Bravo Serengeti, Kilimanjaro Queens fanyeni kweli

Muktasari:

Serengeti ikiwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam iliifunga Congo mabao 3-2 katika mechi ya raundi ya tatu ya kuwania kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa timu za Vijana zitakazofanyika mwakani, Madagascar.

JUZI Jumapili ilikuwa ni siku ya furaha sana kwa mashabiki wa soka wa Tanzania baada ya timu za Taifa za Vijana U17, Serengeti Boys na ile ya Wanawake ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Queens kufanikiwa kupata ushindi muhimu katika michezo yao.

Serengeti ikiwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam iliifunga Congo mabao 3-2 katika mechi ya raundi ya tatu ya kuwania kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa timu za Vijana zitakazofanyika mwakani, Madagascar.

Wakati vijana hao wakiwatoa kimasomaso Watanzania katika mchezo huo na sasa wakisalia kwenda kumaliza kazi mjini Brazzaville, Congo katika mechi ya marudiano wiki mbili zijazo, dada zao Kili Queens waliwanyoosha wenyeji wao timu ya taifa ya Uganda kwa mabao 4-1 kwenye mchezo wa nusu fainali ya michuano ya Kombe la Chalenji.

Kili jioni ya leo itakuwa na kibarua cha kuweka rekodi ya kutwaa taji la michuano hiyo kwa mara ya kwanza kwa kuvaana na Kenya ambao waliing’oa Ethiopia kwa mabao 3-2 katika nusu fainali nyingine iliyochezwa juzi mjini Kampala, Uganda.

Imani ya wengi ni kwamba wawakilishi wetu hao watafanya kweli kwa kuhakikisha wanapata ushindi kwenye mchezo huo unaotarajiwa kuwa mkali dhidi ya Harambee Starlets ili kubeba taji hilo kwa mara ya kwanza ikiwapokea ndugu zao Zanzibar Queens.

Zanzibar ambao waliondoshwa kwenye michuano hiyo kwa aibu kwa kukandikwa jumla ya mabao 30-1 kupitia michezo yao mitatu, ndio iliyokuwa watetezi wa taji hilo baada ya kulitwaai miaka 30 iliyopita mnamo mwaka 1986 michuano ilipoasisiwa.

Tunaamini wawakilishi wetu hao watapambana ili kulirejesha taji hilo katika ardhi ya Tanzania kwa mara nyingine tena kwa sababu tunawaamini wachezaji wetu wanajua kiu ya Watanzania kwa michuano ya kimataifa.

Kwa miaka mingi Tanzania imekuwa na bahati mbaya ya kufanya vema kwenye michuano ya kimataifa inayoshiriki kuanzia ngazi za klabu mpaka timu za taifa, hivyo nafasi iliyopata katika michuano ya Chalenji sio ya kuiacha ipotee hivi hivi.

Kitu cha muhimu ni kuwaombea dua njema na wachezaji wetu kujituma kwa kila dakika za mchezo huo uwanjani, ili mwishowe tufarijike kwa kurejea na ubingwa nyumbani.

Kwa upande mwingine, kazi kubwa iliyofanywa na Serengeti Boys mpaka sasa katika michuano inayoshiriki kwa hakika inahitaji pongezi za dhati, ingawa wachezaji wake hawapaswi kubweteka kwani kazi iliyopo mbele yao ni kubwa zaidi.

Ushindi wa mabao 3-2 ni mkubwa, lakini unaiweka timu hiyo katika hatari kubwa ya kukwama kufuzu fainali za mwakani kama hawataenda kupambana kiume ugenini.

Mwaka 2012 Congo tuliwafunga hapa nyumbani bao 1-0 katika hatua kama hiyo kwa ajili ya kuwania fainali za Afrika za mwaka 2013, lakini tulipoenda kwao tulipoteza mchezo kwa mabao 2-0 na hivyo kutolewa kwa mabao 3-1.

Mwanaspoti haina nia ya kuikatisha tamaa timu yetu, lakini kwa jinsi Congo walivyopambana na kujipatia mabao hayo mawili ugenini huenda yakawapa jeuri zaidi, ndio maana tunataka Serengeti Boys ijiandae mara mbili na maandalizi ya awali.

Mchezo ujao ni mgumu zaidi kwa vile watakuwa ugenini kwenye nchi ambayo mwaka 2012 waliifanyia sivyo ndivyo vijana wetu wa Serengeti Boys kipindi hicho na kupata ushindi kwao wa mabao 2-0, pia ikumbukwe mabao mawili waliyopata juzi ni faida kubwa kwao.

Hivyo ni lazima vijana wetu waandaliwe kisaikolojia na mbinu zaidi za kuhakikisha wanaenda kupata ushindi mwingine ugenini ama kulazimisha sare na katu isiruhusu kufungwa kwani kama ikifunga bao 1-0 safari ya Serengeti itakuwa imeishia njiani.

Tunawaamini vijana wetu na jopo lao la makocha chini ya ‘Mchawi Mweusi’, Bakar Shime, ila tunasisitiza tusiridhike na matokeo ya juzi na kudhani tayari tumeshafuzu ni lazima tukapambane maradufu ugenini ili Tanzania iende Madagascar.

Kwenda kwenye fainali hizo sio heshima kwa Tanzania, lakini kwa vijana waliojitoa na kupambana mwanzo mwisho kwenye hatua ya awali mpaka walipofikia itakuwa ni heshima kubwa na kujitangaza ndani na nje ya nchi kama mashujaa wa taifa.

Tanzania hatujawahi kucheza fainali kama hizo kwani mwaka 2004 licha ya Serengeti Boys kufuzu kwa kuing’oa Zimbabwe, lakini ilichongewa na kung’olewa kwa kosa la kufanya udanganyifu wa mmoja wa wachezaji wake na kuadhibiwa na Shirikisho la Soka la Afrika (Caf).

Shime Watanzania tuendelee kuiunga mkono timu yetu kwa hali na mali ili Oktoba 2 ikamalize kazi mjini Brazzaville kwa kuamini nia, nguvu na sababu ya kufanya hivyo wanayo,.

Tuna kila sababu ya kufuzu kwa kuwa tuna kikosi kizuri. Tunaiombea kila la heri Serengeti na tunaiombea dua nje Kili Queens vilevile.