Mahadhi kaanza kunogewa

Tuesday February 13 2018Juma Mahadhi

Juma Mahadhi 

By THOBIAS SEBASTIAN

WINGA wa Yanga, Juma Mahadhi, ameanza kunogewa na mechi za kimataifa baada ya kuliomba benchi lake la ufundi kumpa nafasi ya kudumu akichagizwa na bao alilofunga Yanga ilipoichapa St. Louis ya Shelisheli bao 1-0 Jumamosi.

Nyota huyo aliyejiunga na Yanga Juni 2016 akitokea Coastal Union, amekuwa na wakati mgumu Jangwani akishindwa kujihakikishia nafasi kikosi cha kwanza, lakini kwa sasa amedai amezaliwa upya baada ya mechi hiyo ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

“Nikicheza vizuri mechi hizi za kimataifa zitakuwa njia yangu ya kuonekana na timu nyingine kwani viongozi, makocha na mawakala wa timu kubwa huwa wanafatilia michuano hii,” alisema Mahadhi ambaye mwaka huu ameifungia Yanga mabao mawili, moja kwenye Kombe la Mapinduzi na la juzi la Ligi ya Mabingwa.

Winga huyo anaamini kadiri atakavyopewa nafasi kikosi cha kwanza ndivyo atakavyokuwa mtamu zaidi.

Yanga ambayo kesho Jumatano itaikaribisha Majimaji katika Ligi Kuu Bara, itaifuata St. Louis kwa mechi ya marudiano ikihitajika kushinda ama kuambulia sare yoyote kutnga raundi ya kwanza.