Yanga na Azam zirudishe vichwa uwanjani

Monday March 13 2017

 

YANGA na Azam FC ndiyo wawakilishi pekee wa Tanzania kwenye mashindano ya Kimataifa. Yanga iko kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika huku Azam ambayo ndiyo klabu yenye miundombinu ghali zaidi Afrika Mashariki inacheza Kombe la Shirikisho.

Kwa mfumo wa michuano hiyo ya msimu huu, timu hizi zina nafasi kubwa ya kufuzu katika hatua ya makundi kama zikituliza akili uwanjani na kutengeneza matokeo kwa vile wigo umepanuliwa kwa maana ya idadi ya timu shiriki. Kwenye hatua ya makundi timu zimeongezwa huku lengo la waandaaji likiwa ni kutoa nafasi zaidi kwa timu za Afrika kuonyesha vipaji vyao pamoja na kukuza soka na kuibua wachezaji wengi kwenye ligi za ndani.

Yanga ambayo iko kwenye raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika ililazimishwa kutoka sare na Zanaco ya Zambia kwenye Uwanja wa Taifa ambapo mchezo wa marudiano utafanyika nchini Zambia siku chache zijazo.

Mechi ya Dar es Salaam Yanga ilionyesha jitihada lakini tunadhani walipaswa kupata ushindi kutokana na nafasi walizotengeneza lakini bado muda upo na nafasi ipo ya kufanya chochote na kusonga mbele zaidi ya pale walipofika msimu uliopita. Hayo ndiyo mashindano ambayo klabu yenye umri wa Yanga inapaswa kuyacheza vizuri na kuonyesha ukomavu wake tofauti na ligi ya ndani ya nchi.

Azam yenyewe ilicheza na Mbabane ya Swazilanda jana usiku na itarudiana nayo vile vile wiki mbili zijazo ugenini.

Kwa aina ya matokeo waliyopata, bado timu zote zina nafasi ya kufuzu na kusonga mbele kwenye mashindano hayo ambayo yana heshima kubwa Afrika. Azam imekuwa ikifanya vizuri katika misimu ya hivi karibuni jambo ambalo limewashawishi CAF kuipanga kwenye hatua ya kwanza badala ya kuanzia kwenye mtoano kama timu zingine za ukanda huu wa Afrika Mashariki.

Mashabiki na Watanzania wote wana shauku ya kuona Azam ikiingia kivingine kwenye michuano ya msimu huu kutokana na kikosi kipana ilichonacho chenye wachezaji wenye uzoefu na wanaoandaliwa kwenye mazingira ya kiuchezaji kuliko timu zingine za Tanzania na ukanda huu

Jambo la msingi ambalo timu hizi zinapaswa kufanya ni kutuliza akili zikiwa uwanjani na kutengeneza matokeo. Kila mmoja atekeleze wajibu wake na aelewe umuhimu wake kwenye timu katika kusaka ushindi.

Mashindano hayo ya kimataifa ndiyo yenye heshima na yanayopandisha hadhi ya timu pamoja na wachezaji husika.

Maoni yetu sisi Mwanaspoti ni kwamba timu hizi zisibabaike wala kutishika na mazingira ya ugenini, zijiandae mapema kisaikolojia. Wanatakiwa wakumbuke kuwa, soka siyo maneno ya midomoni, ni vitendo zaidi uwanjani.

Wachezaji na makocha wajipange kimchezo na waumize akili wahakikishe wanafanya vizuri katika mechi hizo za marudiano ili kutetea hadhi ya nchi kwa vile ni heshima kubwa kama Tanzania itakuwa na timu mbili kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho.

Kufuzu kwa timu hizi mbili katika hatua ya makundi, si tu kwamba itasaidia katika uuzaji wa wachezaji, bali itasaidia pia katika kuboresha kiwango cha soka la nchi pamoja na kurudisha heshima ya nchi kwani ndiyo mwanzo wa CAF kutuongezea idadi ya timu shiriki kwenye mashindani ya misimu ijayo.

Kwa kuzingatia hilo, viongozi wanatakiwa waziandae timu zao vizuri kisaikolojia ndani na nje ya uwanja, wafanye kila linalowezekana kuweka mikakati mapema na hata kuwahi kwenye nchi husika kufanya maandalizi ya dhati na kuepuka zimamoto ambazo mara zote zimekuwa zikidhohofisha ushiriki wa timu zetu.

Viongozi wanapaswa kutambua umuhimu wa nafasi zao na dhamana walizopewa na wanachama. Wapambane kutetea masilahi ya klabu zao kwenye mashindano hayo, wachezaji waandaliwe vizuri ili watulize akili wafanye kazi.

Maoni yetu bado kabisa nafasi ziko wazi kwenye mashindano hayo, yeyote anaweza kufuzu awe mwenyeji au mgeni na tukifanya makosa tunaweza kujikuta kwenye majuto makubwa.

Yanga ikitolewa kwenye Ligi ya Mabingwa itapata nafasi nyingine ya upendeleo ya kucheza mtoano kwenye Kombe la Shirikisho, lakini ingekuwa raha na fahari zaidi kama ingepambana kufuzu Ligi ya Mabingwa na Azam ifuzu kwenye shirikisho.

 Wigo utakuwa mkubwa zaidi na zikifuzu zote inamaanisha kwamba zitakuwa kwenye mashindano mpaka Julai, maana yake ni kuwa zitapata muda wa kujiimarisha zaidi kutokana na changamoto mbalimbali na hiyo itaimarisha hata ligi yetu.

Nafasi ipo wazi kabisa Azam na Yanga zisituangushe Watanzania. Tunazitakia kila la kheri timu zetu za Yanga na Azam kwenye mashindano haya tukiamini zitaweka uzalendo mbele.