Yanga safi sana, ila kazi haijaisha

Kikosi cha Yanga kilichowatoa nishai MC Alger  katika mechi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika iliyopigwa juzi Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam. Yanga inahitaji ushindi ama sare yoyote katika mchezo wa marudiano wikiendi hii mjini Algiers, Algeria ili isonge mbele na kutinga hatua ya makundi ikiwa ni kwa mara ya pili mfululizo. PiCHA:SAID KHAMIS

Muktasari:

>>Yanga imeendeleza rekodi yake ya tangu mwaka 2012 ya kutopoteza pambano lolote uwanja wa nyumbani dhidi ya timu zinazotokea Afrika ya Kaskazini ambazo kwa miaka ya nyuma zimekuwa zikiisumbua timu hiyo nje ndani.

WAWAKILISHI pekee wa Tanzania katika michuano ya soka ya kimataifa ngazi ya klabu, Yanga juzi Jumamosi ilikifanya kile ambacho mashabiki wa soka nchini walikuwa wakikiombea.

Timu hiyo ilipata ushindi mbele ya timu ya MC Alger ya Algeria katika pambano la kwanza la hatua ya mtoano ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuichapa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Yanga imeendeleza rekodi yake ya tangu mwaka 2012 ya kutopoteza pambano lolote uwanja wa nyumbani dhidi ya timu zinazotokea Afrika ya Kaskazini ambazo kwa miaka ya nyuma zimekuwa zikiisumbua timu hiyo nje ndani.

Bao pekee lililotumbukizwa kimiani na Thabani Kamusoko, lilitosha kuifanya Yanga angalau kupumua mbele ya Waarabu hao, japo ukweli ni kwamba vita kwa wawakilishi wetu hao dhidi ya MC Alger ni kama imeanza upya.

Ndio! Ushindi iliyopata Yanga ni kiduchu sana kwa timu hiyo, rekodi zinaonyesha hivyo kuwa, Yanga imekuwa ikipata wakati mgumu kuweza kupata matokeo mazuri ugenini katika nchi za ukanda huo.

Mara zote imekuwa ikipata matokeo mazuri na ya kuridhisha nyumbani dhidi ya timu za Waarabu, lakini zikienda ugenini zimekuwa zikipoteza michezo yao na kung’olewa kiulaini.

Ni mara mbili tu Yanga iliweza kupata matokeo ya sare ugenini mbele ya timu za Kiarabu, ilifanya hivyo mwaka 1992 ilipolazimisha sare ya 1-1 dhidi ya Ismailia ya Misri na kurudia tena 2008 ilipotoka sare kama hiyo na Al Akhdar ya Libya.

Rekodi mbaya kwa Yanga ni kwamba katika historia ya ushiriki wake wa michuano ya Afrika, haijawahi kuitoa timu ya Afrika Kaskazini, kitu ambacho kwa mwaka huu ni lazima Yanga irekebishe makosa baada ya ushindi wa nyumbani.

Mwaka juzi ilikaribia kuitemesha taji Al Ahly ya Misri kwa kuichapa bao 1-0 jijini Dar es Salaam na kukaza katika mechi ya marudiano kwa kufungwa idadi kama hiyo kabla ya penalti kuwaondoa mashindanoni.

Hata mwaka 2008 walipotoka sare ya 1-1 na Al Akhdar, wengi waliamini Yanga ilikuwa inafuzu kwa kurudiana na wapinzani wao nyumbani, lakini kilichotokea ni kwamba wawakilishi hao walikubali kipigo cha bao 1-0 na kung’olewa kwa 2-1.

Hata hivyo, kwa kuwa miaka inaenda na soka halichezwi kwa historia ama rekodi ni zamu ya nyota wa Yanga na benchi lao la ufundi kuhakikisha safari hii wanavunja mwiko huo wa kushindwa kuzing’oa timu za Afrika Kaskazini.

MC Alger ni wazuri na hata katika pambano la juzi, ni kama walikuwa wakisaka sare lakini aina ya uchezaji wake unaonyesha sio timu nyepesi na Yanga wikiendi hii itakuwa na kibarua kigumu katika pambano lao la marudiano.

Hata hivyo, hiyo isiwafanye wachezaji wa Yanga kukata tamaa, waende Algiers wakiamini kuwa wanaweza kupata matokeo bora zaidi na kusonga mbele.

Kitu cha kufurahisha ni kwamba kwa miaka ya karibuni Yanga imekuwa ikicheza vyema na kwa kujiamini ikiwa ugenini kuliko mechi za nyumbani na kwa kuwa imeshindwa kupata matokeo ya ushindi mnono jijini Dar es Salaam ni wajibu wao kuhakikisha wanapata matokeo mazuri ugenini ili isonge mbele kucheza katika hatua ya makundi.

Yanga inaweza kabisa kama wachezaji wataamua kucheza kama walivyocheza juzi, muhimu ni kuhakikisha hawavimbishwi vichwa kwa matokeo ya Jumamosi kwa sababu kazi iliyopo mbele yao ni kubwa kuliko wanavyofikiria.

Benchi la ufuindi la Yanga chini ya George Lwandamina linapaswa kufanyia kazi mapungufu yalioonekana kwenye pambano la kwanza dhidi ya Mc Alger ili mechi ijayo iwe rahisi kwao hata kama wanacheza ugenini.

Uzoefu na rekodi tamu alizonazo Mzambia huyo dhidi ya timu za Afrika Kaskazini unaweza kuwa msaada mkubwa kwa Yanga kuweka rekodi ya kutinga makundi ya michuano hiyo ya CAF kwa mara ya pili mfululizo, kitu ambacho kabla ya hapo hakuna klabu ya Tanzania iliweza kufanya hivyo.

Mwanaspoti linawaombea kila la heri Yanga kwa maandalizi yao ya mechi ya marudiano ugenini ili ipate matokeo bora zaidi, kitu ambacho siyo tu itakuwa ni heshima na faraja kwa klabu hiyo, lakini hata kwa soka la Tanzania. Kila la heri!