Shirikisho Barani Afrika. Sababu nyingine ni pamoja na mfungo wa mwezi mtuku wa Ramadhani,” alieleza Meneja Uhusiano huyo.