Msuva anawasikia mnachosema

SIMON Msuva anashangazwa na maneno ya watu kuwa amekosa tuzo ya Mchezaji Bora kutokana  kitendo cha kugongana na mwamuzi, Ludovick Charles, wakati wa mchezo  wa mwisho wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Mbao.

Katika mchezo huo, Msuva alionyeshwa kadi ya njano baada ya kudaiwa kumsukuma mwamuzi pamoja na wachezaji wenzake dakika ya 76 wakipinga mwamuzi Ludovick kutowapa penati baada ya Obrey Chirwa kuangushwa na kipa eneo la hatari.

Msuva alikuwa anawania tuzo hiyo sambamba na  Mohammed Hussein ‘Tshabalala wa Simba na Aishi Manula wa Azam. Tuzo hiyo sasa imetua kwa Tshabalala.

Msuva alisema yeyote anaweza kupata tuzo kutokana na vigezo na amempongeza Tshabalala kwa kuchukua tuzo hiyo mwaka huu.

“Unapomzungumzia Msuva ujue kila mmoja anamwangalia na watu wanasema kuwa nimekosa uchezaji bora kwa sababu ya lile tukio la  mwamuzi katika mchezo dhidi ya Mbao, lakini sidhani kama ni sahihi uchezaji bora ukahusishwa na hayo mambo,” alisema.

“ Kwanza siku ile mwamuzi hakupigwa wala kufanyiwa vurugu, tulimfuata  kwa lengo la kutoa malalamiko yetu kuhusiana na maamuzi yake, lakini  kwa sababu mimi nilionekana na nikapewa kadi ndio maana  umekuwa mjadala mkubwa.”

Msuva alisema kukosa tuzo hiyo hakumvunji moyo kwani kuna mwongezea kasi ya kupambana zaidi ili kupata tuzo nyingine zijazo za ndani na hata nje ya nchi.