Lacazette awavuruga mashabiki wa Arsenal

Muktasari:

Mshambuliaji huyo Mfaransa amekuwa katika wakati mgumu tangu alipotua Arsenal

LONDON, ENGLAND. Kufungwa hakujawahi kufurahisha, asikwambie mtu. Tena kama utafungwa na hasimu wako.

Basi bana, hicho kimeikuta Arsenal juzi Jumamosi walipochapwa na Tottenham Hotspur kwenye Ligi Kuu England jambo ambalo limemfanya shabiki mmoja wa Arsenal kuchukua uamuzi wa kuichoma moto jezi ya straika wao, Alexandre Lacazette.

Shabiki huyo alikerwa na kitendo cha straika huyo wa Kifaransa kushindwa kusawazisha bao baada ya kupata nafasi ya kufanya hivyo.

Bao la kichwa la kipindi cha pili kutoka kwa straika anayetisha kama njaa, Harry Kane lilitosha kuipa Spurs ushindi muhimu kabisa dhidi ya mahasimu wao hao kwenye London derby.

Kocha, Arsene Wenger amekiri kwamba kipigo hicho ni pigo kubwa katika kampeni yao ya kufukuzia nafasi ya nne ili kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao na sasa matumaini yao yapo kwenye Europa League pekee.

Katika mechi hiyo, Lacazette alitokea benchi kuchukua nafasi ya Henrikh Mkhitaryan, ambaye alionekana kuwekwa mfukoni na mastaa wa Spurs na kushindwa kufurukuta kabisa.

Baada ya kuingia tu, straika Lacazette alikosa nafasi mbili za wazi, moja ikiwa yeye na goli tu, lakini akashindwa kutumia fursa hiyo na kuifanya Arsenal kutoka mikono mitupu uwanjani.

Mashabiki wa Arsenal kwa sasa wanafurahi kwa kuwa Lacazette si straika wao namba moja baada ya ujio wa Pierre-Emerick Aubameyang kikosini.

Aubameyang naye alicheza, lakini hakufanya kitu kwa sababu ni kama aliwekwa kiswani vile baada ya viungo wa Arsenal kuonekana kubanwa katikati ya uwanja na kushindwa kufikisha mpira kwa supastaa huyo wa Gabon, aliyetokea Borussia Dortmund.

Mechi nyingine ya ligi, Arsenal watacheza Machi Mosi, watakapomenyana na vinara Manchester City.