Kili Marathon yazinduliwa rasmi Moshi zawadi kibao

Moshi, Kilimanjaro.Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mgwila amezindua mashindano ya mbio za Kilimanjaro Premium Lager Marathon 2018  kwenye hoteli ya Kibo Palace Homes kwa kushirikisha wadhamini, Chama Cha Riadha Mkoa wa Kilimanjaro (KAAA) na waandaaji wa mbio hizo.

Akizindua mbio hizo, Mgwila aliwapongeza wadhamnini na waandaaji wakiongozwa na Kilimanjaro Premium Lager 42km, Tigo-21km Grand Malt 5km  na wadhamini wengine wa meza za maji kwa kazi nzuri kwani wamezifanya mbio hizi ziwe maarufu tangu kuanishwa kwake miaka 16 iliyopita na hivi kufanya Moshi na Kilimanjaro kwa ujumla ifahamike na watu kutaka kupatembelea.

 “Ofisi yangu iko tayari kushirikiana na nyinyi na kuwa mwenyeji wa tukio hili muhimu kwani tutahakikisha kuna usalama wa kutosha ili washiriki wawe salama na amani wakati wote wa mashindano,” alisema huku pia akitoa rai kwa washiriki kuhakikisha wanatembelea vivutio mbalimbali vya utalii ndani na nje ya Kilimanjaro baada ya mbio hizo.

Mgwila aliwapongeza wadhamini wengine wakiwemo First National Bank, Kilimanjaro Water, Diamond Motors Ltd, KK Security, Keys Hotel, TPC Sugar, Simba Cement, KNAUF Gypsum, AAR ambao ndio wabia rasmi wa matibabu, Kibo Palace Hotel iliyodhamini uzinduzi huo na waandaaji  Wild Frontiers, Deep Blue Media na Executive Solutions ambao ni waratibu wa kitaifa.

 Akizungumza katika uzinduzi huo Meneja Masoko, Udhamini, Habari na Promosheni wa TBL Group Afrika Mashariki, George Kavishe alisema Kilimanjaro Premium Lager inajivunia kudhamini mbio hizo kwa miaka 16 sasa kutokana na weledi na uzoefu mkubwa wa waandaaji ambao wamefanya mbio hizoziwe maarufu sana na moja ya matokeo makubwa nchini.

Alisema kwa mwaka huu, Kilimanjaro Premium Lager imejiandaa vizuri kwani itatoa zawadi zenye thamani ya Sh20 milioni ambapo mshindi wa kwanza wa mbio za kilometa 42 kwa mwanaume na mwanamke kila mmoja atapata Sh 4milioni.

Alisema mbio za kilometa 5 maarufu kama Fun Run, zinazodhaminiwa na Grand Malt pia zitafanyika ambapo watu wa rika zote wanaruhusiwa kushiriki.

“Hizi ni mbio za kujifurahisha kwa hivyo watu wa rika zote wanakaribishwa kushiriki ili pia iwe kama sehemmu ya mazoezi huku wakipata kinywaji chao cha Grand malt chenye afya tele,” alisema Kavishe. 

Kaimu Mkurueni wa Tigo Kanda ya Kaskazini, Henry Kinabo alisema wamejiandaa vizuri kwa kilometa 21 na kuwataka washiriki wajiandikishe kwa wakati kwani mbio hizo zimekuwa maarufu sana na hii imewapasababu zaidi ya kuendelea kudhamini mbio hizo.

Alisema katika mwaka wake wanne wa udhamini, Tigo itatoa zawadi zenye thamani ya Sh11 Milioni ambapo washindi wa kwanza hadi 10 watapata zawadi huku wa kwanza kwa upande wa wanaume na wanawake akipata Sh2 Milioni  kila mmoja na kuongeza kuwa washiriki wote watakaomaliza mbio hizo watapata medali.

Mkurugenzi Mtendaji wa Wild Frontiers ambaye pia ni Muandaaji wa mbio hizo, John Addison alisema maandalizi yote yamekamilika na mbio za mwaka huu zitafanyika katika Machi 4 katika  Chuo Cha Ushirika Moshi kuanzia saa kumi na mbili asubuhi ambapo mbio za kilometa 42 zinatarajiwa kuanza.

“Tunawashukuru mno wadhamini wetu kwa kutuunga mkono kwani tunatarajia kuwa mashindano ya mwaka huu yatakuwa makubwa nay a kusisimua zaidi,” alisema.