Alliance FC,Biashara Utd kikaangoni upya

Mwanza. Ligi Daraja la Kwanza itaendelea kesho Jumamosi, macho yatakuwa Kundi C kujua nani kati ya wababe wa Kanda ya Ziwa, Alliance FC, Biashara United  atanusa kupanda Ligi Kuu msimu ujao.

Biashara United yenye pointi 23, itakuwa na kibarua kizito cha kuwavaa Rhino Rangers kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine mjini Musoma.

Alliance yenye pointi 19, itakuwa Shinyanga kuwakabili maafande wa Transit Camp katika mchezo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Kambarage, mjini Shinyanga.

Biashara United kama itashinda mchezo huo basi itakuwa imenusa Ligi Kuu msimu ujao huku Alliance wakipata ushindi na Dodoma FC wakapoteza kwa Oljoro basi nao watakuwa kwenye nafasi nzuri ya kupanda daraja.

Kocha wa Biashara United,Omary Madenge alisema wamejipanga kuhakikisha wanashinda mechi tatu zilizobaki ikiwemo dhidi ya Rhino Rangers.

“Mashabiki waendelee kutupa sapoti tumejipanga msimu huu kupandisha timu Ligi Kuu tumebakiza mechi tatu ambazo zote lazima tushinde”alisema Madenge.

Kocha Msaidizi wa Alliance FC,Kessy Mzirai alisema mchezo huo utakuwa na umuhimu mkubwa kwao kupata pointi tatu kama wanataka kupanda daraja msimu ujao.

“Bado tuna nguvu na hatujakata tamaa, tumejipanga kimkakati kushinda michezo mitatu iliyobaki ili kufikia kile tulichokilenga ili msimu ujao tucheze Ligi Kuu,” alitamba Kocha huyo.