JICHO LA MWEWE: Anko Ngassa ana kitu kizito moyoni

Monday November 5 2018

 

By Edo Kumwembe kumwembe@yahoo.com

UNCLE Mrisho Ngassa. Mmoja kati ya wanadamu wazuri ambao unaweza kukutana nao nje ya uwanja wa soka. Mtu hapo. Hana matatizo na watu. Ndio maana wachezaji wenzake wanamuita Anko. Ndani na nje ya klabu anazochezea.

Kwa sasa anatembea na siri nzito kifuani. Kwanza kabisa kuna faraja anaipata kwa kucheza Yanga. Anapata faraja kubwa sana kuliko hata mara ya kwanza alipoivaa jezi ya Yanga akitokea Kagera Sugar. Kila bao analofunga sasa hivi, au analotengeneza sasa hivi analifurahia zaidi kuliko mabao aliyokuwa anafunga na kutengeneza katika ubora wake.

Amepitia kipindi kigumu hapo katikati. Kipindi cha kucheza Mbeya City na Ndanda hakikuwa kizuri kwake. Watu walimbeza, walimkejeli, walimdharau. Ni kweli muda wake ulionekana kupita. Hakuwa na furaha alipoitazama Yanga ikicheza.

Shukrani kwa miguu mizito ya akina Juma Mahadhi, hatimaye Yanga waliona ni bora kuwa na Ngassa mzee kuliko Mahadhi kijana. Na sasa amerudi Yanga. Hapana shaka anapata faraja lakini bado ana kitu kizito moyoni.

Kwanza kabisa atakuwa amezielewa timu zinazoitwa Simba na Yanga. Alipokuwa fomu, alipokuwa anafunga kadri anavyojisikia, Mrisho alikuwa kipenzi cha matajiri wa Yanga. Walipokea simu zao na wakamuweka katika mioyo yao.

Muulize kama walikuwa wanapokea Simu zake wakati akiwa Ndanda au Mbeya City? Hawakuwa wanafanya hivyo. Mrisho amesema hilo hivi karibuni. Lakini pia ndani ya moyo wake Mrisho anajua kwamba amerudi Yanga kwa sababu ya umaskini wao.

Wakati akiwa Mbeya City na Ndanda, Mrisho alikuwa katika ubora wake wa kawaida sio kama ule wa zamani. Hata hivyo alikuwa anatamani sana kurudi Yanga. Viongozi wa Yanga walikuwa hawapokei simu zake na wanamkimbia. Hii ni baada ya kumtumia kwa muda mrefu na pia kumbania dili zake huku pia wakimpa ushauri mbovu wa maisha yake.

Moja kati ya ushauri mbovu ambao walimpa ni ule waliompa usiku fulani pale viwanja vya Leaders akiwa nao ndani ya gari. Walimwambia asiende El Marreikh ya Sudan na asaini kwao. Akaacha mshahara wa dola 5,000 na kuichezea timu yao kabla ya kuamua kuachana naye miaka miwili iliyofuata na wakagoma kumuongezea mkataba. Akaenda zake Sauz.

Leo wamemrudisha kwa sababu mbili. Kwanza ni kwa sababu ya akina Mahadhi kushindwa kufanya kile ambacho Simon Msuva alifanya. Msuva aliziba pengo lake na kisha Wanayanga wakamsahau Ngassa. Akina Mahadhi walishindwa.

Lakini pili ni hili la umaskini wa Yanga kwa sasa. Kama Yusuph Manji angekuwepo Yanga wangekuwa na pesa nyingi na badala yake wangekwenda nje kusaka winga mkali kwa bei yoyote ile. Haya ndio yalikuwa maisha ya Yanga ya kitajiri. Pesa ilikuwa inaongea.

Wakati watu wa Yanga wakimkimbia Ngassa miaka michache iliyopita walikuwa na pesa. Walikuwa matajiri sokoni. Katika soko la ndani wao ndio walikuwa wamelikamata halafu klabu nyingine zinagawana wachezaji ambao walikuwa hawatakiwi na Yanga.

Mrisho yote haya anayafahamu ndio maana kwa sasa ana kitu kizito moyoni. Hata sasa kuna viongozi ambao wanaongea mbovu wakiwa pembeni. Inaonekana kama ilikuwa hisani tu kumrudisha Jangwani wakati yeye mwenyewe anaamini kwamba anastahili kucheza Yanga kwa mambo mawili. kwanza kwa aliyowatendea siku za nyuma, lakini pili nadhani bado anajiamini kuwa ana kiwango cha kucheza Yanga.

Wao watu wa Yanga hawaamini sana hivyo. Siku tajiri akirudi rasmi klabuni na kuendeleza matanuzi nadhani jina la Mrisho ni miongoni mwa majina ambayo naamini yawekewa mstari kwa kalamu nyekundu. Ndivyo ilivyo.

Ukiachana na mambo ya Yanga, ni wazi kwamba moyo wa Mrisho una kitu kizito pindi anapotazama orodha ya wachezaji wanaosafiri kwenda Lesotho kucheza pambano ambalo linaweza kuweka historia ya Taifa Stars kwa kufuzu kwa mara ya pili kwenda Afcon.

Ndiyo, Mrisho angeweza kuwepo katika orodha hii kama mchezaji staa kama ilivyo Mbwana Samatta kama tu angeamua wakati ule akiwa moto kwenda Norway kucheza soka la kulipwa. Sasa hivi angekuwa mbali zaidi.

Angekuwa ameiva kuliko Mbwana. Angekuwa amepikwa katika misingi ya soka la Ulaya kwa muda mrefu na si ajabu mpaka sasa angekuwa katika kasi ile ile ambayo alikuwa nayo zamani. Angekuwa mchezaji mkongwe na anayeheshimika zaidi kikosini na kwa mashabiki. Pengine zaidi ya Samatta. Pengine angekuwa anatokea Bayer Leverkusen au Napoli.

Haya yote yapo katika kifua cha Mrisho kwa sasa. Hawezi kufungua mdomo wake na kusema. Hata hivyo anajua kwamba anapitia katika kipindi cha dharau huku akina Samatta wakiheshimika sana. kama angeweza kurudisha nyuma nyakati asingerudia makosa. Hata hivyo wakati ule tulikuwa tunamuhasa sana. washauri wake walikuwa wabovu.

Hata hivyo kwa sasa anafarijika. Anafarijika kwa kila bao analofunga na analotengeneza. Walau yupo Yanga na watu wanaweza kumuangalia kwa jicho tofauti na lile ambalo walikuwa wanamuangalia wakati akiwa Mbeya City au Ndanda. Walau wanapokea simu zake.