Cheka, Mfilipino kuzicha Mtwara

Mtwara. Bondia Francis Cheka anatarajia kuzichapa na bondia kutoka nchini Ufilipino, Arnel Tinampay siku ya Pasaka Aprili Mosi mwaka huu mjini Mtwara.

Akizungumza leo Ijumaa, Februari 23 wakati wa kutambulisha pambano hilo, meneja wake Beuty Mmari alisema, Cheka ameamua kucheza mapambano yake mkoani Mtwara kama sehemu ya kurudisha heshima nyumbani anakotokea.

“Cheka ni mzaliwa wa Mtwara amefanya kazi zake nyingi nje ya Mtwara, hili pambano ni sehemu ya kurudisha nyumbani kile ambacho amekuwa akikifanya maeneo mengine nje ya nyumbani na mechi hii ni kubwa ya kimataifa ameamua kuifanyia nyumbani,”alisema Mmari

“Cheka sasa hivi anaelekea kustaafu ngumu, kwahiyo katika mipango aliyoiandaa ni pamoja na kufanya kazi za kijamii ndani na nje ya Mtwara, ameona heshima hii airudishe nyumbani kwa sababu anaamini muda mrefu sana alitumika maeneo mengine,na wanaMtwara naomba waichukulie hii kama fursa,”alisema Mmari

Promota wa Cheka, Jay Msangi alisema pambano hilo litafanyika katika uwanja wa Nangwanda Sijaona ambalo litakuwa la raundi kumi.

‘Ufilipino ina mabondia mahiri sana,atakayekutana na Cheka ana historia anatokea katika kambi ya Pacquiao na mwalimu wake, Dante Almario alikuwa mwalimu wa Pacquiao hivyo anakutana na bondia mwenye uwezo mkubwa namba mbili, lakini msisahau Cheka ni bondia mkongwe ambaye ameweza kuwa bondia wa dunia, hivyo utakuwa mchezo wa kihistoria hasa Mtwara,’alisema Msangi

Bondia huyo ameahidi kufanya vizuri katika pambano hilo la kimataifa na kuendelea kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania.

“Sifahamu uwezo wa Mfilipino, lakini uwezo wangu binafsi naufahamu kama nimeweza kuwa bingwa wa dunia, niwahakikishie wanamtwara na Tanzania kwa ujumla nitafanya vizuri kwa ajili ya kusapoti Mtwara ni vizazi vijavyo vya fani hii,”alisema Cheka

Aidha Cheka kwa sasa atakuwa balozi wa mji wa kihistoria wa Mikindani uliopo eneo la Mikindani mjini Mtwara ambapo pia amepata baraka za kimila kutoka kwa wazee.