Uanachama wa Zanzibar ulete tija soka la visiwani

THELUTHI mbili (2/3) ya nchi wanachama wa Shirikisho la Soka Afrika (Caf), kwa kauli moja wameipigia kura na kukubali visiwani vya Zanzibar kuwa wanachama wa kudumu wa shirikisho hilo.

Maamuzi hayo yalifikiwa jana Alhamisi kwenye Mkutano Mkuu wa Caf uliokuwa ukiambatana na Uchaguzi Mkuu wa uongozi mpya wa shirikisho hilo uliofanyika mjini Addis Ababa, Ethiopia ambapo wajumbe wake waliridhia suala hilo.

Hili ni jambo la kupongezwa na kuhitimisha kilio cha muda mrefu cha visiwa hivyo katika kuomba kuwa wanachama wa kudumu za Caf na hata Shirikisho la Soka Duniani (Fifa).

Dalili za Zanzibar kuwa wanachama wa kudumu zilianza kuonekana tangu Januari 12, mwaka huu, wakati Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya Caf iliporidhia kulipeleka suala la Zanzibar kwenye mkutano huo wa Ethiopia.

Pia kwa miaka mingi Zanzibar imekuwa ikililia kupata uanachama wa kudumu na mwaka 2004 ilifanikiwa kuridhiwa, lakini ikagomewa naFifa ambalo lenyewe linaitambua Tanzania kama nchi wanachama.

Hata hivyo, mwaka huo Zanzibar ilipata fursa ya klabu zake kutengana na zile za Tanzania Bara katika ushiriki wa michuano ya kimataifa yaani Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika.

Lakini, neema iliyopata sasa Zanzibar kupitia Chama cha Soka visiwani humo (ZFA) ni kwamba, sasa timu za soka za taifa za Zanzibar kuanzia Zanzibar Heroes, Zanzibar Queens na timu za vijana za U17 na U20 zimepata baraka ya kushiriki michuano yote inayosimamiwa na Caf ikiwamo ile ya Afcon.

Hii ni tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma ambapo, timu hiyo ya Zanzibar na wachezaji wake walichangamana na wale wa Tanzania Bara kuunda Taifa Stars, kitu ambacho kwa sasa ni kwamba kila upande utakuwa unajitegemea Afrika.

Mahali pekee ambako wachezaji wa pande mbili watakapokutana na kuunda timu moja ni katika ushiriki wa michuano inayosimamiwa na Fifa kama michuano ya kufuzu fainali za Kombe la Dunia na ile ya Vijana na Wanawake kwa ujumla.

Hii ni taarifa njema kwa wadau wote wa soka nchini, kutokana na ukweli kwamba Zanzibar ilikuwa ikililia nafasi hiyo ili kuondokana na kivuli cha Tanzania Bara na wakati mwingine kuleta msigano hasa katika uteuzi wa timu ya taifa na masuala ya ruzuku.

Kupatikana kwa nafasi hiyo adhimu ina maana kwamba, Zanzibar sasa itakuwa ikiendesha mambo yake kwa ujitegemea, ikiwamo kuhudhuria pia mikutano ya Caf katika kupanga na kuandaa sera na mipango ya maendeleo Afrika.

Pia, itakuwa na haki ya kushiriki uchaguzi wa Caf moja kwa moja ikiwamo kutoa mgombea, mbali na suala zima la kunufaika na ruzuku inazotolewa na Caf kwa maendeleo ya soka ambazo zilikuwa zikidaiwa zikikwama Dar es Salaam.

Mwanaspoti linapongeza juhudi zilizofanywa na ZFA na viongozi wa TFF kupitia Rais Jamal Malinzi katika kuhakikisha Zanzibar inapata uanachama kamili Caf ila ingependa kuona soka la visiwani linanufaika sasa kwa maamuzi hayo ya Addis.

Ndio, kwa muda mrefu soka la Zanzibar limekuwa likiporomoka kwa kasi tangu Zanzibar ilipoanza kujitegemea katika michuano ya kimataifa ngazi ya klabu na vidole vya lawama vilikuwa ikielekezwa Bara kuwa ndio chimbuko la matatizo.

Hata ulipokuwa ukifanya uteuzi wa wachezaji wa Taifa Stars, Zanzibar walikuwa wakilalamika kwamba wanatengwa na kupendelewa zaidi Bara, lakini kwa sasa hilo halitakuwapo tena kwenye michuano ya Afrika.

Zanzibar ijivunge mkanda kwelikweli na hakutakuwa na visingizio tena.

Tunaamini miaka michache ijayo yale yaliyokuwa yakielekezwa kama lawama Bara kwa kukwamisha maendeleo ya soka ya visiwani, yatamalizika na soka la Zanzibar kuinuka kwa kasi na kuleta tija kwa manufaa ya visiwa hivyo.

Matarajio yetu ni kuja kuiona Zanzibar ikiongeza changamoto kwa Tanzania Bara kwa mafanikio itakayokuwa nayo kisoka Afrika, sawia na kufungua milango kwa nyota wake wenye kujiuza katika soka la kimataifa, ili kuthibitisha kuwa ilicheleweshwa sana kuwa kwao chini ya kivuli cha Tanzania Bara.