Nyika, wakishindwa kurudi na medali tusiwalaumu

Friday March 24 2017

 

TIMU ya taifa ya Tanzania ya mchezo wa riadha, imeondoka nchini jana mchana kutokea jijini Arusha kwenda Kampala, Uganda tayari kwa ushiriki wa mashindano ya Mbio za Nyika za Dunia (Cross Country 2017).

Mbio hizo zinatarajiwa kufanyika keshokutwa Jumapili nchini humo na msafara wa timu yetu kwenda huko una jumla ya watu 40 wakiwamo wanariadha 28.

Msafara huo uliondoka kwa usafiri wa basi kwenda kwenye michuano hiyo,  itakayoshirikisha wanamichezo 410 kutoka nchini 51 duniani watakaoshindana kwenye mbio nne tofauti.

Wanariadha na viongozi wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) wameondoka wakiwa na matumaini makubwa ya kurejea na medali kutoka kwenye mbio hizo.

RT na wanamichezo wetu wanaamini kuwa, huu ni wakati wao wa kuanza kurejesha heshima ya mchezo huo kwa Watanzania hususani mashabiki wa riadha.

Hakuna siri, riadha imepoteza mvuto na msisimko wake, kutokana na kushindwa kwao kufanya vizuri kwenye anga za kimataifa.

Kwa siku za karibuni angalau kuna dalili za mafanikio zilizoanza kuonekana ikiwamo kufanya vizuri kwa mwanariadha Felix Alphonce Simbu aliyetwaa medali ya dhahabu kwenye michuano ya Mumbai Marathoni 2017.

Mwanariadha huyo pia alijaribu kuitoa kimasomaso kwenye Michezo ya Olimpiki 2016 ya Rio de Janeiro, Brazil Agosti mwaka jana kwa kumaliza katika nafasi ya tano.

Aina ya wanariadha wanaokwenda kutuwakilisha Uganda na ubora wa rekodi zao unawapa matumaini makubwa Watanzania na hata Mwanaspoti linaamini jeshi lililotumwa kutuwakilisha Kampala ni mashujaa wa ushindi.

Hata hivyo, namna timu hiyo imeondoka ni kinyonge mno, huku ikiwa haijapewa kipaumbele tofauti na inavyokuwa kwa timu nyingine za taifa, hususani zile za soka.

Wawakilishi hao wamechukuliwa kawaida tu, licha ya jukumu kubwa walilonalo katika kulipigania taifa kwenye mashindano hayo mikubwa, kitu ambacho Mwanaspoti linapata shaka ya kuweza kufanya vema kwenye mbio hizo.

Kwa wanamichezo kusafiri kwa umbali mrefu wa zaidi ya kilomita 900 kwa kutumia usafiri wa basi ni moja ya sababu ya kutengeneza mazingira magumu ya timu yetu kushindwa kurejea nchini na medali.

Hatuwakatishi tamaa ama kutaka kumlaumu yeyote, kwani tunajua hali halisi ya kifedha iliyonayo RT na hata kuweza kutuma timu ya wachezaji 28 ni kuonyesha namna gani viongozi wa RT wanahitaji pongezi zao kwa dhamira waliyonayo ya kuiletea nchi medali kutoka Uganda.

Lakini kwa mazingira ya safari ya wanamichezo wetu kwenda kwenye michuano hiyo mikubwa wakitumia basi la jeshi kwa umbali mrefu namna hiyo ni wazi, ni kama tunawatengenezea mazingira ya kufeli mapema kabla hata ya kushindana.

Mbaya ni kwamba timu imechelewa kuondoka Arusha tofauti na ratiba ya awali kufuatia mabadiliko madogo ya baraza la mawaziri likiigusa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. Awali ilielezwa kuwa timu hiyo ingeagwa jana saa 2 asubuhi kisha kuanza safari majira ya saa 3 asubuhi, lakini ikashindikana.

Aliyekuwa waziri wa wizara hiyo na aliyekuwa akabidhi bendera saa 2 asubuhi, Nape Nnauye uteuzi wake ulitenguliwa, hivyo kukwamisha shughuli hiyo kufanyika kwa wakati uliopangwa awali, badala yake shughuli hiyo  imefanyika mchana.

Hali hiyo imefanya wawakilishi wetu kupewa ugumu wa kufanya vema kwenye michuano hiyo, ingawa tunaamini kwa uzalendo walionao ili kupambana na kuitoa kimasomaso Tanzania kwenye mbio hizo.

Kwa namna ya mazingira hayo yalivyo hata kama timu yetu ikishindwa kurudi na medali yoyote hatupaswi kuja kuwalaumu kwa sababu tumeshindwa kuitengenezea mazingira mazuri ya kufanya vema kwenye michuano hiyo.

Usafiri wa barabara unafahamika na kwa mchezaji anayekaa kwa zaidi ya saa 9 akiwa safarini, kunaweza kumpunguza ufanisi wake na mbaya muda ambao wanamichezo wetu watakaowasili Kampala na kujiweka tayari kuingia kwenye mbio hizo ni mchache na sio rafiki kwa kuwapa mafanikio.