Papy Tshishimbi: Kuboresha soka Tanzania kuanze na viwanja

Thursday March 26 2020

 

By Papy Tshishimbi

BAADA ya kutoa maoni yangu kuhusu soka la Tanzania katika muda ambao nimekuwa hapa nchini, leo nichukue nafasi kuangalia safari ya kukuza soka la hapa kama ambavyo dhamira ya serikali na hata Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limekuwa likijipanga kufanya.

Kama ambavyo niliandika katika maoni yangu yaliyopita sio kweli kwamba Tanzania hakuna vipaji. Hapa kuna vipaji vingi sana lakini shida kubwa au changamoto ninayoiona ni jinsi gani ya safari ya kuviandaa imefanyika.

Wachezaji wengi hapa hawakupitia msingi mzuri wa malezi ili waje kuwa wachezaji bora kiushindani na hata kufundishika kwa kukosa msingi sahihi ya kukua kwao mpaka kufika juu. Inawezekana zipo sababu mbalimbali za hili kutokea.

Hata wale ambao wamebahatika kufika juu wakati huu sasa ndio wanaonyesha kipi walikikosa wakati wanapita huko na hapa sioni kwamba wao kama wachezaji wanatakiwa kulaumiwa sana kwa kuwa hawajahusika katika hilo ni kama mzazi unapoona mtoto wako amekuwa mtu mzima kisha hana elimu ya kuweza kumsaidia katika maisha lakini kama hukumsomesha na kumtengenezea njia nzuri ya kukua kwake huwezi kumlaumu mtoto badala yake utamuangalia mzazi wake.

Nilichogundua Tanzania kuna viwanja vingi sana ambavyo vimekuwa vikitumiwa na vijana mpaka kuchezwa hata mechi kubwa za ligi madaraja mbalimbali na hata Ligi Kuu ambavyo sisi huku tumekuwa tukivitumia.

Katika viwanja vingi ambavyo vipo changamoto ni kwamba vingi vimekuwa vikikosa ubora ambao ungesaidia hata mchezaji mdogo kukitumia kama njia ya kumkuza vyema katika soka lake.

Advertisement

Inajulikana kwamba maisha ya soka la Afrika viwanja kama hivyo sio kitu vigeni, lakini kwa ndoto ambayo kijana mdogo anakuwa nayo kisha kuwa na kiu ya kutaka kuona anafika mbali basi ni vyema sasa akili pia ikabadilika.

Kuna haja kubwa kwa Tanzania kuhakikisha kwanza viwanja hivi vinaboreshwa kwa haraka ili kuwasaidia hata vijana kujifunza mambo mbalimbali wakiwa wadogo kabla ya kufika juu.

Nimekuwa nikiona jinsi makocha wa kigeni wakitoa mazoezi mbalimbali ambayo mengi yalipaswa kuwa mchezaji amefundishwa akiwa chini lakini sio ngazi ya juu ya Ligi Kuu.

Hapa Tanzania kuna muamko mkubwa wa wananchi kupenda mpira na pia hata muamko wao kuja viwanjani ni mkubwa sana na bahati nzuri zaidi hata viwanja hivyo vipo katika mikoa mbalimbali jambo ambalo kama muamko wa mashabiki ungetumiwa vizuri ungesaidia kuweza kukarabati viwanja hivi.

Eneo muhimu katika matengenezo haya ni eneo la kuchezea ambalo ndio malengo sahihi ya kuweza kutumika kukuzia vipaji mbalimbali kama kila mamlaka ya kila mkoa ingekuwa na jicho la mbali.

Niliwahi kuuliza ni nani anayemiliki viwanja hivi nikaambiwa chama cha siasa (CCM) ambacho ndio wanaviongozi mbalimbali katika kila eneo ambalo viwanja hivi vipo.

Endapo vijana wangeboreshewa viwanja hivi basi wangekuwa wamepata nafasi nzuri ya kujua mambo mengi sahihi ya kukua kwao lakini pia sio tu vijana hata huku ligi kubwa za juu bado viwanja hivihivi vingesaidia kupatikana kwa ushindani mzuri wa ubora kwa timu zote.

Zinapochezwa mechi kubwa mashabiki wanaingia wengi na unaambiwa kuna fedha zinakatwa kwa ajili ya wamiliki wa viwanja, bado najiuliza kama hilo ni kweli kwanini fedha hizo hazijaweza kutunzia viwanja husika kwa kuwa ndio vinavyozalisha fedha?

Mashabiki wanalipa fedha kuja viwanjani kuangalia soka safi lakini soka hilo huchezwa katika eneo la kuchezea sasa kama halitakuwa katika ubora kumfanya mchezaji kuonyesha uwezo wake ni sawa na kuwaibia mashabiki fedha zao.

Rai yangu viwanja hivi hata kama vitapishana hadhi na kile cha Taifa au hata Uhuru basi ni vyema kwa haraka mamlaka zikaangalia namna ya kuviboresha hata kwa eneo la kuchezea liwe na hadhi ya juu.