Tambwe afichua njama za Simba

Thursday April 20 2017

 

By Khatimu Naheka

YANGA wanaanza tizi leo Alhamisi kwa ajili ya kujiandaa na mechi yao ya robo fainali ya Kombe la FA dhidi ya Prisons. Lakini Amissi Tambwe amewaambia Yanga kwamba kama wakikubali kuendelea kuchezewa akili na Simba watatema ubingwa wao na watapoteza thamani yao mbele ya mashabiki.

Tambwe amewaambia Yanga kwamba Simba wanachofanya kwa sasa ni kuwatoa kwenye mstari kwa kuwapa presha ya mambo mengi ikiwemo pointi za mezani, hivyo amewasisitiza waache kuelekeza akili zao kwa Simba, haitawasaidia.

Raia huyo wa Burundi ambaye anakubalika kwa viongozi wa Simba, alisema amegundua kutoka kwenye vyanzo vyake vya uhakika kwamba Simba wanapambana usiku na mchana kutaka kuwa mabingwa ambapo endapo Yanga itafanya makosa ya kushindwa kutengeneza utulivu na umoja ndani ya timu yao, itakula kwao.

Staa huyo amewasisitiza Yanga kwamba watulize mguu uwanjani na kucheza soka kutafuta pointi zao na muhimu zaidi wapige bao nyingi ili kukwepa mtego wa kulingana na Simba kwenye matokeo ya mwisho wa msimu.

Kama Simba ikipewa pointi za rufaa iliyokata dhidi ya Kagera Sugar na akishinda mechi zilizosalia ataishia kwenye pointi 71 ambazo Yanga wakishinda michezo yao yote pamoja na viporo watakomea hapohapo.

“Unajua Simba msimu huu wanataka ubingwa kwa njia yoyote, sasa kama Yanga tukiendelea kufuatilia hili sakata lao, litatumaliza Yanga umoja ndani ya timu yetu kwa sasa ili tumalize ligi kwa kishindo,” alisema Tambwe.

“Jingine kwa sasa kama tukishinda mechi zetu mbili ina maana tutapanda juu ya msimamo kwa tofauti ya mabao ambayo sasa tutatakiwa kuongeza kufunga mabao zaidi ili tusisogelewe na Simba nafurahi kuona wenzangu wamepona, lakini pia uongozi ujue jinsi ya kuboresha motisha katika mechi hizi zilizosalia ili tusitetereke.”

Yanga ipo nafasi ya pili nyuma ya Simba yenye pointi 62 (zikiwamo tatu ilizopewa kwa rufaa yao ya Kagera Sugar).

Yanga ina pointi 56 ila ina uwiano mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa japo wana michezo miwili mkononi.