Bossou ajirudisha Yanga, usajili wafungwa

Beki wa Yanga, Vicent Bossou

Muktasari:

Mchezaji huyo atachukua nafasi ya Mbuyu Twite ambaye Mwanaspoti linajua kwamba wikiendi iliyopita Pluijm na Katibu Mkuu wa Yanga, Baraka Deusdedit walimuita wakamwambia sasa ni mchezaji huru anaweza kutafuta timu nyingine.

HANS Pluijm siku hizi akienda kwenye mazoezi Yanga anakaa pembeni tu anaangalia mavitu ya George Lwandamina. Kocha huyo Mzambia tayari ameshafanya usajili mmoja wa kiungo mkabaji, Justine Zulu ambaye ni raia wa Zambia.

Mchezaji huyo atachukua nafasi ya Mbuyu Twite ambaye Mwanaspoti linajua kwamba wikiendi iliyopita Pluijm na Katibu Mkuu wa Yanga, Baraka Deusdedit walimuita wakamwambia sasa ni mchezaji huru anaweza kutafuta timu nyingine.

Usajili wa pili wa Lwandamina ilikuwa ni straika Mzambia anayecheza Congo Brazaville, Winston Kalengo lakini ilishindikana wiki iliyopita baada ya Wakongo hao kumuwahi na kumtia noti alizoshindwa kuzikataa.

Kocha huyo ambaye ana akiba kubwa ya wachezaji kwenye mafaili yake kutokana na uzoefu wake na soka la Afrika, aliamua kuanza mazungumzo mara moja na straika mwingine mahiri ambaye alimwambia yuko tayari anawasikiliza Yanga tu wamwabie wanampa bei gani.

Ila ghafla juzi akabadili tena mawazo na kukata jina la straika huyo, baadaye akawaambia viongozi anataka kusajili beki wa maana kutoka nje atakayeimarisha safu la ulinzi baada ya kuona kila dalili kwamba Vincent Bossou ataondoka.

Lakini jana Jumatatu Bossou akiwa Dar es Salaam alimpigia simu Lwandamina na kumwambia anarudi kufanya kazi baada ya dili lake kushindikana. Hivyo kocha huyo amewaambia viongozi hatafanya tena usajili mpya kama Bossou atarudi kwani haoni tena sababu.

Habari za ndani ambazo Mwanaspoti imezipata ni kwamba mchezaji huyo alikuwa akitikisa kiberiti ili Yanga wamtulize lakini walipomwambia unaweza kwenda akanywea. Lwandamina ambaye amekuwa makini mno mazoezini na wachezaji wameanza kuzoea aina ya utendaji ambayo ni ya umakini na kwenda na muda kwa kila jambo.

“Tunahitaji kuboresha safu ya ulinzi sidhani kama tutatafuta mshambuliaji kwasasa,’’ alisema.