Wakali wa Ballond’Or waanza kutajwa

Muktasari:

Cristiano Ronaldo ndiye mchezaji anayeshikilia tuzo ya Ballon d'Or kwa sasa na ametajwa tena kugombea

MASUPASTAA, Gareth Bale, Cristiano Ronaldo na Kevin De Bruyne ni miongoni tu mwa majina ya awali ya mastaa wa nguvu kwenye soka ambao watachuana kuwania Tuzo ya Ballon d’Or.

Orodha ya majina imeanza kutolewa na Jarida la France Football ambapo taarifa zinasema kutakuwa na wachezaji 30 ambao wataingia kwenye mchujo kabla ya kupatikana wale watakaoingia fainali ya kuwania tuzo hiyo ya ubora wa soka duniani ambayo hutolewa kila mwaka.

Ronaldo, ambaye ameondoka katika klabu yake ya Santiago Bernabeu ya Real Madrid, ameshatupia mara nne kwenye Serie A ya Italia msimu huu akiwa na kikosi cha Juventus ndiye mchezaji anayeshikilia tuzo hiyo kwa sasa.

Lakini kwa majina 10 ya awali yaliyolewa, Ronaldo atakutana na vyuma kama Sergio Aguero, De Bruyne, Bale, Alisson Becker, Thibaut Courtois, Roberto Firmino, Diego Godin, Edinson Cavani na Karim Benzema.

Majina mengine yataendelea kutolewa katika kinyang’anyiro hicho kupata mchezaji bora wa mwaka huu wa mchezo wa soka, ambapo kwenye tuzo ya Fifa, Luka Modric wa Real Madrid na Croatia, ndiye aliyeibuka mchezaji bora wa mwaka wa dunia, akibeba pia tuzo ya kuwa mchezaji bora wa Ulaya. Modric pia alichaguliwa mchezaji bora wa Kombe la Dunia.