NIACHE :Sichezi lakini ni suala la muda tu

Muktasari:

  • Mwanaspoti imefanya mahojiano ya kina na mshambuliaji huyo ambaye amefungukia maisha yake ya soka akiwa Prisons, Simba na mengineyo yanayomhusu nje ya soka.

UWEZO wa kufunga mabao ni kitu pekee kinachomtofautisha mshambuliaji na mchezaji wa nafasi nyingine. Mashabiki wanaweza kukuita galasa endapo utashindwa kupachika mabao kama ilivyokuwa kwa Fernando Torres, akiwa na Chelsea.

Wapo wanaotolewa kwa mikopo ili wakaongeze makali yao, lakini kwa upande wa kikosi cha Simba moja ya wachezaji hao ni Mohammed Rashid ‘MO’ ambaye msimu uliopita alikuwa moto wa kuotea mbali akiwa na Tanzania Prisons, lakini kwa sasa anapigiwa hesabu za kukopeshwa.

Alifanya vizuri akiwa na maafande hao wa Mbeya kwa kufunga mabao tisa ndio maana Simba iliamua kumsajili mara tu baada ya msimu wa 2017/18 kumalizika kwa sasa ni kama picha kwa mshambuliaji huyo limebadilika.

Mwanaspoti imefanya mahojiano ya kina na mshambuliaji huyo ambaye amefungukia maisha yake ya soka akiwa Prisons, Simba na mengineyo yanayomhusu nje ya soka.

MAISHA NDANI YA SIMBA

‘Simba ni Simba tu asikuambie mtu’ hiyo ni kauli ya MO ambaye amekiri kuona tofauti ya maisha baada ya kujiunga nao msimu huu, akitokea Prisons ya Mbeya ambayo aliachana nao baada ya kuacha alama ya mabao tisa.

“Ukweli haufichiki yapo mambo ambayo nimepiga hatua ya kimaisha tangu nijiunge na Simba, ambayo isingekuwa rahisi wakati nipo na Prisons, nimefanya vitu vingi vya kimaendeleo na ninaamini nitapiga hatua zaidi,” anasema.

Wakati akidai kimaisha yupo vizuri vipi kuhusu kiwango chake kutokana na kukosa nafasi na kugeuka mtazamaji wa mechi 11 ambazo tayari Simba wamecheza? MO anasema hilo ndilo jambo la kwanza katika kazi yake ya soka.

“Nimejifunza madini mengi kutoka kwa kocha, wachezaji kutoka mataifa mbalimbali, ninayoyafanyia kazi katika mazoezi binafsi, ipo siku ninachokisema kwa sasa kitakuwa kwenye matendo,” anasema.

Anajifananisha na staa wa Ulaya, Alex Sanchez wa Manchester United ambaye aliondoka Udinese ya Italia akiwa kwenye kiwango bora lakini akapotelea Barcelona na mara baada ya kujiunga na Arsenal ndipo aliporejea kwenye kile kiwango chake cha ufungaji.

“Maisha ya mpira huwa yanabadilika na haina maana kutofanya vizuri kwenye timu moja ni sababu ya kutofanya vizuri kwenye timu nyingine kuna sababu nyingi ambazo huwa nyuma ya pazia, mfano mimi nimewakuta Emmanuel Okwi na Meddie Kagere wapo kwenye kiwango cha juu, kocha anahitaji matokeo, ipo siku nitapewa nafasi nitabadilisha upepo kwani Mwalimu Aussems anapenda kasi yangu,” anasema.

ILIKUAJE PRISONS

Hakusita kuweka wazi namna timu hiyo ilivyomsaidia kutangaza kiwango chake, huku akimtaja kocha Abdallah Mohammed ‘Bares’ kwamba alikiendeleza na kufanya aonekane na klabu kubwa Simba.

“Unajua wadau wa soka wanaweza wakaniona kama vile nazingua baada ya kufika Simba, ukweli kwamba Prisons nilipewa sana nafasi na timu ilikuwa inanitegemea, siwezi kuisahau katika historia ya maisha yangu ya mpira,”anasema.

