MAKALA: Usiibetie Yanga kwenye penalti

Friday January 12 2018

OBREY CHIRWA: Staa huyu Mzambia ndiye kinara wa

OBREY CHIRWA: Staa huyu Mzambia ndiye kinara wa mabao ndani ya Yanga  akiwa amefunga mara sita kwenye mechi za Ligi Kuu Bara. Alikosa penalti yake ya kwanza klabuni hapo ambayo  nyuma ya pazia mengi yamejificha.  Penalti hiyo imeiondosha Yanga kwenye Kombe la Mapinduzi. 

By GIFT MACHA

KAMA unatazama mechi ya Yanga halafu ikaenda hadi kwenye hatua ya penalti, kama ni usiku, zima tu televisheni yako ukalale. Mikwaju ya penalti inaitesa vibaya mno Yanga, tena si kidogo.

Mabingwa hao wa kihistoria wa Ligi Kuu Bara wamekuwa na mkosi mkubwa na mikwaju hiyo ya penalti, na kama hawatajirekebisha hali hiyo itaendelea kuwatibulia hesabu zao. Yanga imekuwa ovyo kwenye kupiga penalti, mpaka inakera.

Juzi Jumatano Yanga ilitupwa nje ya michuano ya Kombe la Mapinduzi na URA ya Uganda baada ya kufungwa kwa mikwaju ya penalti 5-4. Ilikuwa mechi ya nusu fainali ya michuano hiyo iliyoasisiwa mwaka 2007.

Unafikiri hiyo ni mara ya kwanza kwa Yanga kuangushwa kwenye mikwaju ya penalti? Tazama hapa mechi Yanga ilivyoangushwa na mikwaju hiyo tangu 2014 tu mpaka leo. Inasikitisha.

Yanga vs Al Ahly (2014)

Mwaka huo Yanga ilikutana na bingwa mtetezi wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Al Ahly. Wadau wengi wa soka nchini waliamini ilikuwa ni mechi ya kukamilisha ratiba tu kwani Yanga isingeweza kufanya lolote mbele ya Al Ahly.

 Mechi ya kwanza ilipigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na Yanga ikashinda bao 1-0. Shujaa wa mchezo alikuwa Nadir Haroub ‘Cannavaro’. Ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Yanga kuifunga Al Ahly baada ya miaka 32.

Mechi ya marudiano ikafanyika pale Alexandria Misri. Yanga ikiwa chini ya Hans Van Pluijm ikatandaza kandanda safi mpaka Waarabu hao wa Misri wakastaajabu.

Mechi ikamalizika kwa Al Ahly kushinda 1-0. Mwamuzi akaamuru ipigwe mikwaju ya penalti ili kumpata mshindi. Bundi akaamka Jangwani.

Katika penalti tano za mwanzo, aliyekuwa kipa wa Yanga, Deogratius Munishi ‘Dida’ alifanya kazi ya ziada na kupangua mbili. Kilikuwa ni kiwango bora zaidi kuwahi kukishuhudia kwa Dida. Bahati mbaya wachezaji wa Yanga nao wakawa wanakosa. Mwisho wa siku Yanga ikatolewa kwa penalti 4-3.

Yanga vs Azam (2015)

Mechi hii ilikuwa robo fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kagame Cup) mwaka 2015. Yanga ilikutana na Azam katika hatua hiyo na mpira ukapigwa mpira mwingi sana. Hadi dakika 90 zinamalizika hakuna timu iliyokuwa imeweza kupata bao.

Habari mbaya kwa Yanga ni pale mechi hiyo ilipotakiwa kuamuliwa kwa mikwaju ya penalti. Kweli chizi haponi. Yanga haikuweza kufurukuta kwenye mikwaju hiyo na ikatupwa nje na Azam iliyokwenda kutwaa ubingwa huo.

