Lipuli isipojishtukia itarudi ilikotoka

Monday April 3 2017

 

By MWANASPOTI

LIPULI FC ya Mkoa wa Iringa ndiyo iliyokuwa timu ya kwanza kupanda Ligi Kuu Bara kwa msimu ujao wa 2017-2018, kisha ikafuatiwa na Singida United kisha Njombe Mji.

Timu hiyo imerejea kwenye ligi hiyo baada ya kupita zaidi ya miaka 15 tangu iliposhuka daraja miaka ya mwanzoni mwa 2000. Ni miaka mingi sana.

Lipuli na timu hizo nyingine mbili zitachukua nafasi za timu tatu zitakazochemsha kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu na kushuka daraja. Kupanda daraja kwa timu hizo za Lipuli, Singida United na Njombe Mji ni fursa nzuri kwa mashabiki wa soka na wakazi wa mikoa hiyo kuishuhudia Ligi Kuu na kuziona klabu kubwa nchini ambazo zitakuwa zikipishana katika mikoa hiyo kuvaana na wenyeji wao.

Hata kiuchumi kuna faida kubwa kwa mikoa ambayo imepandisha timu Ligi Kuu msimu ujao, ikizingatiwa ni kipindi kirefu mechi zenye hadhi ya Ligi Kuu hazijachezwa ama kufanyika katika mikoa husika.

Singida wamekuwa wajanja, wameinusa fursa na kuanza mikakati ya kujipanga kuipokea ligi hiyo na kuzipokea klabu kubwa na kongwe nchini kama Simba, Yanga, Azam, Mtibwa Sugar na nyingine zilizopo daraja hilo. Serikali ya mkoa huo na wadau wa soka wameanza ukarabati wa uwanja wao wa Namfua, ili kuruhusu utumike kwa mechi hizo zijazo ambazo zitakuwa na manufaa kwa wenyeji wao.

Hakuna asiyejua Simba na Yanga zilivyo na mashabiki na kwenda kwenye mkoa huo kucheza mechi zao dhidi ya Singida United kutawanufaisha wengi kiuchumi ndiyo maana wamiliki wa uwanja na wenyeji wa Singida wameanza kuchangamkia fursa hiyo.

Bahati mbaya ni kwamba, Lipuli Iringa wenyewe wamechagua mgogoro badala ya maandalizi ya kuelekea kwenye ushiriki wao wa mara ya kwanza kwenye Ligi Kuu.

Viongozi wa klabu hiyo wapo kwenye mgogoro mkubwa wa kiuongozi kiasi cha kutishia ushiriki wao kwa mafanikio kwa msimu wao wa kwanza. La kufurahisha ni kwamba Chama cha Soka Mkoa wa Iringa (IRFA) kimeshtuka na kuchukua hatua ya kuichukua timu iwe chini yao kupitia kamati maalumu ili kuinusuru Lipuli.

Hakuna anayejua sababu ya viongozi wa Lipuli kuanza kugombana sasa wakati walishirikiana miezi michache iliyopita kuipandisha timu yao Ligi Kuu. Pia hiki siyo kipindi kizuri cha wenyewe kwa wenyewe kuanza kutibuana, wakati umesalia muda mfupi kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa Ligi Kuu.

Mwanaspoti linatahadharisha viongozi hao wa Lipuli wanaosigana na wakazi wa mkoa kuwa, wasipojiangalia mapema watalia ligi itakapoanza. Kwa kuwa wote wanaijenga nyumba moja, hawana sababu ya kugombeana fito, bali wamalize tofauti zao mapema ili kufanikisha malengo yao ya kupanda Ligi Kuu.

Ligi Kuu ni ngumu na yenye ushindani mkubwa, hailingani na ligi waliyotokea kucheza ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL), hivyo ni lazima wajipange kwa maandalizi mazuri ikiwamo suala la kujenga umoja na mshikamano na kufanya usajili makini.

Katika kitimtim kama hicho kinachoendelea klabuni kwao ni ngumu kufanikisha malengo yao na ni kama Lipuli wanaanza kujichimbia kaburi la mapema kabla hata ligi haijaanza, kitu ambacho hakivutii wala hakina tija kwa juhudi za walioipandisha.

Viongozi wanaosigana, Mwenyekiti wa klabu hiyo dhidi ya Kamati ya Utendaji iliyotangaza kumvua madaraja, inapaswa kumaliza tofauti zao kwa kuwa siku zote wagombanao ndio wapatanao.

Kuendelea kulumbana na kushikana uchawi itakuja kuigharimu timu yao hata kama itakuwa chini ya kamati maalumu na tunaikumbusha IRFA, wasiichukue timu tu, bali watafute suluhu ya mgogoro uliopo ndani ya klabu hiyo ili kuiokoa.

Kama IRFA, viongozi na wanachama na mashabiki wa Lipuli pamoja na uongozi wa Mkoa wa Iringa hawatajishtukia mapema, wasitarajie timu yao kufanya vyema na kuhimili mikikimikiki ya Ligi Kuu isipokuwa kujiandaa kurejea walipotoka tena kwa kasi ya ajabu.

Kwa sababu umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu, Lipuli haipaswi kuanza kusambaratika mapema hivi hata kabla haijaanza kuionja Ligi Kuu baada ya kupita miaka mingi kuipigania kuishiriki, hii ni aibu kwao na kwa wakazi wa Iringa.

Ikataeni aibu hiyo, kwani hata wapinzani watawacheka ikizingatia kuwa kuipata fursa kama hiyo ya kupanda daraja ni ngumu na huwa haipatikana kirahisi kama ambavyo Lipuli na Wanairinga wanavyotaka kuichezea nafasi waliyonayo na walioigharimia kwa jasho na damu wakati wakishiriki Ligi Daraja la Kwanza (FDL).