Hivi ndio jinsi wachezaji wanaumia ovyo

Friday April 5 2019

 

By DK SHITA SWAMWEL

KWA wafuatiliaji wa soka watakua wanamkumbuka mchezaji wa zamani wa Arsenal ya England, Santi Carzola, ambaye baadaye aliuzwa na kuhamia klabu ya Villareal ya nchini kwao Hispania.

Historia ya majeraha ya kiungo huyu mshambuliaji inaonesha alilazimika kuwa nje mara kwa mara kutokana na majeraha yaliyokuwa yanamwandama hali iliyochangia Arsenal kumuuza.

Katika mechi ya Ligi Kuu ya Hispania La Liga iliyochezwa katikati ya wiki katika siku ya Jumanne kati ya klabu yake ya Villareal na klabu ya Barcelona alionyesha kiwango cha juu katika eneo la kiungo.

Katika mchezo huo mkali Barcelona ilipumzisha mastaa wake kwa ajili ya mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ya wiki ijayo ingawa baadaye ililazimika kuwaingiza wakali wake ikiwamo Lionel Messi baada ya kuwa nyuma kwa mabao 4-2.

Licha ya kwamba Barca walifanikiwa kukomboa na mchezo huo na kuisha kwa sare ya bao 4-4, chamoto walikiona kwani eneo la kiungo lililokuwa chini ya Carzola liliwafanya wakabaji wa Barcelona na kupoteana.

Carzola ambaye sasa yuko fiti amenifanya kulitazama tatizo la wanasoka kutumika sana bila kupumzishwa kama moja ya sababu ya wanasoka kupata majeraha kirahisi mara kwa mara.

Ni kawaida katika medani ya soka kwa wanasoka wenye kiwango cha juu kutumika sana na klabu zao na timu za taifa.

Katika mechi hiyo mbinu iliyotumiwa na kocha wa Barcelona kuwapumzisha mastaa wake ni muhimu sana kwani inatoa nafasi miili ya wachezaji wake wanaotumika sana kupona majeraha ya ndani kwa ndani na pia kuondokana na uchovu wa misuli.

Wanasoka wengi wamekuwa wakipata majeraha ya mara kwa mara kirahisi kutokana na tatizo la kuchezeshwa kila mara bila hata ya kupata mapumziko.

Vile vile kufanyishwa mazoezi magumu kupita kiasi bila kuzingatia ushauri tiba wa kuwapumzisha wanasoka kila wanapotoka katika mechi ngumu.

Madhara gani wanayapata kutokana na kutumika sana?

Moja ya madhara wanayoyapata ni kupata majeraha ya kirahisi mara kwa mara hii ni kutokana na miili yao kukosa nafasi ya kupumzishwa ili kukabiliana na vijeraha vidogo vidogo vya ndani kwa ndani.

Pamoja ya kwamba tishu za mwili wa binadamu hufanya kazi zake kwa ufanisi mkubwa sana lakini pale zinapofanyishwa kazi kupita kiasi huweza kuwa chanzo cha wanasoka wa aina hii kupata majeraha.

Kadiri mwili unavyotumikishwa ndivyo pia unakuwa katika hatari zaidi ya kupata majeraha mbalimbali ikiwamo ya misuli, mifupa na nyuzi ngumu yaani ligamenti na tendoni.

Ili mchezaji kuweza kumudu jambo hili umri alionao una maana kubwa. Wanasoka wanapofikisha umri zaidi ya miaka 30 tayari mwili unakosa uimara ukilinganisha wanapokuwa na umri wa miaka 17-30.

Klabu kubwa ziko macho na umri wa mchezaji kwakuwa wanajua kuwa mchezaji kuwa na umri mkubwa na huku akitumika sana yupo katika hatari ya kukumbwa na majeraha yatokanayo na kutumika sana.

Wachezaji wanapotumika sana miili yao huweza kuambatana na majeraha wakati wanashiriki mazoezi na mashindano mbalimbali.

Wachezaji wanaposhiriki mazoezi magumu kwa muda mrefu au kuchezeshwa michezo mingi bila kupumzishwa hukumbwa na vijeraha na mchoko wa misuli.

Kuyapuuzia majeraha madogo wanayopata, mbinu dhaifu za mazoezi na dosari za programu za mazoezi wanayofanya huchangia kupata majeraha kirahisi.

Majeraha haya hutokana na mrundikano wa majeraha ya kujirudia mara kwa mara katika tishu za mwilini na kisha hapo baadaye jeraha hilo huongezeka ukubwa.

Pengine alipata jeraha katika mechi za kimataifa lakini hakulipa nafasi ya kupumzika majuma kadhaa ili kupona kabisa, baadaye anaposhiriki ligi ngumu ngazi ya klabu hujijeruhi zaidi.

Mwili wa binadamu kwa upande wa misuli na tishu nyingine pale zinapotumika sana huweza kujitengenezea mazingira ya kukabiliana na hali hiyo ikiwamo mbinu mpya za ukarabati wa jeraha na uponaji.

Mwili unapokuwa katika shinikizo kubwa na huku muda ukizidi kuyoyoma huweza kuongeza jeraha juu ya jeraha.

Mambo yanayoweka shinikizo kubwa katika jeraha au tishu ni pamoja kupigwa, kugandamizwa, kupindwa, kuvutwa, kujikunja na kupata mtetemo.

Hali hii huweza kuleta uchovu katika nyuzi ngumu za miishilio ya misuli, nyuzi ngumu zinazounganisha mfupa mmoja na mwingine, mishipa ya fahamu pamoja na tishu nyingine laini.

Ni vizuri klabu kuzingatia ushauri wa madaktari katika kuwatumia wachezaji kwa umakini pasipo kuwasababishia majeraha yasiyo ya lazima.