Fabregas asimulia ya mwakani

Wednesday May 17 2017

 

By London,England

       KIUNGO, Cesc Fabregas, amesema ni jambo la wazi kabisa Chelsea itakuwa na wakati mgumu msimu ujao.

Kiungo huyo amekuwa na msaada mkubwa katika kikosi cha Chelsea kwa msimu huu na kufanikiwa kubeba ubingwa wa Ligi Kuu England, taji ambalo Fabregas anaamini ni bora zaidi duniani.

Katika ushindi wa juzi Jumatatu, kiungo huyo Mhispaniola alifunga bao la ushindi dakika za mwishoni wakati Chelsea ilipoichapa Watford 4-3 katika Uwanja wa Stamford Bridge na hivyo kushinda mchezo wao wa 29 kwa msimu huu.

Dhamira ya Chelsea ni kuweka rekodi ya kushinda mechi 30 kwenye Ligi Kuu msimu huu.

“Ubingwa una raha yake. Nimecheza Hispania, nimetazama mechi nyingi sana Ujerumani, Ufaransa na Italia, nadhani England ni ligi bora kabisa duniani na ndiyo maana inapaswa kuwa na wachezaji bora. Kwenye ligi hii, unafungwa na yeyote,” alisema Fabregas.

“Msimu ujao utakuwa mgumu sana. Tutakuwa na kazi kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, hivyo yatupasa kupandisha kiwango chetu tuweze kushindana kote kote na kwenye Ligi Kuu England.”