Yanga, Mbao watikisa Bunge

Muktasari:

Yanga ilifika bungeni  asubuhi wakiwa na kombe walilolitwaa mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya kufikisha pointi 68, sawa na Simba wakitofautiana kwa mabao.

Dodoma. Bunge lilisimamisha shughuli  kwa muda kuwashangilia mabingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara,Yanga walipofika bungeni kwa mwaliko Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira, Kazi, Vijana na Wenye Ulemavu, Antony Mavunde.

Yanga ilifika bungeni  asubuhi wakiwa na kombe walilolitwaa mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya kufikisha pointi 68, sawa na Simba wakitofautiana kwa mabao.

Mbali na Yanga, timu nyingine iliyotembelea Bunge ni Mbao Fc ya Mwanza ilitinga bungeni ikiongozwa na kocha Ettiene Ndaliyagile.

Yanga iliingia bungeni saa 9:40 asubuhi  wakati wa kipindi cha maswali na majibu na kumlazimu Mbunge wa Viti Maalum (Chadema)

Aida Kenani aliyekuwa akiuliza swali la nyongeza kusimama kwa muda kupisha wabunge waliokuwa wakishangilia kwa kupiga makofi na vifijo.

Mara baada ya kuingia Wabunge hao walianza kupiga makofi ambapo aliyekuwa akiongoza kikao hicho  Mwenyekiti wa Bunge,Najma Maftah Giga aliwataka wabunge hao kutulia.

“Waheshimiwa order please (utulivu tafathali, manapoteza muda,”alisema Giga na kuwafanya wabunge kutulia kwa muda na hivyo kumpa nafasi mbunge huyo kuendelea kuuliza swali.

Mara baada ya kumalizika muda wa maswali na majibu alisimama Mwenyekiti wa Bunge, Najma na kuitambulisha timu hiyo hali ambayo ilizidisha shangwe na makofi kwa wabunge.

‘’Tunao wageni 33 wa Mavunde ambao ni wachezaji wa timu ya Yanga ya Jijini Dar es Salaam,’’ alisema mwenyekiti huyo na kuibua tena shangwe kwa wabunge mashabiki wa Yanga.

‘’Wachezaji hawa samahani Waheshimiwa mashabiki wa Simba naombeni mnyamaze, Waheshimiwa wabunge timu hii bingwa mara tatu inaongozwa na Salaam Mgemi Mjumbe wa Kamati ya Utendaji wa klabu hiyo,’’ alisema.

Alisema ni lazima aseme kwa sababu timu hiyo imeisha pongezwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (Fifa).

Najma pia aliitambulisha timu ya Mbao Fc  waliokuwa wageni wa Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula.

Mbao ipo Dodoma ikijiandaa na mechi ya fainali ya Kombe la FA dhidi ya Simba itakayochezwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.