Mwamba ulivyoigomea Chelsea mabao 21

LONDON, ENGLAND. CHELSEA imegongesha mwamba mara 21 kwenye Ligi Kuu England msimu huu ikiwa ni zaidi ya mara tatu ya ilivyogongesha Manchester United. Kama mipira yao yote waliyopiga ingetinga wavuni, bila shaka Chelsea wasingekuwa kwenye nafasi ya tano katika msimamo wa ligi hiyo wanayoshika kwa sasa.

Staa wa Chelsea, Eden Hazard ndiye mchezaji wa mwisho wa kikosi hicho cha Stamford Bridge kugongesha mwamba Jumapili iliyopita wakati walipochapwa 2-0 na Liverpool kwenye mchakamchaka wa ligi hiyo. Rekodi zinaonyesha baada ya kuchezwa mechi 34 kwenye ligi hiyo, The Blues wao ndio waliogonesha mwamba mara nyingi kama ingekuwa ubingwa wanabeba kwa jambo hilo, basi wangejibebea taji lao.

Hizi hapa ndio timu zilizogongesha mwamba mara nyingi kwenye Ligi Kuu England msimu huu.

Tottenham – mara 12

Kwenye msimamo wa Ligi Kuu England, Tottenham Hotspur wanashika nafasi ya tatu kwa kukusanya pointi 67 walizovuna kwenye mechi zao 33. Wababe hao wanaonolewa na Muargentina Mauricio Pochettino wamefunga mabao 64 kwenye ligi hiyo msimu huu, lakini wangefunga zaidi kama mastaa wake wasingegongesha mwamba mara 12. Timu nyingine zilizogongeza mwamba mara 12 ni Fulham na Newcastle United.

Everton – mara 13

Msimamo wa Ligi Kuu England unavyosomeka, Everton ipo kwenye nafasi ya tisa huko na pointi zao 46 walizovuna kwenye mechi 34. Kwa msimu huu, Everton wao imeshinada mechi 13, wakitoka sare saba na kupoteza mara 14 na kufunga 46 na kufungwa 44. Wababe hao wa Goodison Park wangefunga mabao mengi zaidi kama mashuti yao 13 waliyopiga golini yasingegonga mwamba.

Crystal Palace – mara 15

Wakali wa Selhurst Park wamekusanya pointi 39 katika mechi zao 34 walizocheza kwenye ligi na hivyo kushika nafasi ya 13 katika msimamo. Palace wamefunga mabao 40 tu na kufungwa 46, lakini mambo yangekuwa tofauti kama wasingegongesha mwamba mara nyingi. Palace wana -6 kwa sasa kwenye tofauti yao ya mabao ya kufunga na kufunga, lakini wangekuwa na +9 kama si mipira yao 15 waliyopiga kugonga mwamba kwenye ligi.

Liverpool – mara 17

Fowadi ya Liverpool imefunga mabao 77 kwenye Ligi Kuu England msimu huu yaliyowafanya kukusanya pointi 85 zinazowafanya kushika usukani wa ligi hiyo baada ya kucheza mechi 34. Msimu huu, Liverpool imeshinda mechi 26 ikitoka sare mara saba na kupoteza mara moja tu huku ikiruhusu wavu wake kuguswa mara 20. Hata hivyo, Liverpool ingefunga mabao mengi zaidi kama isingegongesha mwamba mara 17 kwenye ligi hiyo wanayopambana kusaka ubingwa wao wa kwanza.

Man City – mara 19

Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu England, Manchester City wanachuana jino kwa jino na Liverpool kwenye mbio za ubingwa wa ligi msimu huu wakiwa wamekusanya pointi 83 katika mechi 33 walizocheza. Kwenye ligi hiyo, Man City ndio waliofunga mara nyingi zaidi, mabao 86, lakini wangekuwa wamefunga zaidi ya mabao 100 kama mipira yao 19 waliyopiga ingegonga mwamba na kuwa timu inayoshika namba mbili kwa kugongesha mwamba mara nyingi zaidi kwenye ligi hiyo.

Chelsea – mara 21

Wakali wa Stamford Bridge wanapambana na hali yao kusaka kuwania nafasi ya kuwapo ndani ya Top Four ili kufuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao wakishika namba tano kwenye msimamo na pointi zao 66 walizovuna kwenye mechi 34. Wako pointi sawa na Arsenal wanaoshika namba nne, tatizo wametofautiana kwenye mabao ya kufunga na kufungwa tu. Chelsea wao wamefunga mabao 57, lakini wamekuwa na mabao mengi zaidi kama wasingegongesha mwamba mara 21 kwenye ligi hiyo msimu huu.

Timu nyingine

Kwenye ligi ya msimu huu kuna timu kibao zilizogongesha mwamba mara nyingi, ikiwamo Bournmeouth, Burnley, Cardiff City na Huddersfield zilizogongesha mwamba mara 11, wakati West Ham imefanya hivyo mara 10 huku Leicester City, Southampton na Wolves zikiwa zimegongesha mwamba mara tisa.

Arsena wamegongesha mwamba mara saba, huku Brigton, Manchester United na Watford zikiringana kwa kugogesha mwamba mara sita kila mmoja katika mechi zao walizocheza msimu huu kwenye mikikimikiki hiyo ya Ligi Kuu England iliyofikia patamu kabisa.