Timu zilizopanda daraja zisipoteze muda

Monday March 20 2017

 

LIGI Kuu ya Tanzania msimu ujao itashuhudia timu tatu mpya zilizopanda hivi karibuni kutoka kwenye miji ya Iringa, Singida na Njombe.

Timu zilizopanda kucheza Ligi Kuu msimu ujao ni Singida United ya Mkoa wa Singida, Lipuli FC ya Iringa na Njombe Mji.

Ujio wa timu hizo umepokewa kwa furaha kubwa na mashabiki wa soka kuanzia mikoa zinakotoka na Tanzania yote kwa ujumla kwani,  wataanza kuona ladha mpya kutoka mikoani ambako inaaminika kwamba ndiko chimbuko la vipaji vya soka.

Ukweli ni kuwa mashabiki wa mikoa hiyo ambayo zamani ilikuwa na timu za Ligi Kuu, walikosa burudani kwa miaka mingi hadi sasa wataanza kupata ladha ikiwa ni pamoja na kuziona klabu kubwa za Yanga, Simba na Azam.

Lakini, maoni yetu ni kwamba huu sio wakati wa timu hizo kupiga siasa na kukubali kuwa chambo za baadhi ya watu ambao, wanazitumia kwa manufaa yao binafsi.

Viongozi wa hizo timu wakae chini wajipange na kukaa mkao wa Ligi Kuu kwa kuwa sasa wanaingia kwenye mashindano magumu na ambayo yanahitaji fedha na mipango ya maana kwelikweli.

Huu ndiyo muda wa kusaka wadhamini wapya na imara zaidi, huu ndiyo muda muafaka wa kutengeneza safu imara ya uongozi na kujenga maridhiano mazuri ambayo yatawajenga na kuwaimarisha zaidi msimu utakapoanza.

Kwa kuwa na mipango mizuri ya masoko itasaidia kuwa na klabu imara kiuchumi ambayo, itasaidia zaidi kwenye usajili imara na kuwa na kambi nzuri ya maandalizi muhimu yanayostahili kwa wanasoka.

Klabu zisiishie kushangilia kupanda daraja na kucheza Ligi Kuu Bara tu, zikasahau kufanya maandalizi zikidhani kwamba msimu uko mbali, hakuna jambo zuri ambalo linakuja kwa kushtukiza kila kitu cha maana au mafanikio makubwa yanayotokea kwenye mpira yanaanza kwa maandalizi kabambe na sio ya mchezomchezo kabisa.

Mikoa ambayo klabu hizo zimepanda ina wafanyabiashara wengi wa maana ambao, wakishawishiwa kwa mipango ya maana na inayoonekana yenye wasimamizi mzuri, kamwe hawawezi kushindwa kuwekeza.

Mdhamini yeyote anawekeza fedha zake sehemu kwa lengo la kujitangaza na kuwafikia watu wengi kwa wakati mfupi, hakuna mtu anayependa kujihusisha na vitu vibovu na visivyo na mipango madhubuti.

Hivyo, basi kwa Mji Njombe, Singida United na Lipuli FC huu ni wakati wa kujipanga na kubuni mikakati imara itakayowawezesha kuonyesha ushindani na kuzipa changamoto klabu kubwa badala ya kuwa wasindikizaji ama kugeuzwa kapu la kubeba pointi tatu kila zinapoingia uwanjani.

Huu ni wakati wa kujipanga na kujenga misingi imara kuliko kusubiri muda wa maandalizi umalizike bila kufanya lolote la maana na hapo ndipo, mikakati ya zimamoto huibuka.

Kama wakishindwa kujipanga, itakuwa ni aibu na mwanzo wa kuvurunda kwa timu hizo ngeni kwenye ligi, kitu ambacho hakitakuwa na maana yoyote kwa mikoa husika haswa ukizingatia kwamba, wadau wamekomaa na kuzipa kila aina ya sapoti ili kuhakikisha timu zao hizo zinapanda  ili kukuza vipaji na kutangaza zaidi soka ya maeneo husika.

Tunatarajia soka la ushindani msimu ujao ambalo tunadhani kwamba, litatokana na maandalizi ya maana ambayo tunasisitiza kwamba yanapaswa kuanza sasa kuanzia kwa viongozi wenyewe, wanachama na mashabiki.

Lakini, mashabiki wa mikoa husika bado wanaendelea kuwa na jukumu kubwa na muhimu la kuhakikisha wanaendelea kuziunga mkono timu hizo kwa hali na mali ili ziweze kufikia malengo kwenye mashindano.

Jukumu la kuzipa hamasa kwa kufika uwanjani kwa wingi ikiwa ni pamoja na kusafiri na timu kila zinapocheza iwe ndani ama nje ya kituo ili kuwapa hamasa wachezaji kwa kuwashangilia.

Pia, tunatoa wito pia kwa wadau wa mikoa husika kuzisaidia timu hizo kwa kila namna hasa wakati huu zitakapokuwa kwenye maandalizi kwani, nyingi hazijapata wadhamini hivyo, kuendelea kutegemea nguvu ya wananchi wa maeneo husika badala ya kuwaachia mzigo viongozi.