Wanakuja, wanasepa Big Six EPL vita kali tu

Friday May 17 2019

 

LONDONN, ENGLAND. MANCHESTER City na Liverpool zinaripotiwa kwamba vita yao itaendelea kwenye usajili zikichuana kunasa wachezaji matata ili kuja kushindana kwenye ligi msimu ujao.

Lakini suala la usajili ni mchakato utaohusisha vigogo vingine kwenye Ligi Kuu England kama vile Chelsea, Tottenham, Arsenal na Manchester United ambazo bila ya shaka zitaingia sokoni kunasa wachezaji ili huo msimu ujao uwe wa vuta nikuvute.

Kinachotarajiwa kutoka kwenye klabu za Big Six kwenye Ligi Kuu England wakati wa kipindi hiki cha usajili ni kuwa bize kutafuta wachezaji wapya wa kuboresha vikosi vyao.

Huu hapa mtoko wa Big Six kwenye dirisha hili la usajili wa majira ya kiangazi huko Ulaya ili kutengeneza vikosi matata vitakavyotoana jasho kwenye Ligi Kuu England msimu ujao.

MAN CITY

Inaowasaka: Kipa, beki wa pembeni, beki wa kati, kiungo mkabaji, kiungo, fowadi

Advertisement

Wanaoondoka: Claudio Bravo, Danilo, Nicolas Otamendi, Eliaquim Mangala, Vincent Kompany, Ilkay Gundogan, Leroy Sane.

Bajeti: Pauni 150 milioni

Mipango: Pep Guardiola angehitahi kukifanyia marekabisho kidogo tu kikosi chake, lakini shida ni kwamba wachezaji wake muhimu umri umeanza kuwatupa mkono huku wakiwa na wasiwasi wa kukumbana na adhabu. Vincent Kompany, Fernandinho na David Silva wote hao wanahitaji wabadala wao katika kipindi cha miezi 18 ijayo huku wakali kama Ilkay Gundogan na Leroy Sane wamekuwa na viwango visivyoeleweka. Kutokana na hilo, ndio maana Man City inatazamiwa kuwa bize kwenye dirisha lijalo la usajili kunasa wachezaji wapya ambapo bajeti yao ya sasa ya Paunni 150 milioni itaongezeka kwa kuuza wachezaji.

Wachezaji wengi inaowasaka mmoja wao ni staa wa Benfica, Joao Felix, lakini wanamsaka pia mchezaji wa Atletico Madrid, Rodri anayetajwa kuwa na thamani ya Pauni 60 milioni, huku ikipambana kunasa huduma ya Ben Chilwell wa Leicester City, ambaye iliweka kando kidogo usajili wake baada ya Oleksandr Zinchenko kufanya vizuri.

Atletico ni miongoni mwa timu nyingi zinazomtaka Nicolas Otamendi na ndio maana unamwona kabisa mchezaji huyo akiondoka Etihad kumpatia pesa Guardiola za kuongezea kwenye usajili.

LIVERPOOL

Inaowasaka: Kipa, beki wa kushoto, winga, straika

Wanaoondoka: Simon Mignolet, Alberto Moreno, Daniel Sturridge, Dejan Lovren, Rafael Camacho, Xherdan Shaqiri

Bajeti: Pauni 100 milioni

Mipango: Liverpool ina kikosi matata na makinda balaa kabisa ambao wanamfanya Kocha Jurgen Klopp kutokuwa na presha kubwa. Mkurugenzi wa Michezo, Michael Edwards na timu yake ya usajili wameshaanza michakato ya kuhakikisha wanakifuma kikosi hicho kuwa imara kabisa ili kuwa na nguvu ya kupambana na kubeba mataji msimu ujao.

Mipango yao ni kusaka wachezaji wenye umri wa miaka 20 ili kuendana na falsafa za kocha wao, Klopp huku wakitazama pia kwenye bei zao. Orodha yao ina wachezaji wengi inaowasaka akiwamo winga wa Villarreal, Samuel Chukwueze, staa wa Ajax, David Neres na mchezaji wa Bayer Leverkusen, Julian Brandt huku wakimfuatilia kwa karibu winga wa Lille, Nicolas Pepe na beki kinda wa Bristol City, Lloyd Kelly.

Liverpool inahitaji kipa wa kumsaidia Alisson Becker baada ya kuonekana kama Mignolet ataondoka huku mpango wao ni kumchukua pia straika wa Celta Vigo, Maxi Gomez. Xherdan Shaqiri amekuwa na msimu mzuri, lakini mambo yalivyo anaweza kuachana na wababe hao wa Anfield kwenye dirisha lijalo la majira ya kiangazi.

