Simba inatawala Yanga ikiwepo

Muktasari:

Hadi leo hii unaposoma hapa Simba imefikisha siku 31 kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu wakati ambao Yanga haijasafiri na ipo mjini imejaa tele. Yanga inajikongoja katika nafasi ya tatu na pointi 15.

KUNA kausemi kalikuwa kanazunguka kwenye mitandao ya Kijamii kuwa ukisikia Simba anaongoza Ligi ujue Yanga haipo mjini, sasa usemi huo umegeuka baada ya Simba kuwafanyia kitu mbaya watani zao hao na kuongoza ligi wakati wakiwa mjini.

Hadi leo hii unaposoma hapa Simba imefikisha siku 31 kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu wakati ambao Yanga haijasafiri na ipo mjini imejaa tele. Yanga inajikongoja katika nafasi ya tatu na pointi 15.

Simba ilipanda kileleni mwa msimamo wa Ligi Septemba 17 baada ya kuifunga Azam bao 1-0 kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam na tangu hapo haijashuka hivyo kutimiza idadi ya siku 31 huku wapenzi wa timu hiyo wakitamba kuwa huo ni mwendo mdundo mpaka ubingwa.

Mbeya City ilianza kwa kuongoza Ligi kwa siku saba kabla ya kushushwa na Azam Septemba 10 kwa kipigo cha mabao 2-1. Hata hivyo Azam iliongoza ligi hiyo kwa siku saba tu na kushushwa na Simba inayoongoza mpaka sasa wakati Yanga haijaonja hata nafasi ya pili.

Hata hivyo Simba bado haijafikia rekodi ya kukaa kileleni kwa muda mrefu ambapo ilifanya hivyo msimu uliopita kwa kukaa siku 36 ambapo ilikuwa kati ya Machi 10 baada ya kuifunga Ndanda mabao 3-0 hadi Aprili 16 ambapo ilishushwa na Yanga iliyoifunga Mtibwa Sugar bao 1-0 katika mechi ya kiporo.

 

HALL NOMA

Rekodi za kocha wa zamani wa Azam, Stewart Hall zinaonekana kumtesa kocha Mhispania, Zeben Hernandez ambaye katika mechi tisa ameshuhudia timu yake ikikusanya pointi 12 na kushuka hadi nafasi ya saba ambayo ndiyo mbaya zaidi kushikwa na Azam katika kipindi cha miaka sita iliyopita.

Hernandez ameiongoza Azam kushinda mechi tatu tu kati ya tisa za msimu huu huku akifungwa mara mbili na kupata sare nne. Azam haijapata ushindi wowote katika mechi zake tano za mwisho.

Msimu uliopita Azam ikiwa chini ya Hall ilishinda mechi nane kati ya tisa za mwanzo na kupata sare moja hivyo kukusanya pointi 25 idadi ambayo Azam hata wakizidisha mara mbili pointi zao za sasa hawaifikii. Msimu huo Azam ilikuwa ikichuana na Yanga kileleni.