Kombe la Dunia na athari za kiufundi kwa timu

Tuesday July 10 2018

 

FAINALI za Kombe la Dunia mwaka huu zimekuwa kivutio licha ya wasiwasi uliokuwapo awali. Kulikuwa na shaka kuhusiana na usalama kuhusiana na nchi mwenyeji, Russia. Baadhi ya mashabiki walihofia kwenda kwa sababu za kisiasa, lakini pia hofu za ubaguzi.

Hatua ya robo fainali ndiyo imeshavukwa ambapo timu za mataifa makubwa kisoka, zimefungishwa virago. Pamekuwapo mapinduzi mengi katika soka, lakini msingi wake hutokea kwenye klabu na si timu za taifa, hii ikiwa ni kwa vile vikosi vya timu za taifa hukaa pamoja kwa muda mfupi tu, hasa vinapojiandaa kwa mechi za mashindano kama haya, kisha wachezaji hurudi katika klabu zao.

Kumbe basi ni makocha wa klabu pamoja na wakufunzi wengine ndio wenye majukumu ya kuwatengeneza wachezaji na kuwaweka kwenye mfumo unaotakiwa, lakini pia na wachezaji wenyewe kujituma kwenye mazoezi ya mmoja mmoja kama afanyavyo Ronaldo.

Hispania ilikuwa na Kocha Fernando Hierro, anayekiri mabadiliko makubwa kwenye soka, akisema katika miaka ya 2008, 2010 na 2012 walikuwa na aina fulani ya wachezaji waliocheza katika kiwango ambacho hakuna aliyekuwa amefanya kabla.

Sasa, 2018, mengi yamebadilika na timu nyingi zinacheza soka la kujihami, wakati mwingine ukuta ukiwa na watu watano, kitu kilichokuwa kimesahaulika, lakini pia kuna mipira mingi ya moja kwa moja.

Ni muhimu sana kocha kukaa na wachezaji kwa muda mrefu na kwa Hispania naweza kusema kwamba moja ya sababu za kuondoka mapema ni Hierro kuwa kocha, kwa maana nyingine shida haikuwa kwenye maendeleo ya kimbinu.

Hierro aliwekwa kwenye nafasi ambayo naweza kusema isiyowezekana kirahisi, akitumia wachezaji walioteuliwa na kuwekwa kikosini na kocha mwingine na pasipo hata muda wa kutia humo mawazo yake.

Walipocheza dhidi ya Morocco na Urusi, kuna nyakati Hierro alikuwa kana kwamba kaganda kwa sababu wachezaji wale hawakuwa wake na hata kama walikuwapo asiowataka, hakuwa na la kufanya kwa sababu aliteuliwa siku mbili tu kabla ya kuanza mashindano, alipofukuzwa Julen Lopetegui kwa sababu za kutangazwa kujiunga na Real Madrid kuchukua nafasi ya Zinedine Zidane aliyekimbilia timu ya taifa ya Qatar.

Chama cha Soka cha Hispania kilikuwa na hofu Lopetegui angeigawa timu, kuwapendelea wa Real Madrid na kuwakandamiza wa Barcelona. Ikumbukwe tayari kwenye kikosi hicho kuna mahasimu wawili, Ramos (Real) na Gerard Pique (Barca) wote wakicheza kwenye beki ya kati. Pique akiunga mkono Katalunya kujitenga huku Ramos ambaye ni nahodha akihubiri umoja wa kitaifa.

Baada ya kufanya vibaya kwenye mashindano mawili yaliyopita mfululizo, Lopetegui alionekana amewafufua na kuwatengeneza vyema Hispania na walitabiriwa makubwa kama si kiburi cha Real Madrid na Rais wao, Florentino Perez, kumtangaza kuwa kocha wao wakati Hispania wakiwa tayari wamewasili Russia.

Naamini wangefika mbali zaidi wakiwa na Lopetegui kuliko Hierro aliyekaa tu kama kivuli, akitegemea nguvu na uwezo wa mchezaji mmoja mmoja pasipo kuwa na falsafa, kwani hangeweza kuiingiza ndani ya siku mbili hizo alizokuwa nazo.

Nakumbuka Xavi alisema Hispania wamekuwa na wakati mgumu dhidi ya timu zinazotumia mfumo wa 3-5-2 kama Chile walivyowafanya mwaka 2014 na Italia 2016, kwa sababu ni vigumu kutia shinikizo kubwa dhidi ya timu yenye watu watano pale nyuma, hasa wakiwa na namba tisa mahiri kama Stanislav Cherchesov wa Russia alivyowatikisa kwenye mechi waliyovuliwa ubingwa.

Kwa upande wa Ujerumani, kocha Low anakiri kwamba wachezaji wake walikuwa na tatizo la kujiamini mno, kujiona kwamba kuwa mabingwa watetezi na kikosi kilichosheheni nyota basi wawadharau wapinzani wao, matokeo yake wakaenda sare mechi moja, wakafungwa moja na kushinda moja, wakawa wametolewa.

Wengine wanamlaumu Low kwa kuchagua majina makubwa, lakini watu wenyewe ‘wazee’ badala ya kuchukua chipukizi wa sasa ambao damu inachemka.

Alimwacha Leroy Sane wa Manchester City aliye kwenye kiwango cha juu na kuchukua wakongwe. Analaumiwa pia kumchukua na kumchezesha Mesut Ozil wa Arsenal ambaye hakuwa na jipya zaidi ya ‘uvivu’ uwanjani.

Low ana tatizo moja – anashindwa kupata uwiano kikosini kati ya ushambuliaji na beki tangu kwenye fainali za miaka minne iliyopita, ambapo aliokolewa na Miroslav Klose aliyefunga bao muhimu dhidi ya Ghana kabla ya kuwaongoza tena kwenye robo fainali.

Mwaka huu hawakuwa na Klose bali Thomas Muller, lakini hawakutisha kwenye ushambulizi licha ya kumiliki mpira kwa asilimia 65.3 kwenye hatua ya makundi.

Wapinzani wao walikuwa wakifanya mashambulizi ya kushitukiza na Ujerumani haikuwahi kushitukia wala kujilinda, licha ya kwamba ilioneshwa hayo hata kwenye mechi za kirafiki za kujiandaa kwa fainali hizi.

Brazil vile vile imekuwa ikicheza ‘open football’ wakati wenzao wakiegesha basi na kuwashitukiza kwenye ushambulizi, ndiyo maana iliwagharimu dhidi ya Ubelgiji.

Brazil inabaki kuwa timu iliyocheza soka la kuvutia zaidi licha ya kufungasha virago. Watu wanasema Kombe la Dunia halina mwenyewe na huenda mwaka huu wakachukua watu wasiofikiriwa kabisa.