Mambo yamezidi kumnyokea Kessy

Muktasari:

  • Beki wa zamani wa Yanga, Hassan Kessy mambo yanamnyokea huko Zambia baada ya timu yake ya Nkana ya Zambia kutinga nusu fainali ya Kombe la Barclays na wakiifunga Green Buffaloes kwenye fainali basi watatwaa taji hilo.

HUENDA beki wa zamani wa Yanga, Hassan Kessy akatwaa ubingwa wake wa kwanza nchini Zambia kama timu anayoichezea ya Nkana itafanikiwa kuifunga Young Green Buffaloes kwenye mchezo wa fainali ya kombe la Barclays.

Nkana imetinga hatua hiyo ya fainali ambayo itachezwa Novemba 10 kwa kuifunga Power Dynamos kwa mikwaju ya penalti 5-4 baada ya kwenda sare ya mabao 2-2.

Kessy anaamini anaweza kushinda ubingwa wake wa kwanza nchini humo kutokana na ubora wa kikosi chao.

“Ligi imemalizika kwa hiyo nguvu zetu zote tunazielekeza kwenye huo mchezo, siwezi kuongea mengi ila binafsi napenda kuwa mshindi inshu za maandalizi ya mbinu kocha atakuwa anafahamu zaidi nini cha kufanya,” alisema Kessy.

Nkana itaingia kifua mbele kwenye mchezo huo kutokana na kuwa kwao na uhakika wa kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kumaliza msimu wa 2017/18 wakiwa kwenye nafasi ya pili.

Timu hiyo anayoichezea Kessy imemaliza nafasi ya pili ikiwa na pointi 76.

Kocha wa zamani wa beki huyo,George Lwandamina ndiye aliyeibuka na ubingwa wa Ligi Kuu Zambia akiwa na ZESCO United kwa kukusanya jumla ya alama 80.