BOBAN, OKWI AWAPA SALUTI

Achana na wachezaji wale ambao wanapenda kuiga staili ya uchezaji wa mastaa wa Ulaya, kwa Mo ni tofauti anakosha na winga anayekipiga African Lyon Haruna Moshi ‘Boban’ pamoja na Mganda Emmanuel Okwi alidai ana nidhamu ya hali ya juu na kila anachokifanya.

“Kiukweli nikikutana na Boban ana kwa ana nitamwambia neno moja kwamba yeye ndiye alifanya nipende sana mpira, jamaa ni fundi, ana vionjo ambavyo ilikuwa ngumu kuchoka kumwangalia akicheza, nilitamani itokee siku nicheze pamoja naye ama nimuone kwenye timu ya Taifa Stars,”anasema.

ELIMU YAKE

Amemaliza kidato cha nne mwaka 2016 katika shule ya Sekondari ya Pugu Boys, baada ya hapo akaamua kujikita moja kwa moja na mpira wa miguu “Niliamini njia yangu ya kutoka kimaisha ni kukitumia kipaji alichonipa Mwenyenzi Mungu,” anasema.

MADEMU WA DAR

Katika stori za hapa na pale Mwanaspoti lilimuuliza eti wewe unapenda sana mademu wa Dar! Mo alipigwa na butwaa na kuhoji mademu wa Dar! mwandishi akaendelea ndio ukweli upo wapi juu ya hilo! Ndipo alipoangua kicheko na kutamka kuwa nina mchumba bhana.

“Kitu kimoja kinachonishangaza kwa mabinti wa Dar es Salaam, najiuliza namba yangu wameipata wapi, ila jambo kubwa nina mchumba wangu na huwa nawaambia ukweli ili wasiendelee kupoteza muda wao.

“Mambo hayo wakati nikiwa Prisons, sikuwahi kutafutwa kiasi hicho na wanawake, nadhani ukubwa wa Simba ndio unaowafanya wanione kirahisi, kikubwa nina misimamo yangu, najitambua kwamba nipo kwenye timu hii kwa ajili ya kazi,” anasema.

MSOSI WAKE

Kuhusu mambo ya maakuli kwake hayana mbwembwe nyingi, asubuhi anajipigilia chapati mbili, chai ya maziwa na pembeni lazima yawepo matunda, lakini wakati wa mchana anapendelea ugali wa dona, samaki na mboga za majani, usiku mpango mzima ni kitu cha mtume yaani wali wa nazi na maharage.

“Nikiwa nyumbani ndio chakula ninachokipendelea, kambini tunapangiwa kulingana na majukumu ya kazi yanayokuwa mbele yetu, mfano tunaepushwa sana vyakula vya mafuta, muda wa kula unakuwa maalumu saa tatu kabla ya mazoezi,” anasema.

PAMBA ZAKE

MO sio mtu anayeumiza akili avae pamba za bei ghali anadai bado hajafikia maisha hayo, badala yake akiona nguo inayomkaa vizuri mwilini basi ananunua na kuendelea na maisha yake.

STAREHE USIPIME

Mbali na mpira wa miguu mchezo mwingine anaoupendelea Mo ni kucheza mpira wa wavu ambao alidai ni fundi na pia anapenda kuangalia senema ambazo zinafundisha maisha.

UZURI, UBAYA WA USTAA

MO anasema kitendo cha kujulikana zaidi akiwa na Simba anajikuta anasaidiwa matatizo yake kwa uharaka, tofauti na alivyokuwa Prisons, lakini pia hasara zake inapotokea akapatikana na skendo basi anaonekana mpumbavu mbele ya Watanzania.

“Namuomba Mungu anisaidie kuniepusha na matukio ya ovyo, kwani sipendi kuwa mchezaji wa ajabu, natamani niwe mfano wa kuigwa kwa wachezaji wengine.