Mapema tu, wamevunja na kuweka rekodi

REKODI huwekwa na kuvunjwa. Ndivyo unaweza kusema kutokana na badhi ya rekodi ambazo zimevunjwa na kuwekwa kwa kipindi hiki cha Ligi Kuu Bara iliyofikia raundi ya 14 kwa baadhi ya timu.
Ligi Kuu msimu huu ina ongezeko la timu nne, kutoka 16 hadi 20 lakini kwa kipindi kifupi ambapo hata mzunguko wa kwanza haujamalizika wapo Makocha mabao wameweka rekodi mpya huku wengine wakivunja.
Mwanaspoti imetazama kwa umakini mechi zilizochezwa katika viwanja mbalimbali hapa nchini na kukuletea baadhi ya rekodi mpya zilizowekwa pamoja na zile zilizovunjwa na makocha wa timu hizo.

SELEMAN MATOLA - LIPULI
Lipuli iliweka rekodi mpya ya kupata matokeo mazuri ambapo aliifunga Mbao FC inayonolewa na aliyekuwa bosi wake Amri Said ‘Stam’ ikiwa ugenini kwa mabao 3-1.
Ikumbukwe makocha hawa waliwahi kufanya kazi wote ndani ya Lipuli ambapo Stam alikuwa bosi wa Matola na msimu huu wamekutana katika dimba la CCM Kirumba dhdi ya Mbao iliyokubali kufa kwa kichapo hicho.
Hiyo ilikuwa ni rekodi mpya kwa Matola kumfunga aliyekuwa bosi wake katika mechi ya ushindani ya Ligi Kuu akiwa ugenini na kuwaacha mashabiki wa Mbao midomo wazi.

MWINYI ZAHERA - YANGA
Mkongo huyu ameweka rekodi tamu msimu huu baada ya kucheza mechi 10 bila kupoteza hata mmoja huku ikiwa imeshinda michezo nane na sare mbili tu.
Timu hii ndio Klabu pekee iliyocheza michezo michache kuliko nyingine, ingawa imefanya vizuri zaidi ya hata zile zilizocheza mechi nyingi.
Hadi sasa Yanga chini ya Zahera imevuna pointi 26  sawa na watani zao Simba ambao wametangulia mchezo mmoja na kukaa nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu.

DADY GILBERT - ALLIANCE FC
Kocha huyu mpya wa  Alliance FC ameweka rekodi tamu katika michezo mitatu aliyosimamia hadi sasa akiwaacha mbali waliokuwa watangulizi wake Mbwana Makata na Renatus Shija.
Kabla ya Makata na Shija hawajaachana na timu hiyo mpya kwenye Ligi Kuu, walikuwa wamesimamia mechi 11 na kuambulia pointi sita tu na kukaa mkiani lakini baada ya ujio wake  Gilbert amekusanya pointi saba kwenye michezo mitatu tu na kuchumpa hadi nafasi ya 16. Hii ni rekodi mpya na tamu.

AMRI SAID - MBAO FC
Kocha huyu Bora wa mwezi Agosti alivunja rekodi kwa Simba baada ya kuwafunga katika mchezo wa Ligi Kuu ikiwa ni mara ya kwanza kwa timu hiyo kupata pointi tatu mbele ya Wekundu hao.
Mbao ambayo ni msimu wake wa tatu katika Ligi matokeo mazuri iliyopata kwa bingwa huyo mtetezi ilikuwa ni sare ya msimu uliopita ya mabao 2-2 lakini mbali na hiyo ilikuwa ikichezea kichapo tu.
Lakini Said baada ya kutua Mbao amevunja rekodi kwa mara ya kwanza kuwafunga Simba bao 1-0 mchezo ambao ulipigwa Septemba 20 kwenye dimba la Kirumba.

ALLY BIZIMUNGU - MWADUI  FC
Msimu uliopita Mwadui ikiwa uwanja wa nyumbani ilipata suluhu ya bila kufungana dhidi ya majirani zao Stand United, lakini mechi ya mzunguko wa pili ililala kwa kipondo cha mabao 2-0 katika uwanja wa CCM Kambarage mjini Shinyanga.
Msimu huu Bizimungu raia wa Rwanda amevunja rekodi kwa kuifunga bao 1-0 Stand United mchezo uliopigwa uwanja wa CCM Kambarage mjini Shinyanga.

RAMADHANI NSAZURWIMO - MBEYA CITY
Kikosi cha Prison chini ya Kocha Abdalah Mohamed ‘Bares’ kilikuwa kiboko kwa majirani zao Mbeya City hasa msimu uliopita baada ya kupata pointi nne kwenye mechi walizokutana.
Lakini mambo yamebadilika msimu huu kwa kocha wa Mbeya City, Ramadhan Nswazurimo kuvunja uteja kwa kuwabanjua Prison mabao 2-0 katika msimu huu mzunguko wa kwanza.
Ushindi huo ilikuwa ni kama kulipa kisasi kutokana na msimu uliopita Prison kushinda mabao 3-2 kisha kutoa suluhu ya bila kufungana, kipindi hiki imeanza na maumivu.

BAKARI SHIME - JKT TANZANIA
JKT Tanzania sio timu ngeni kwenye ligi kwani ilikuwepo na ikashuka daraja, msimu huu imerudi upya na imeweka rekodi ya kipekee chini ya kocha Bakari Shime baada ya kushika nafasi ya saba kwenye msimamo kwa pointi 18.
JKT Tanzani ilianza vyema michuano hii ikiwa na rekodi nzuri baada ya kupanda Ligi Kuu ilionyesha uwezo wa kufika hadi Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho (ASFC) msimu uliopita na kuziacha mbali timu nyingine ilizopanda nazo msimu huu.
Hadi sasa timu hiyo imepoteza mechi mbili kati ya 13 ilizocheza na imeonyesha ushindani hata kuzipita timu kongwe kwenye Ligi Kuu kutokana na soka la ushindani inalocheza.

HANS PLUIJM - AZAM FC
Ukiachana na kutwaa tuzo ya Kocha Bora mwezi Oktoba, Pluijm amekuwa na rekodi tamu kwa msimu huu hadi sasa kwani licha ya kucheza mechi nyingi kuliko wapinzani wake, Simba na Yanga bado timu yake imeendelea kujikita kileleni.
Azam imekuwa na rekodi nzuri kwa kucheza michezo 12 na kushinda tisa, huku ikipata sare tatu na kukusanya pointi 30 na kuziacha Simba na Yanga katika nafasi ya pili na tatu.
Kocha huyu ambaye aliwahi kuzinoa Yanga na Singida United na kuziachia mafanikio mazuri ikiwamo ubingwa wa Ligi Kuu hasa Yanga bado anaendelea kujitengenezea rekodi nzuri kwenye soka la Tanzania.

PATRICK AUSSEMS  - SIMBA
Licha ya kwamba timu hii imepoteza mechi kwenye Ligi Kuu, lakini Kocha Aussems ameweka rekodi tamu kwa kikosi chake kuwa bora katika kufunga mabao mengi kuliko timu zingine zote.
Mbelgiji huyu ameisaidia hadi sasa Simba kufunga mabao 23 huku ikiwa timu ya pili kuruhusu mabao machache (manne) nyuma ya Azam  waliofungwa mawili tu langoni mwao.
Kama haitoshi Aussems ametengeneza kikosi chenye ushindani kwa wachezaji wake kwa kila mmoja kufanya kile mwenzake anachowefanya.