Ugomvi wa Okwi na Abalora ulikuwa hivi

MECHI ya Simba na Azam FC ilikuwa na mvuto wa aina yake lakini licha ya mchezo wenyewe, kulikuwa na matukio tofauti.

Mlipili na Kapombe wawa Chambo

Simba ambao walikuwa wenyeji wa mechi hiyo ya Ligi Kuu, ndiyo walianza kuingia uwanjani kwenye 'pichi' ingawa Azam wao waliwatangulia wakati wa kuwasili uwanjani wakitokea kambini.

Sasa wakati wanaingia katika sehemu hiyo ya kuchezea kwa ajili ya mazoezi ya kupasha misuli wakitokea vyumbani, Simba waliwatanguliza mabeki, Shomari Kapombe na Yusuph Mlipili ambao walikimbia moja kwa moja hadi uwanjani na baada ya dekunde kama 30,  makipa Aishi Manula na Ally Salim nao walitoka na dakika moja baadaye, wakatoka timu nzima.

Kitendo hicho hakikuwa cha kawaida na mara nyingi hutokea pindi timu hiyo au watani wao wa jadi Yanga wanapokuwa na mechi ngumu.

Sakata la Okwi na Abalora

Mshambuliaji, Emmnauel Okwi ambaye ndiyo mfungaji wa bao pekee la Simba la dakika ya 36 katika mchezo huo uliomalizika kwa 1-0.

Okwi alikuwa na mzozo wa mara kwa mara na mlinda mlango wa Azam FC, Razack Abalora hasa dakika 20 walipogonga wakati wanawania mpira. Abalora alihisi kama Okwi amemfanyia kusudi na alitaka kumuumiza akawa 'anamkoromea',  kitendo ambacho ni kama kikamtia hasira mshambuliaji huyo ambaye alifanya kazi ya kuliwinda goli kwa nguvu kwa kupiga mashuti ya mara kwa mara ambayo mengine yaliokolewa na kutoka nje akafanikiwa kufunga.

Waghana kivutio

Vikosi vya Simba na Azam vinaundwa na sehemu kubwa ya wachezaji kutoka Ghana,  ambapo jana kwa pamoja, mchezo huo uliwakutanisha nane katika uwanja mmoja.

Wachezaji wa Azam kutoka Ghana ni pamoja na Razack Abalora ambaye ndiyo alidaka golini kwa dakika zote 90, Yakub Mohamed, Danniel Amor, Enock Atta na Benard Arthur, wakati Simba ilikuwa na Asante Kwasi, James Kotei na Nicholas Gyan.

Kitendo cha wachezaji hao nane kukutana katika mchezo mmoja ni kivutio tosha na hata wachezaji wenyewe licha ya mapambano ya ndani ya uwanja, baada ya dakika 90 kumalizika, waliungana na kusalimiana kwa furaha.

Waamuzi chini ya ulinzi

Mara baada ya mwamuzi wa kati, Jonisia Rukyaa kupuliza kipenga cha kumaliza mchezo, yeye na wasaidizi wake, Soud Lila, Helen Mduma na Isihaka Mwalile walilazimika kutolewa uwanjani hapo kwa ulinzi wa askari polisi kutokana na ghasia za hapa na pale zilizokuwa zikifanywa na baadhi ya wachezaji.

Mlinda mlango wa Azam, Razack Abalora ndiyo alikuwa kinara wa kuwazonga waamuzi hao, akilalamika kuwa hawakuchezesha kwa haki.            

Penalti hewa

Kati ya matukio yote yaliyofanyika uwanjani,  lililowaumiza Azam ni kile kitendo cha beki wa Simba Asante Kwasi kucheza mpira  'Takolingi' shambulio lililofanywa na Shaaban Idd  na kusisitiza ni penalti jambo ambalo halikumshawishi mwamuzi, Jonisia akaachana nao.         

St Louis wamshuhudia Okwi na wenzake

Wapinzani wa Yanga wa mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kikosi cha St Luis ya  Shelisheli, walifika uwanjani na kushuhudia mechi hiyo ya Azam na Simba kwa dakika 45.

Kikosi hicho ambacho kitacheza wikiendi hii, msafara wao uliingia uwanjani hapo mapema kabla ya mechi kuanza na kwenda kukaa upande ambao kwa Tanzania unaaminika ni kwa ajili ya mashabiki wa Yanga na kushuhudia mechi hiyo.

Hata hivyo, hawakukaa hadi mwisho, mara baada ya dakika 45 za mchezo kumalizika, waliondoka zao kwenda kupumzika.