NOMA-Hawa Wamepigwa mateke England

Sunday April 15 2018

 

TANGU ilipoanzishwa mwaka 1992, Ligi Kuu England imekuwa maarufu kwa kuchezwa soka linalotumia ubavu zaidi.

Soka la England halijawahi kuwa la kiufundi sana na hilo waachiwe tu Wahispaniola, lakini linapokuja suala la kutumia ubavu na nguvu, hicho ndicho kitu kinachofanya mashabiki kuipenda mikikimikiki ya Ligi Kuu England.

Mastaa kwenye ligi hiyo wanapigwa sana mateke na ndiyo maana wachezaji kama Dele Alli, Ashley Young wameibuka na mbinu yao ya kujiangusha kila wanapoguswa ili kuepuka kuumizwa. Staa wa Crystal Palace, Wilfried Zaha aliwahi kulalamika kwamba amekuwa akipigwa sana mateke na ngwara ndani ya uwanja na kumfanya aishie kuuguza tu michubuko na vidonda.

Hii hapa orodha ya wachezaji waliochezewa rafu mara nyingi kwenye Ligi Kuu England msimu huu na kuonyesha kwamba kuwa staa kwenye ligi hiyo, unapaswa kuwa na mwili mgumu wa kuvumilia mateke.

Alvaro Morata- rafu 58

Kuna sababu kibao zinazomfanya straika Alvaro Morata apambane na hali yake kwenye Ligi Kuu England baada ya huu kuwa msimu wake wa kwanza kwenye michuano hiyo. Straika huyo Mhispaniola alitua Chelsea kwenye dirisha la majira ya kiangazi la mwaka jana akitokea kwenye ligi inayotumia ufundi mwingine na si ubabe, La Liga. Kabla ya mechi ya jana Jumamosi ya ushindi wa 3-2 iliyopata Chelsea ugenini kwa Southampton, Morata alikuwa amepigwa rafu mara 58 ikiwa kama karibu mgeni kwenye Ligi Kuu England.

Eden Hazard - rafu 61

Moja ya sababu zinazomfanya Eden Hazard kuwa mhanga wa kupigwa sana rafu kwenye Ligi Kuu England ni kutokana na mapenzi yake ya kutaka kuwa na mpira muda mrefu kwenye miguu yake. Hazard anapenda sana kukokota mipira na mabeki wa Ligi Kuu England huwa hawafagilii kabisa hayo mambo. Walau kidogo kwa msimu huu, supastaa huyo wa Chelsea amepigwa rafu mara chache ukilinganisha na misimu mingine ambayo alikuwa kwenye fomu kubwa. Kwa msimu huu, Hazard amepigwa rafu mara 61, lakini hiyo ilikuwa kabla ya mechi za wikiendi hii, ambapo chama lake la Chelsea lilicheza na Southampton huko St. Mary’s.

Joe Allen - rafu 64

Haya yanaitwa maajabu mchezaji ambayo ulitarajia kumwona akipiga wenzake rafu mara nyingi, yeye ndiye aliyefanyiwa hivyo. Joe Allen huko kwenye kikosi cha Stoke City ameonekana kupewa majukumu ya kuwa kiungo wa kuchezesha tu, kutengeneza nafasi za kupatikana mabao na matokeo yake amejikuta akiwa kwenye mtego wa kutolewa macho na mabeki wengi wa timu pinzani. Kutokana na hilo, staa huyo wa zamani wa Liverpool amejikuta akiwa kwenye orodha ya wachezaji waliopigwa rafu nyingi kwenye Ligi Kuu England msimu huu baada ya kuchezewa madhambi mara 64. Kiungo Joe Allen ni moja ya wachezaji ambao pengine msimu ujao wakaonekana kwenye Championship kutokana na timu yake ya Stoke City kuwa kwenye hatari ya kushuka daraja.

Christian Eriksen - rafu 65

Matata ya Tottenham Hotspur kwenye Ligi Kuu England yanategemea zaidi ubora wa kiungo wa kimataifa wa Denmark, Christian Eriksen. Kiungo huyo anacheza mpira mkubwa sana na amekuwa sehemu ya mipango ya kocha Mauricio Pochettino katika kikosi hicho cha Spurs kwa sababu ndiye fundi wa kuamuru mchezo wa aina gani unapaswa kuchezwa kwa wakati husika. Jambo hilo limemfanya Eriksen kuwa sehemu ya kuchungwa zaidi na mabeki wa timu pinzani na hivyo kuishia kupigwa tu rafu uwanjani ili kumpunguza kasi. Kwenye Ligi Kuu England msimu huu kabla ya usiku wa jana kuwakabili Manchester City, Eriksen alipigwa rafu 65.

