Makipa walioingia nyavuni mara nyingi

LONDON, ENGLAND,

ASIKWAMBIE mtu, magolikipa ni watu muhimu sana kwenye soka kama ilivyo washambuliaji. Kwa mfano David de Gea amekuwa na msaada mkubwa sana kwenye kikosi cha Manchester United.

Hata hivyo, kuna nyakati hizo, hata uwe kipa mahiri kiasi gani, kuna siku kwenye mechi unakumbana na kasheshe la kuokota mipira kibao kwenye wavu wako, kwa maana ya kufungwa mara nyingi katika mechi moja. Hilo pengine linaweza kusababishwa na ubora wa wapinzani wenu, mabeki wabovu au kuwa na siku mbaya tu kwenye ofisi yako, ambayo ni golini.

Unamkumbuka kipa Wojciech Szczesny? Wakati akiwa Arsenal, alikuwa mahiri sana lakini alikubali kufungwa mabao manane katika mechi moja wakati kikosi chake kilipomenyana na Man United kwenye mchezo wa Ligi Kuu England. Mechi hiyo ya msimu wa 2011/12, Arsenal ilichapwa 8-2, huku Wayne Rooney akifunga hat-trick.

Hata hivyo, usimcheke Szczesny tu? Hawa hapa makipa unaowaaminia kuwa ni matata kwenye milingoti mitatu lakini wameshawahi kupigwa nyingi katika mechi moja kati ya nyingi walizocheza.

5. Petr Cech – mabao 5 vs Arsenal

Kabla hajajiunga na Arsenal, Petr Cech alikuwa mmoja wa wachezaji muhimu kabisa kwenye kikosi cha Chelsea, aliposimama golini wapinzani walipata shida sana. Jambo hilo lilimfanya ashinde mataji kibao alipokuwa na The Blues. Lakini, katika moja ya mechi baina ya klabu yake hiyo ya zamani na hii ya sasa, kipa Cech aliruhusu mabao matano kwenye wavu wake, The Gunners wakimtesa.

Chelsea walichukua uongozi mara mbili katika mechi hiyo, lakini Arsenal ilitokea nyuma mara zote hizo kisha kuongoza. Straika Robin van Persie alipiga hat-trick usiku huo, Arsenal ikiichapa Chelsea 5-3.

4. Thibaut Courtois – mabao 5 vs Barcelona

Real Madrid ilianza msimu kwa mwendo wa kusuasua sana na hakika moja ya mechi zao mbaya kabisa ni ile ya El Clasico iliyokwenda kucheza uwanjani Nou Camp. Barcelona nayo ilianza msimu kwa kasi hafifu, lakini ilitumia nafasi ya ubovu wa mahasimu wao hao kuweka rekodi zao sawa kwenye mechi ya El Clasico.

Katika mechi hiyo, kipa Thibaut Courtois aliruhusu wavu wake kuguswa mara tano, huku Luis Suarez akifunga hat-trick. Mechi ilimalizika kwa matokeo ya 5-1, wenyeji Barcelona wakitoka uwanjani kibabe na hiyo ikawa mwanzo wa Kocha Julen Lopetegui kufutwa kazi huko Santiago Bernabeu.

3. Iker Casillas – mabao 5 vs Barc elona

Kipindi kingine ambacho Barcelona iliipiga Real Madrid Bao Tano ilikuwa mwaka 2010, ambapo mechi hiyo ilifanyika tena Nou Camp, Los Blancos wakakutana na kipigo cha 5-0. Katika mechi hiyo, David Villa alifunga mabao mawili, kisha Xavi, Pedro na Jeffren walifunga mabao mengine matatu yaliyobaki kuhitimisha tano.

Kipa Iker Casillas alikuwa kwenye goli la Real Madrid katika mechi hiyo na alikuwa nahodha wa wababe hao wa Bernabeu, lakini hakuwa na kitu cha kufanya kwenye mechi hiyo licha ya kwamba walikuwa hawajapoteza mechi yoyote kati ya 19 walizocheza kabla ya kwenda kukutana na kipigo hicho kizito huko Nou Camp.

2. de Gea – mabao 6 vs Man City

Manchester City ilikuwa kwenye msimu wake moto kabisa kwenye kuelekea kubeba ubingwa wa kwanza wa Ligi Kuu England. Hiyo ilikuwa kwenye msimu wa 2011/12 na moja kati ya mechi uhimu kabisa kwa msimu huo ni ile iliyoichapa Manchester United mabao 6-1.

Katika mechi hiyo, Man United kipa wake alikuwa David De Gea na kwamba siku hiyo alikuwa bize tu kuokota mipira kwenye wavu wake, ambapo washambuliaji Edin Dzeko na Mario Balotelli kila mmoja alifunga mara mbili, kabla ya Sergio Aguero na David Silva kuongeza mengine mawili na kuhimisha idadi hiyo ya mabao sita, huku Man United ikipata bao moja tu la kujifariji.

1. Kepa Arriz abalaga – mabao 6 vs Man City

Kipa, Kepa Arrizabalaga ametua kujiunga na Chelsea mwanzoni mwa msimu huu kwa pesa nyingi sana katika dirisha la majira ya kiangazi akitokea kwenye kikosi cha Athletic Bilbao. Kabla ya hapo, hakuwa amewahi kuruhusu wavu wake kuguswa mara sita katika mechi moja, hadi hapo alipowakabili Manchester City kwenye Ligi Kuu England Jumapili iliyopita ambapo Chelsea ilichapwa mabao 6-0 uwanjani Etihad.

Katika mechi hiyo, straika Sergio Aguero alifunga hat-trick yake ya 11 kwenye Ligi Kuu England, huku wafungaji wengine walikuwa Raheem Sterling, aliyetupia mbili na Ilkay Gundogan moja. Kilikuwa kipigo kizito kwa Chelsea ambacho kinatetemesha kibarua cha Maurizio Sarri.