Mastaa lakini hawakugusa timu za Taifa

Muktasari:

  • Wachezaji mbalimba wameshindwa kupata namba katika timu zao za taifa kutokana na kuwepo kwa wachezaji bora zaidi katika mataifa yao

MILAN, ITALIA. WIKIENDI ya mechi za kimataifa imewadia. Ni wakati kama huu ambapo mashabiki wa soka duniani kote wamekuwa wakikumbuka jinsi ambavyo mataifa mbalimbali yalijaza wachezaji wenye vipaji kiasi kwamba kuna baadhi ya mastaa walikosa nafasi ya kukipiga katika timu za taifa.

Kama ingekuwa katika zama hizi si ajabu wangepata nafasi lakini kwa zama hizo hawakugusa hata timu zao za taifa.

Paolo Di Canio (Italia)

Katika orodha hii anaweza kuwa mchezaji mwenye kipaji zaidi ambaye hakuwahi kugusa katika kikosi cha Timu ya Taifa ya Italia. Kama ukilinganisha kipaji cha Mario Balotelli wa leo halafu ukijiuliza kwanini Di Canio hakuichezea Italia unaweza kushangaa. Licha ya ubora wake katika soka la England ikiwemo kupiga mabao ya mvuto lakini kamwe Di Canio hakuwahi kuichezea Italia. Mafanikio yake pekee ilikuwa ni kugusa katika kikosi cha Timu ya Taifa cha Vijana U-21. Kwa wakubwa hakugusa.

Mikel Arteta (Hispania)

Kipaji kingine kikubwa ambacho hakikuwahi kugusa katika jezi ya timu ya taifa. Arteta alitisha katika kikosi cha Everton chini ya David Moyes lakini kamwe hakuwahi kuvaa jezi ya Timu ya Taifa ya Hispania.

Kuna wakati Waingereza walitamani aichezee timu yao lakini haikuwezekana. Hata wakati alipoingia Arsenal bado haikumsaidia kuitwa Hispania. Sababu moja kubwa ni kuwa Hispania ilikuwa imesheheni wachezaji wengi mahiri eneo la kiungo ambao ndio walikuwa muhimili katika timu. Arteta angemng’oa nani katika kikosi cha Hispania kilichosheeni kina Xavi, Andres Iniesta, Xabi Alonso, Cesc Fabgregas na David Silva?

Thorsten Fink (Ujerumani)

Ni wazi hakuwahi kuwa mchezaji aliyetisha sana lakini daima alikuwa na mchango mkubwa uwanjani na alihaha kila sehemu. Sawa Ujerumani ilikuwa na mastaa wazuri lakini kwa mchezaji ambaye alitoa mchango mkubwa katika kikosi cha Bayern Munich akitwaa mataji manne ya Ligi Kuu, Matatu ya Kombe la Ligi na moja la Ulaya inashangaza kuona Fink hakuitwa katika kikosi cha Timu ya Taifa ya Ujerumani.

Mafanikio yake pekee ilikuwa kuichezea Timu ya Taifa ya Ujerumani ya U-21 mechi moja tu. Kwa sasa ni kocha wa Grasshoppers ya Uswisi.

Sylvain Distin (Ufaransa)

Mmoja kati ya mabeki ambao waliheshimika katika soka la England baada ya kucheza kwa kipindi kirefu akiwa na kikosi cha Everton chini ya Kocha David Moyes. Alipambana kadiri alivyoweza lakini kamwe hakuwahi kuwashawishi makocha wa Timu ya Taifa ya Ufaransa wamchukue katika ufalme wao. Mbaya zaidi kwa Distin hata akitazama nyuma bado rekodi yake haionyeshi kama aliwahi kukipiga katika timu za vijana za Ufaransa

Steed Malbranque (Ufaransa)

Kama ilivyokuwa kwa Distin ndivyo ilivyokuwa kwa Steed. Kiungo huyu alikuwa na mwendelezo wa ubora sana akiwa na klabu tatu za Ligi Kuu ya England; Fulham, Spurs na Sunderland.

Hata hivyo, makocha waliona haikutosha kwao kumchukua staa huyu.

Labda kwa sababu alikuwa anacheza katika zama za kina Patrick Vieira, Emmanuel Petit, Zinedine Zidane na wengineo lakini kama ingekuwa England au kwingineko, basi ni wazi Malbranque angeitwa katika kikosi cha timu ya taifa. Kinachoshangaza ni kwamba Malbranque alikuwa na uwezo pia wa kukipiga katika kikosi cha Timu ya Taifa ya Ubelgiji kwa vile alikuwa amezaliwa Mouscron, Ubelgiji lakini ni wazi timu zote mbili za taifa zilikuwa zimempuuza.

Steve Bruce (England)

Alikuwa mwamba katika safu ya ulinzi ya Manchester United mwanzoni mwa zama za Kocha Sir Alex Ferguson. Kamwe hakuwahi kugusa katika kikosi cha Timu ya Taifa ya England. Hakukuwa na sababu nyingine ya msingi zaidi kwanini hakuwahi kugusa jezi nyeupe za England ukweli ni kwamba wakati huo England ilikuwa imebarikiwa kuwa na mabeki bora sana wa kati. Inawezekana hakuonewa.

Romain Weidernfeller (Ujerumani)

Alikuwa kipa wa kudumu katika kikosi cha Borussia Dortmund ambacho kilitesa Ulaya katika utawala wa Kocha Jurgen Klopp.

Wakati mastaa wenzake karibu wote walikuwa wanaitwa katika timu zao za taifa lakini Weidernfeller hakuitwa katika kikosi cha Timu ya Taifa ya Ujerumani.

Maxi Lopez (Argentina)

Straika mwenye kipaji wa Argentina aliyetamba katika soka la Italia. Lopez aliiwakilisha Argentina katika soka la vijana lakini kamwe hakuwahi kugusa katika kikosi cha timu ya taifa ya Argentina huku uwezo wa mastaa wengine wa Argentina kama kina Carlos Tevez, Gonzalo Higuain au Sergio Aguero ukionekana kuwa kikwazo kwake. Aliwahi kukaririwa akidai alikuwa tayari kukipiga katika timu ya taifa ya Italia kama angeitwa, lakini hata hivyo Waitaliano hawakuwahi kumuita.