JICHO LA MWEWE: Tusidanganyane, kila mtu atavuna alichopanda Misri

MTU mmoja aliniuliza hivi: ‘Braza tunaiandaaje Taifa Stars kuelekea Misri’. Ni mtu ninayemheshimu kwa hiyo sitamtaja. Ni kiongozi wa soka. Alikuwa anaomba mchango wangu kuhusu namna tunavyoweza kuiandaa timu yetu.

Nilimwambia nitamjibu katika makala ili na Watanzania wengine waelewe. Leo nataka kumjibu ili tuelewane vyema. Kwanza kabisa sitegemei maajabu yoyote kutoka kwa Taifa Stars pale Misri. Sitaki kuwa mnafiki kabisa.

Ni kweli mpira wa Afrika wakati mwingine haueleweki, lakini sitaki kuwa mnafiki. Katika kundi lolote ambalo Taifa Stars ingepangwa lazima ingekuwa vibonde (underdog). Hili liko wazi kwa sababu tuliruhusu mpira wetu uachwe mbali na wenzetu. Pengo ni kubwa sana hata kama tumefuzu.

Tunajiandaaje? Ukweli hauwezi kujiandaa kwa michuano mikubwa wakati tukiwa tumebakiza wiki nne kabla ya michuano kuanza. Hakuna kikubwa ambacho unaweza kubadili. Michuano kama hii unajiandaa kabla haujafuzu. Ndio isishangae.

Michuano kama hii unajiandaa kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita. Unajiandaa kwa kuwa na ligi bora na yenye ushindani. Unajiandaa kwa kuwa na wachezaji wengi waliokwenda nje ndani ya kipindi hicho na kufanikiwa kuonyesha viwango kwa wenzetu.

Hili la pili tumeanza kujitahidi na kwa kiasi fulani limesababisha hata tufuzu. Kina Mbwana Samatta, Simon Msuva na wengineo wanaocheza nje walileta chachu katika kikosi cha Stars na kwa kiasi kikubwa walileta tofauti.

Hata hivyo, bado sana. Wakati Stars ikiwa na Samatta na Msuva, nchi nyingi ambazo zinashiriki michuano ya Afcon zina nyota kibao ambao, wanacheza Ulaya na zitawaacha nyumbani kwa kukosa nafasi katika vikosi vyao. Huu ni ukweli unaoumiza zaidi lakini lazima tuuseme.

Kuna nchi kama Senegal ambayo inaweza kuleta kikosi cha pili cha mastaa wao watakaowacha nyumbani na bado maisha yakawa magumu kwa Stars. Hata hivyo, wanachokifanya hawakukifanya kwa siku moja. Wamejiandaa kwa miaka mingi. Kina Sadio Mane wametokomea Ulaya miaka mingi iliyopita. Sisi tuna nyota tunaowategema na kuwapenda kama kina John Bocco wapo nyumbani.

Litakapokuja suala la uzoefu utaweza kuiona Stars ikishindwa kufurukuta. Wenzetu wamepambana kwa miaka mingi iliyopita. Sisi hapa kwetu ndio kwanza kina Samatta wameanza kupambana na uzoefu wa kucheza soka Ulaya.

Lakini, jambo la pili ambalo linaonyesha hatuna maandalizi ya michuano hii ni namna ligi yetu inavyoendeshwa. Asilimia 70 ya wachezaji wa Stars wanacheza katika ligi ambayo imeendelea kuwa vichekesho kwa kila namna. Hasa msimu huu.

Wanacheza katika ligi ambayo haina mdhamini, ligi ambayo ina viwanja vibovu, ligi ambavyo inaendeshwa katika staili ya bora liende. Unamwandaaje mchezaji wa kucheza Afcon kupitia katika ligi yetu wakati akina Mane, Idrissa Gana Gueye, Kalidou Koulibaly, Riyad Mahrez na wengineo wanatoka katika ligi bora za Ulaya?

Kuna nchi zina ligi bora kama Afrika Kusini na bado mastaa wao hawawezi kupambana na akina Sadio Mane.

Vipi sisi ambao tuna ligi ambayo Coastal Union wanawasili Dar es Salaam saa chache kabla ya mechi na kupigwa mabao 8-1? Unamuimarisha vipi Bocco kupitia aina hiyo ya mechi wakati Mane anatoka kucheza fainali za Ligi ya Mabingwa wa Ulaya na Liverpool pale Madrid? Tuwe wakweli jamani.

Kwa hiyo tuiache Stars kama ilivyo? Mtu anaweza kuuliza swali hilo. Jibu lake ni hapana. Kuna namna ya kufanya. Suala muhimu ni kuwaimarisha wachezaji kisaikolojia.

Kuwaambia watulie na wapambane. Waelewe umuhimu wa michuano. Waelewe kwamba hatuhitaji aibu ya kufungwa mabao mengi. Zama hizo zimepita.

Itakuwa ujinga kwa sasa kuwafua wachezaji kupitiliza. Hakuna haja ya kusoma vichwa vya habari ambavyo havitakuwa na maana. Itatia aibu kusoma vichwa vya habari kama vile ‘Amunike awafua Stars saa nne juani’. Wachezaji wanafuliwa kwenye klabu zao sio wakiwa timu ya taifa.

Kila mchezaji atavuna kutoka katika alichokipanda akiwa na klabu yake. Hakuna maajabu ambayo yanaweza kumbadilisha mchezaji kwa wiki nne. Huu ndio ukweli ambao wengi hatutapenda kuusikia, lakini lazima usemwe mapema.

Kila siku tunazungumza habari za mastaa wetu kwenda kucheza katika klabu zilizo katika ligi imara zaidi. Huu ni wakati wa mavuno. Tutavuna tulichopanda. Wenzetu huwa wanavuna walichopanda katika nyakati kama hizi.

Tuitumie michuano hii kuimarisha ndoto za vijana wadogo kama wale waliopo Serengeti. Tunahitaji kufuzu mara kwa mara. Wanahitajika wakae mbele ya televisheni zao na kujifunza vitu.

Lakini, kikubwa zaidi wanahitajika kuondoka sasa kwenda nje ili walau na sisi tuelekee katika michuano kama hii tukiwa washindani katika miaka ya mbele.

Kwa sasa sio washindani. Ni washiriki. Hata mashabiki wajifunze kuukubali ukweli huu mpaka wakati wa michuano. Tusiweke mategemo makubwa katika vichwa vya wachezaji.

Tunakwenda Misri kujifunza zaidi. Kujua ni wapi wenzetu walifanikiwa na sisi bado tumezubaa., tukitoka Misri tutapiga soga zaidi na kuelimishana.