MO Rashid Simba ndiyo basi tena

Saturday April 11 2020

 

By YOHANA CHALLE

KUSAJILIWA katika klabu kubwa zaidi kwenye soka la Tanzania, Simba au Yanga, ni ndoto ya wachezaji wengi wanaoinukia nchini.

Moja ya sababu zinazowafanya kutamani kusajiliwa kwenye timu hizo ni pamoja na kutangaza soko lao kimataifa kutokana na timu hizo kupata nafasi ya kushiriki michuano mikubwa Afrika mara kwa mara.

Uhakika wa malipo yao wakati wa usajili, mishahara mikubwa na bonasi zinazotokana na wao kufanya vyema kwenye ligi na mashindano mengine, ni kati ya vitu vingine vinavyowavutia wengi kujiunga na miamba hiyo ya soka la Bongo.

Mohamed Rashid ‘Mo Ibrahim’ ambaye kwa sasa anakipiga katika kikosi cha JKT Tanzania kwa mkopo akitokea Simba, anaeleeza mengi kuhusu usajili wake ndani ya klabu hiyo ya Msimbazi hadi kuondoka kwake. Alitua Simba akitokea Prisons ya Mbeya.

KILICHOMKIMBIZA SIMBA

“Nilifurahia maisha ya Simba wakati wa Kocha Pierre Lechantre kwa maana yeye ndiye aliyependekeza nisajiliwe, hivyo nikawa napata nafasi kubwa ya kucheza kila mara, lakini kutua kwa Patrick Aussems kulinifanya kuanza kupotea.

Advertisement

“Nilipoona mambo hayapo sawa nikaamua kuondoka kwa mkopo ili kusaka nafasi ya kucheza kila wakati na nina furaha hapa JKT Tanzania. Nimefanikiwa katikahilo na kurejesha uwezo wangu.

“Unajua makocha wa kigeni wanapomhitaji mchezaji ujue kuna kitu amekiona, na anapokukataa kuna sababu pia kutokana na mfumo wake, hivyo Lechantre aliniona wakati Simba ikiikabili Tanzania Prisons hapa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.”

Ushindani wa namba ilikuwa sababu moja wapo iliyomkimbiza mchezaji huyo ndani ya kikosi cha Simba kutokana na kuwakuta wachezaji waliomzidi kiwango.

ANAMKUBALI BOCCO

“Nilipokuwa nje ya Simba nilimtazama John Bocco kwa jicho la tofauti sana, lakini mara baada ya kujiunga Simba ndio alikuwa msaada mkubwa kwangu.

“Bocco sio tu alikuwa nahodha kwenye timu, bali pia alikuwa akinishauri mambo mengi ili kuhakikisha nafikia yale ambayo nilikuwa natamani.

“Timu kubwa zinakuwa na makocha wengi wenye uwezo tofauti, hivyo hata mbinu zao zinakuwa tofauti ambazo zinakupa maarifa ya maisha ya soka.”

HARUDI TENA SIMBA

“Bado nipo JKT kutokana na mkopo wa mkataba wa Simba na hakuna mazungumzo yoyote hadi sasa, na hata kama wakisema watahitaji kuniongezea mkataba sitakuwa tayari.

“Nahitaji kupata timu ambayo itanipa nafasi ya kucheza kila wakati, hii itanifanya kuonekana zaidi na kukuua zaidi ya hapa.”

ALIVYOWATOSA YANGA

“Yanga walinihitaji. lakini kikubwa nilichokuwa nakitazama kwa upande wangu ni maslahi binafsi na sio kitu kingine maana ofa zilikuwa nyingi tena kwa wakati mmoja.

‘Maisha ya soka la Bongo siku zote inategemea na upepo wa wakati huo uliopo na hapo lazima uzichange vyema karata zako.

“Nikathaminisha dau ambalo Yanga waliniambia na timu nyingine ambazo walileta ofa nikaamua kuachana na Yanga, hivyo hakuna sababu nyingine zaidi ya dau lililowekwa mezani.”

AMTIBUA BABA YAKE

Wazazi wengi hawaamini soka kama ni sehemu moja wapo ya kijana kufanikiwa kwenye maisha yake kutokana na mfumo wa soka letu lilivyokuwa miaka ya nyuma.

“Baba yangu hakupenda nijihusishe kabisa na soka, alipenda nisome ili siku moja amuone kijana wake yupo katika levo fulani kwenye elimu.

“Mambo mengi nilikuwa napata sapoti kutoka kwa mama yangu kwani nilichokuwa namuambia alikuwa akinisapoti lakini mzee hakutaka kabisa kusikia kuhusu soka.”

KIKOSI CHAKE

Kikosi bora cha Mo Rashid ni Patrick Munthali (JKT Tanzania, Shomary Kapombe (Simba), Hansi Masoud (Alliance FC), Edson Mugisha (Kagera Sugar), Mohamed Faki (Mbeya City), Jabir Aziz ‘Stima’ (JKT Tanzania), Ally Kagaw, Danny Lyanga (JKT Tanzania), Mgandila Shaaban (Ruvu Shooting), Adam Adam (JKT Tanzania) na Sixtus Sabilo wa Polisi Tanzania.