Simba yapata upenyo mwingine

Muktasari:

Kamati ya Sheria, Katiba na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), imechukua zile pointi tatu za Kagera Sugar ilizokuwa imepewa Simba na ile Kamati ya Saa 72, lakini wao wala hawashtuki, kwani wana upenyo mwingine wa kuweza kutwaa ubingwa kiulaini.

HESABU za Simba bado zinaruhusu. Bado haijafa kwenye mbio zake za kusaka ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu.

Wababe hao wa Msimbazi wamepata upenyo mwingine baada ya kuchungulia kwenye hesabu za pointi na kuona kumbe inawezekana.

Kamati ya Sheria, Katiba na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), imechukua zile pointi tatu za Kagera Sugar ilizokuwa imepewa Simba na ile Kamati ya Saa 72, lakini wao wala hawashtuki, kwani wana upenyo mwingine wa kuweza kutwaa ubingwa kiulaini.

Ishu nzima ni hesabu tu. Simba kwa sasa ndiyo vinara, wakiwa na pointi 59, tatu zaidi ya Yanga. Kwenye ligi, Simba imebakiza mechi tatu, Yanga ikisaliwa na tano. Kwa maana hiyo, Simba ikishinda mechi zote zilizobaki, itaongeza pointi tisa, wakati Yanga ikishinda zake zote itazoa jumla ya pointi 15.

Kwa hesabu za hapo juu, ina maana Yanga kutwaa ubingwa ni lazima ishinde mechi zote zilizobaki kama Simba watakuwa wameshinda za kwao zote. Hapo kutakuwa na pengo la pointi tatu, faida itakuwa kwa Yanga.

Lakini sasa, Yanga haipaswi kupoteza pointi hata kwa sare tu, kwani ikipata sare mbili tu katika mechi zake zilizobaki, Simba bingwa. Kwani Yanga itakuwa  imemaliza ligi na pointi 67, moja nyuma ya zile ambazo zitakazovuna na Simba. Kwa hesabu hiyo, ndio maana viongozi wa Simba wanacheka tu, wanaamini sare mbili kwa Yanga inawezekana. Yanga imebakiza mechi zake dhidi ya Kagera Sugar, Toto Africans, Mbeya City, Prisons na Mbao FC ambao itawafuata jijini Mwanza.

LakiniSimba wao kwenye pointi hizo 15 inazozisaka Yanga, wao wanaombea wapoteza nne tu, zinawatosha kuubeba ubingwa.

Mechi za Simba zilizobaki ni dhidi ya Mwadui, Stand United na African Lyon ambapo kama watashinda zote bado watakuwa kwenye njia sahihi ya ubingwa. Hata hivyo Simba italazimika kushinda kila mchezo kwa mabao angalau manne ili ikitokea Yanga imepoteza mchezo mmoja waweze kutwaa ubingwa kwa tofauti ya mabao.

Yanga ndiyo inayoongoza kwa mabao ikiwa imefunga mabao 50, sita zaidi ya Simba ambayo maamuzi ya jana imeifanya kusaliwa na mabao 44.

HUKUMU YENYEWE

Akisoma hukumu ya Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji, Katibu Mkuu wa TFF, Celestine Mwesigwa alisema kamati imeamua kuzirejesha pointi Kagera baada ya kubaini mapungufu katika hukumu ya Kamati ya Saa 72.

Miongoni mwa mapungufu yaliyotajwa ni rufaa ya Simba kuwasilishwa nje ya muda, rufaa kutokidhi vigezo pamoja na kikao cha Kamati ya Saa 72 kuhusisha wajumbe ambao hawaruhusiwi kuhudhuria kikao hicho.

“Kamati imebatilisha hukumu ya Kamati ya Saa 72 baada ya kugundua mapungufu ya rufaa hiyo ambapo iliwasilishwa nje ya muda lakini pia haikukidhi vigezo,” alisema Mwesigwa.

“Wapo baadhi ya watendaji wa Bodi ya Ligi Kamati imejiridhisha waliipotosha kamati ya saa 72, hivyo imependekeza wapelekwe kamati ya maadili kujadiliwa,” alifafanua.

Hata hivyo Makamu wa Rais wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ alisema wanasubiri kupata hukumu hiyo wajue cha kufanya, lakini akisisitiza kuwa kamati inapaswa kuuthibitishia umma je Mohammed Fakhi alikuwa na kadi tatu za njano au la.