Huu ndio wakati wa nyota wetu kuchangamka

Friday March 31 2017

 

By MWANASPOTI

MUDA mfupi ambao Mbwana Samatta ameutumia ndani ya klabu ya Genk ya Ubelgiji, umejipambanua namna gani soka la kulipwa hasa barani Ulaya lilivyo.

Samatta wa sasa amenoga maradufu na yule aliyekuwa TP Mazembe ya DR Congo na uzuri soka ni mchezo wa hadharani, anachokifanya kwenye mechi za Ligi Kuu ya Ubelgiji (Jupiler League) na hata katika michuano ya Ligi Ndogo ya Ulaya (Europe League) kimekuwa kikionekana wazi.

Hata katika mechi za timu ya taifa, Taifa Stars zikiwamo zile za mashindano na za kirafiki soka la Samatta limejitofautisha na lile la nyota wengine wa timu hiyo. Tumekuwa tukimuona anavyojitoa kwa jasho na damu kuipigania Stars, hata majuzi tumemuona akifanya yake mbele ya Botswana na kuifungia mabao mawili yaliyowapa ushindi muhimu wikiendi iliyopita.

Ndivyo ilivyo kwa Thomas Ulimwengu, ambaye safari hii alishindwa kujiunga na wenzake kutoka Sweden kutokana na kusumbuliwa na majeraha, lakini hata katika mechi alizokuwa akija kucheza alikuwa akijitofautisha na wenzake.

Ulimwengu kwa miaka mitano alikuwa akicheza soka la kulipwa TP Mazembe kabla ya mwaka huu kuamua kukimbilia Sweden ambako aliwahi kusakata soka enzi anaibukia.

Hii ni kuonyesha soka la kulipwa hasa katika nchi ambazo zina ligi nzuri na miundombinu inayowapa fursa wachezaji kupania ujuzi na ufahamu wake wa kusakata soka linasaidia sana.

Mataifa mengine wakiwamo Wakenywa wamekuwa wakinufaika na suala hilo na kuweka mkazo wa kuruhusu nyota wao kutoka nje kusaka maisha kwa manufaa ya nchi zao.

Juzi tu wakati Samatta akiibeba Stars, Mkenya Michael Olunga anayecheza China aliisaidia Harambee Stars kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya DR Congo. Ndivyo ilivyo kwa nyota wa Uganda, Nigeria, Misri, Zambia na nchi nyingine.

Nini maana yetu? Mwanaspoti linaamini kuwa, Tanzania ina wachezaji wenye uwezo wa kucheza soka la kulipwa, kama wenyewe wana utayari wa kufanya hivyo na ambao, wataungwa mkono na viongozi wa klabu zao kuwafanikishia.

Muhimu ni wachezaji kwanza kuwa na utayari huo kama ambavyo Samatta alivyokuwa wakati akisaka nafasi na hata majuzi alipokuwa nchini aliwakumbusha wenzake kuwa, sio kazi rahisi kutoka kama wenyewe hawatajiandaa kutoka.

Wachezaji wengi wenye vipaji wamekuwa wepesi kutamka mdomoni kutamani kucheza soka la kulipwa, lakini wanashindwa kutekeleza kwa vitendo hata pale wanapopata nafasi ya kwenda nje ya nchi kufanyiwa majaribio. Wamekuwa wakiridhika mapema na kurudi nyumbani kuendelea na mambo yao.

Hata viongozi wa klabu na wasimamizi wa wachezaji hao, wanashindwa kuwapa msukumo wa kupigania kupata nafasi nje ya nchi, badala yao wao ndio huwa wa kwanza kuwahamasisha warudi nyumbani kuendelea kuwa wa hapahapa tu.

Wachezaji vijana na wenye uwezo mkubwa kisoka, lazima wawe na wivu wa maendeleo na kuhamasishwa na namna Samatta anavyozidi kusonga mbele kila uchao. Samatta hakufika pale alipo, ila kwa kuwa alikubali kujitoa kwa uwezo wake na kuzingatia nidhamu na kuchochewa na kiu ya maendeleo.

Hivyo wachezaji wasikubali kuendelea kutembea nyuma ya kivuli cha Samatta badala yake wamtumie kama njia ya kuvuka mipaka na kusaka soka la kulipwa kwa sababu tayari mwenzao ameshawafungulia. Samatta sasa anasomeka na kuifanya Tanzania ifuatiliwe, kwanini wasiichangamkie sasa? Wanataka waje kukurupuka wakati umri na muda umeshawatupa mkono? Hapana wanapaswa kuamka sasa.

Wachezaji wasiishie kuota ndoto tu, watimize ndoto zao kwa kuchangamkia soka la kulipwa hasa wanapopata nafasi ya kwenda nje ya nchi kujaribiwa na katu wasikate tamaa hata kama watakuwa wakianguka kwenye majaribio yao. Hodari yeyote anapojikwaa na kuanguka, huinuka na kukung’uta vumbi, kisha kuanza kusonga mbele na hata kama ataanguka kwa mara nyingine bado hubeba ujasiri wa kujaribu na kujaribu na hatimaye kufika kule alikokusudia. Hata wachezaji wetu wajaribu kupita katika mfumo huo wa kutokata tamaa mradi watimize ndoto zao.