Rage: Mkutano halali, Wadhamini: Wee..thubutu

Aden Rage

MWENYEKITI wa zamani wa Simba, ambaye mashabiki wa klabu hiyo wanamuaminia kwa kutafsiri kanuni na sheria, Ismail Aden Rage ameunga mkono mkutano mkuu ulioitishwa na Rais Evans Aveva lakini Baraza la Wadhamini wa klabu hiyo chini ya uenyekiti wa Mzee Hamis Kilomoni limeweka ngumu na kusema ngoma haifanyiki.

Simba imepanga kufanya mkutano mkuu wa dharura Desemba 11 katika Ukumbi wa Bwalo la Polisi, Oysterbay, Dar es Salaam na moja ya ajenda ni kujadili mabadiliko ya katiba hasa mfumo wa uendeshaji baada ya Bilionea Mohammed Dewji ‘Mo’ kutaka kuwekeza Sh 20 bilioni ili amiliki hisa asilimia 51.

“Tulichoamua wadhamini ni kwamba si busara kuwaachia maamuzi ya Simba wanachama wachache wanaopenda mpira wamiliki klabu, tumeomba vyombo vya michezo vya serikali kuingilia mgogoro huu kwa usalama wa nchi yetu, tayari tumepeleka maombi kwa mkuu wa mkoa kusimamisha mkutano huo,” alisema.

“Hatujatushirikishwa, mambo mengi yanakwenda kinyume na katiba. Viongozi wajipange upya wafuate taratibu zote ndipo waitishe mkutano, watushirikishe sisi kujua jambo litakalojadiliwa,” alisema.

 

Mo atua kwa Kilomoni

“Mo alikuja hapa kwangu na tulizungumza mengi hususani lengo lake la kutaka kuwekeza Simba, sipingani na wazo hilo ila lazima taratibu zifuatwe. Nilimwelekeza cha kufanya na kumpa tahadhari asijaribu kusaini jambo lolote ndani ya Simba kabla hili suala halijajadiliwa na kukubaliwa atapoteza haki zake, kama kuna nyaraka amesaini ataelewa baadaye.

“Hivyo natarajia viongozi wakifuata taratibu ndipo mkutano utaitishwa, wakifuata taratibu za mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji suala la kuwekeza litajadiliwa pia maana si lazima awe Mo. Na atakayewekeza asitarajie atakabidhiwa na hati ya jengo, hapana na asilimia 51 nazo si rahisi,” alisema.

 

Msimamo wa Rage

“Kwa mujibu wa Katiba ya Simba, Rais kwa mamlaka yake akishirikiana na kushauriana na Kamati ya Utendaji kuitisha Mkutano. Hivyo hata mkutano ulioitishwa na klabu sioni tatizo, ni halali,”alisema Rage alipohojiwa na kituo cha redio cha EFM, jana Ijumaa Asubuhi.

“Kuhusu Mzee Kilomoni kupingwa na baadhi ya wanachama, siwezi kusema lolote namheshimu sana ni mkubwa wangu, mzee wangu na utanionea kama nitaamua kujibu yanayomhusu sitaki kumvunjia heshima, hata kama kakosea siwezi kumkosoa hadharani,” alisema Rage.

Chuma Suleiman ‘Bi Hindu’ alimuunga mkono Mzee Kilomoni: “Mkutano si halali hata mabadiliko hayalengi kuisaidia Simba, ila kuleta mabadiliko kwa viongozi na wanaolilia mabadiliko hayo. Bodi ya wadhamini inapuuzwa viongozi wanatupachikia watu tofauti, sijui wamempa Hassan Dalali na wengine, wamempuuza Mzee Kilomoni anayeijua Simba nje ndani...mkutano unaoitishwa kwa sababu ipi.”