JIPANGENI: Wapya watakaokinukisha La Liga msimu ujao

Sunday July 21 2019

 

By FADHILI ATHUMANI

M SIMU mpya wa Ligi Kuu ya Hispania, La Liga unakaribia kuanza. Kwa kifupi tu, ule utamu wa ligi kubwa Ulaya kuanzia ya Hispania, England, Ujerumani, Ufaransa na Italia, zinakaribia kuanza na sasa kinachofanyika ni timu kusajili huku zikiendelea na ziara zao za kujiandaa na msimu mpya.

Huko La Liga, klabu zinasajili tu kuboresha vikosi vyao na mpaka sasa kuna dili tamu zilizokamilika ambazo zilikuwa zinasubiriwa kwa hamu.

Pia kuna dili nyingine kubwa zinatarajiwa na siku yoyote utasikia lolote juu ya dili hizo zitakazoifanya La Liga kuwa tamu zaidi msimu ujao

Achana na ishu ya Neymar ambayo hadi sasa wengi wanaisikilizia akihusishwa kurejea klabu yake ya zamani ya Barcelona kutokea PSG.

Kuna taarifa zinasema mabosi wa Barcelona wamewasilisha ofa poa kwa ajili ya Mbrazil huyo, aliyejiunga na PSG, misimu miwili iliyopita, kwa dau lililoweka rekodi ya Dunia, akitokea Camp Nou.

Wakati tukiendelea kusubiri kushuhudia mwisho wa filamu hii ya Neymar, Mwanaspoti linakuletea orodha ya wachezaji watano wakali waliotua nchini Hispania kukipiga La Liga msimu ujao.

Advertisement

5. LUKA JOVIC – REAL MADRID

Kwa hakika hii ilikuwa ni biashara poa sana kwa Eintracht Frankfurt.

Baada ya kumnunua kwa Euro 7 milioni tu kutoka Benfica ya Ureno, msimu huu wamemuuza kwa Euro 60 milioni kwenda Real Madrid na kuifanya biashara kwenda poa kwa uipande wao wakiondoka na faina nzuri tu. Hii ndio maana halisi ya soka ni biashara.

Luca Jovic, bila ubishi ni mmoja wa nyota waliotikisa msimu uliopita.

Jovic ni fundi wa kutikisa nyavu. Ana kila sababu ya kuwa mmoja wa washambuliaji bora duniani, anahitaji miaka chini ya mitano tu, kabla Dunia ya soka haijaanza kumuabudu.

Usajili wake unatajwa na wachumbuzi wa soka ni mpango wa kumsukuma Karim Benzema nje ya Santiago Bernabeu.

Kuna tetesi Mfaransa huyo, yuko mbioni kutundika daluga. Hiyo ikitokea muda wowote, bila shaka Zidane hatokuwa na presha.

4. FRENKIE DE JONG – FC BARCELONA

Kiungo huyu wa Uholanzi, ni moja ya sehemu ya maamuzi yatakayowanufaisha Barcelona msimu ujao, katika harakati za kusaka ubingwa wa Ulaya na kutetea ubingwa wao wa La Liga.

Frenkie De Jong, anatua Camp Nou, kurudisha imani.

Akiwa ni moja ya chimbuko la mawazo na falsafa ya marehemu Johan Cruyff, De Jong ni mchezaji aliyekamilika ambaye anakwenda Camp Nou, kunogesha safu ya kiungo ambayo kwa muda mrefu imekosa mauda mbwidambi za miguu ya watu kama Andres Iniesta na Xavi.

3. JOAO FELIX – ATLETICO MADRID

Kinda huyu wa Kireno, anatajwa kama mmoja wa mastraika wachanga wanaoibukia kwa kasi.

Usajili wake unaonekana kama moja ya sajili za kubahatisha zilizowahi kufanywa na Atletico Madrid. Diego Simeone, ameamua kucheza kamari, lakini ipo siku watamwelewa.

Ana kila dalili ya kuwa mchezaji bora wa Dunia wa baadae. The Colchoneros, wanaweza wakaonekana kukosea walipotoa Pauni 127 milioni kwa ajili ya kinda huyu, lakini kwa kuwa wanajivunia uwepo wa mmoja wa makocha bora duniani, hawana haja ya kuogopa.

Kingine ni, Joao hayuko pekee yake. Pale Wanda Metropolitano kuna vipaji vingi tu vya kusakata kabumbu, ambao wana uzoefu mkubwa vilevile.

Kama atathibitisha uwezo wake, sidhani kama atapata shida kuzoea mazingira ya Hispania. Anachotakiwa kukifanya ni kucheza soka safi tu.

2. ANTOINE GRIEZMANN – FC BARCELONA

Kumekuwa na mvutano mkubwa kuhusu usajili wa Mfaransa huyu. Barcelona na Atletico Madrid, waalijikuta wakiingua katika zogo kubwa, wakiwania umiliki wa nyota huyu. Hata hivyo, mwishowe, Griezmann, amefanikisha azma yake.

Unavyosoma makala haya, tayari ameshatua Camp Nou na anakwenda kuungana na Lionel Messi, Luis Suarez na Phillipe Coutinho, katika safu ya ushambuliaji ya Barcelona, huku ulimwengu ukiendelea kusubiri kurejea kwa Neymar.

1. EDEN HAZARD – REAL MADRID

Baada ya kukaa Stamford Bridge kwa takriban miaka 10 ya mafanikio makubwa, hatimaye kiungo wa zamani wa Chelsea, Mbelgiji Eden Hazard, alifanikiwa kujiunga na miamba ya soka ya Hispania Real Madrid, ambayo kwa mujibu wa maneno yake, ni klabu ya ndoto zake.

Hazard (28), aliichezea Chelsea mechi 245 na kufunga mabao 85 na baada ya kuwindwa kwa muda mrefu na Los Blancos, hatimaye aliondoka Darajani baada ya kuisaidia Chelsea kutwaa mataji kadhaa isipokuwa ubingwa wa Ulaya na sasa amekwenda kulisaka taji hilo kubwa kwingineko.