Roberto Firmino - rafu 67

Moja ya wachezaji ambao wapo kwenye fomu kubwa sana kwenye Ligi Kuu England msimu huu ni Mbrazili wa Liverpool, Roberto Firmino. Firmino amemfanya kocha Jurgen Klopp kujivunia kuinoa Liverpool kwa sababu ameweza kutengeza kombinesheni matata kabisa kwenye fowadi sambamba na Mohamed Salah na Sadio Mane na kuwafanya wababe hao wa Anfield kuwa tishio ndani ya uwanja. Kwa msimu huu, Firmino ni miongoni mwa mastaa waliopigwa mateke mengi sana ndani ya uwanja baada ya staa huyo kupigwa rafu 67 katika mechi alizoitumikia timu hiyo kabla ya mchezo wao wa jana Jumamosi.

Alexis Sanchez - rafu 74

Kwa msimu huu, Alexis Sanchez alianzia kucheza Arsenal kabla ya kuhamia Manchester United katika dirisha la Januari mwaka huu. Lakini, tangu alipotua Old Trafford, Sanchez ameshuhudia akipigwa mateke mara kadhaa na kusababisha vipigwe faulo ambazo wakati mwingine zimekuwa na manufaa kwa timu yake kutokana na kufunga mabao kutokana na hilo. Lakini, kwa msimu huu, Sanchez ambaye hii leo Jumapili atajiandaa na timu yake kuingia uwanjani huko Old Trafford kumenyana na West Brom, amepiga rafu mara 74 na kuwa kwenye orodha ya wachezaji 10 waliochezewa rafu mara nyingi kwenye Ligi Kuu England msimu huu.

Dele Alli - rafu 79

Umeweza kuona, staa wa Tottenham Hotspur, Dele Alli akisema tu akaze miguu basi anaweza kujikuta akitembelea magongo kutokana na kuwa kwenye orodha ya wachezaji ambao wanachapwa sana mateke kwenye Ligi Kuu England msimu huu. Si kwamba ni jambo zuri kwa Dele Alli kujiangusha, lakini wakati mwingine kwa mateke na ngwara wanazopiga mabeki wa Ligi Kuu England ukisema ukaze miguu basi mambo yanaweza kuwa mabaya na magumu mno kwa upande wako. Kwenye ligi ya msimu huu, Dele Alli amepigwa rafu 79 na kuwa mmoja wa wachezaji watano waliochezewa rafu nyingi kwenye ligi hiyo ambayo Man City wanaweza kuibuka na ubingwa.

Mohamed Salah - rafu 84

Unapokuwa mchezaji hatari tu ndani ya uwanja basi wachezaji wa timu pinzani wote wanakutolea macho wewe unapoingia uwanjani. Supastaa huyo wa Liverpool, Mohamed Salah msimu huu anacheza soka la kiwango kikubwa sana na kuwa kivutio kwa mashabiki wa soka wanaofuatilia ligi hiyo kwa karibu. Mo Salah amewafanya Liverpool kuwa na sababu ya kutazamwa wanapokuwa na mechi zao kutokana na kiwango matata cha mchezaji huyo wa kimataifa wa Misri. Lakini, Salah akiwa anafurahia kiwango chake cha soka, amejikuta kwenye madhara makubwa kutoka kwa mabeki kutokana na kumpiga sana rafu, ambapo hadi kufikia wikiendi, kabla ya mechi ya jana, staa huyo alikuwa amepigwa rafu mara 84 kwenye ligi pekee.

Jordan Ayew - rafu 84

Swansea City wamekuwa kwenye mapambano makubwa kwa msimu huu kuhakikisha kwamba wanajiondoa kwenye hatari ya kushuka daraja na kubaki kwenye Ligi Kuu England. Kabla ya mechi za wikiendi, walikuwa wakishika nafasi ya 15 katika msimamo wa ligi hiyo huku wakifurahia kabisa huduma bora ya staa wao wa kutoka Ghana, Jordan Ayew. Kupenda kuwa na mpira kwenye miguu yake kumemponza staa huyo wa Black Stars na kujikuta akikabiliana na mateke kibao kutoka kwa mabeki wa timu pinzani ambapo kwenye Ligi Kuu England pekee kwa msimu huu amekutana na rafu za maana uwanjani, akiwa amepigwa rafu 84.

Wilfried Zaha - rafu 91

Unaambiwa hivi, Crystal Palace bila ya Wilfried Zaha mambo yao huwa yanakuwa magumu sana. Kwa sasa wanapambana na hali kujiokoa wasishuke daraja na hakika wanafurahia kuwa na huduma ya Zaha katika kikosi chao. Lakini, Zaha kwa msimu huu amekuwa mchezaji aliyekumbwa na balaa la kuchapwa rafu mara nyingi ndani ya uwanja na hilo linatokana na staili yake ya kiuchezaji ya kutaka kukokota mipira muda mrefu. Kwa msimu huu, Zaha ndiye mchezaji aliyepigwa rafu mara nyingi baada ya kuchapwa mara 91 kwenye mechi za Ligi Kuu alizocheza kabla ya wikiendi hii.