CAF yalitunuku jiji la Dar wenyeji AFCON

Muktasari:

Tanzania itakuwa mwenyeji wa fainali za Mataifa ya Afrika vijana U17, mwakani

Dodoma. Tathimini ya awali iliyofanywa na timu ya ukaguzi kutoka Shirikisho la Soka Afrika, (CAF) imeonyesha miundombinu ya viwanja vya jiji la Dar es Salaam ndio inakidhi sifa za kutumika katika mashindano ya Mataifa Afrika kwa vijana chini ya miaka 17.

 Tanzania itakuwa mweyeji wa mashindano hayo yatakayoshirikisha timu za vijana nchi mbalimbali.

 Akizungumza Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Michezo wa Wizara  ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Yusuph Singo alisema timu nyingine ya ukaguzi wa CAF itakuja wakati wowote Aprili.

 “Kwa tathimini ya awali wametaja ni Uwanja wa Taifa, Uhuru na tunaweza kutumia uwanja wa Azam Complex Chamanzi,” alisema Singo.

Kwa viwanja vya kufanyia mazoezi, alisema tathimini hiyo imeonyesha viwanja vya Karume, Gmykhana, Shule ya Kimataifa ya Tanganyika, Bandari na Boko Veterian vinaweza kutumika iwapo vitafanyiwa marekebisho madogo.

 Singo alisema ameridhishwa na maandalizi ya timu ya Taifa ya Vijana ya Serengeti Boys itakayoshiriki katika mashindano hayo kwa kuwa imekuwa ikifanya vizuri katika michezo ya kirafiki licha ya kucheza na wachezaji wenye umri mkubwa kuliko wao.