Hata hivyo, Yanga ililipa kisasi wiki moja baadaye timu hizo zilipokutana tena kwenye mechi ya Ngao ya Hisani. Mechi hiyo ilimalizika kwa suluhu na Yanga ikajitoa kimasomaso kwenye mikwaju ya penalti kwa kuibuka kidedea.

Yanga vs URA (2016)

Mkosi wa kukosa penalti uliindosha pia Yanga kwenye nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi mwaka 2016. Mbabe wa Yanga kwa awamu hii hakuwa mwingine, ni URA ileile iliyoitoa juzi Jumatano.

Katika mechi hiyo ya Januari 10 mwaka huo, timu hizo zilitoshana nguvu ya bao 1-1 katika dakika 90. Hakukuwa na namna nyingine zaidi ya penalti kupigwa ili kupata timu moja ya kwenda fainali.

Wachezaji wa Yanga walionekana kuanza kuathirika kisaikolojia kwa mikwaju hiyo ya penalti baada ya kujikuta wakikosa mara mbili na kuifanya URA kuibuka na ushindi wa 4-3.

Ndoto za Yanga kutwaa ubingwa wao wa pili wa Mapinduzi zikaishia hapo.

Yanga vs Azam (2016)

Mzimu wa mikwaju ya penalti uliendelea kuishi Jangwani ambapo awamu hii Yanga ilikutana na Azam tena kwenye mechi muhimu ya Ngao ya Hisani. Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika, Donald Ngoma alikuwa ameifungia Yanga mabao mawili.

Bahati mbaya kwa Yanga ni kwamba haikuweza kulinda ushindi huo na mabao ya Shomary Kapombe na John Bocco katika kipindi cha pili yalifanya matokeo ya mwisho yawe 2-2.

Timu hizo zilipokwenda kwenye mikwaju ya penalti, Yanga iliangukia pua tena na kupoteza. Awamu hii tena ilikuwa ni aibu kwani Azam iliibuka kidedea kwa penalti 4-1 na kushinda Ngao ya Hisani kwa mara ya kwanza katika historia ya klabu hiyo.

 Yanga vs Simba (2017)

Ni kwenye Kombe la Mapinduzi tena. Simba na Yanga kama zali zilikutana kwenye hatua ya nusu fainali mwaka jana.

Mechi ya kukata na shoka ilimalizika kwa suluhu ndani ya dakika 90 hivyo mikwaju ya penalti ikawa ndiyo njia pekee ya kumpata mshindi ambaye angekwenda fainali.

Sijui nini huwa kinawapata wachezaji wa Yanga pindi linapokuja suala la mikwaju hiyo ya penalti. Simba ilipeleka kilio Jangwani baada ya kuibuka kidedea kwa kufunga penalti 4-2. Yanga ikaodoshwa kwa mikwaju ya penalti tena.

Yanga vs Simba (2017)

Mwaka jana haukuwa mzuri kwa Yanga kwani ilijikuta ikifia mbele ya Simba kwa mara nyingine tena. Awamu hii ilikuwa katika pambano la Ngao ya Jamii.

Licha ya kiungo mpya wa Yanga, Mkongomani, Papy Kabamba Tshishimbi kutandaza kandanda safi na kuwafunika viungo wa Simba, mechi hiyo ilimalizika kwa suluhu.

Yanga ikarejeshwa tena kwenye ugonjwa wake wa penalti. Hakukuwa na jipya. Wachezaji wa Simba walishafahamu kitakachotokea.

Walipiga penalti zao kwa kujiamini wakisubiri Yanga ikose.

Haikuchukua muda mrefu kabla ya Juma Mahadhi kupiga penalti ya mwendokasi iliyopeleka shangwe Msimbazi. Yanga ikalala kwa penalti 5-4.

Yanga kutolewa na URA juzi Jumatano ilikuwa tu mwendelezo wa upigaji mbovu wa penalti ndani ya timu hiyo. Ugonjwa ambao sasa unahitaji tiba.