CHELSEA

Inaowasaka: Beki wa kushoto, beki wa kati, kiungo, winga, straika

Wanaoondoka: Eden Hazard, Callum Hudson-Odoi, Willian, Davide Zappacosta, Danny Drinkwater, Tiemoue Bakayoko, Gary Cahill.

Bajeti: Pauni 150 milioni

Mipango: Chelsea haitaki kumwaachia mchezaji wake yeyote bora aondoke kwenye kikosi hicho hasa kwa kipindi hiki inachokabiliwa na adhabu ya kuzuiwa kusajili.

Bado inaamini rufaa yake iliyokata huko kwenye mahakama ya rufani ya mambo ya michezo CAS inaweza kushinda na kuwa na nguvu kwenye kufanya usajili dirisha lijalo. Lakini, Eden Hazard anataka kwenda Real Madrid, licha ya kwamba wababe hao wa Bernabeu itabidi wapandishe dau lao la kufikia Pauni 100 milioni anazotaka Marina Granovskaia. Chelsea inafahamu pia Willian anaweza kwenda Barcelona huku Bayern Munich ikimtolea macho Hudson-Odoi na Aston Villa na Everton zinawataka kuwabeba jumla Tammy Abraham na Kurt Zouma.

Imefanya usajili wa Christian Pulisic Januari mwaka huu na inaamini ujio wake utakuwa na kitu cha ziada kwenye kikosi chake huku ikitaka kuboresha safu yake ya ushambuliaji kwa kuwapigia hesabu Luka Jovic na David Neres. Makinda wengine inayowasaka ni Houssem Aouar wa Lyon na Bruno Guimaraes wa Athletico Paranaense. Chelsea inataka irudi na nguvu ya kushindania ubingwa msimu ujao.

TOTTENHAM

Inaowasaka: Beki wa kushoto, beki wa kati, kiungo, winga, straika

Wanaoondoka: Serge Aurier, Danny Rose, Kieran Trippier, Toby Alderweireld, Victor Wanyama, Vincent Janssen, Fernando Llorente, Christian Eriksen

Bajeti: Pauni 150 milioni

Mipango: Mauricio Pochettino amewatumia sana wachezaji waliopo kwenye kikosi chake kwa sasa, hivyo anahitaji kuleta wengine wapya kuongeza nguvu. Bajeti yake ni Pauni 150 milioni na pesa nyingine itapatikana kwa kuuza wachezaji. Tottenham inahitaji kujijenga upya kwenye sehemu ya kiungo na mpango wake ni uleule wa kusajili wachezaji wenye umri mdogo ili waje kuuzika baadaye.

Wakati mgumu unaowakabili ni ule wa kuamua nani wa kuondoka hasa baada ya wachezaji hao kucheza kwa kiwango kikubwa sana msimu huu na kuifikisha timu hiyo kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

kwenye mipango yupo staa wa Fulham, Ryan Sessegnon na pia inawasaka David Brooks wa Bournemouth na Jack Grealish wa Aston Villa.

Staa wa Barcelona, anayecheza kwa mkopo Everton, Andre Gomes yupo kwenye hesabu pia sambamba na Gedson Fernandes wa Benfica, Donny van der Beek wa Ajax, Nicolo Zaniolo wa Roma na beki wa Freiburg, Robin Koch. Itafanya usajili pia wa kuzingatia kukipa nguvu kikosi chake cha U-23.

ARSENAL

Inaowasaka: Kipa, beki wa kushoto, kiungo, winga

Wanaoondoka: Danny Welbeck, Aaron Ramsey, Mohamed Elneny, Shkodran Mustafi

Bajeti: Pauni 50 milioni

Mipango: Unai Emery anataka beki wa kati ambaye ataweza kucheza kwa kutumia nguvu na akili ili kuifanya ngome ya timu yake kuwa imara huku akitaka pia viungo wapishi wa mabao na winga matata.

Mkurugenzi mpya wa ufundi anayekuja, Edu ni shabiki mkubwa wa Wilfried Zaha na mpango wake ni kuleta mchezaji mwenye kasi ya aina hiyo kwenye kikosi hicho. Hata hivyo, thamani ya Zaha ni Pauni 80 milioni, hivyo kwenye bajeti yao itabidi wauze wachezaji wengine. Arsenal pia inamtaka Ryan Fraser wa Bournemouth na David Neres wa Ajax.

Wachezaji wengine inaowafukuzia ni Eric Bailly, Djene Dakonam, Mario Hermoso na Samuel Umtiti huku pia ikiwasaka Marcos Llorente wa Real Madrid, Adrien Rabiot, Christopher Nkunku, Nicola Barella wa Cagliari na kiungo wa Sampdoria, Dennis Praet.

Mustafi ni mmoja kati ya wachezaji wanaotazamiwa kuuzwa ili kupata pesa za kuongezea bajeti ya usajili kuleta majembe ya maana kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi huko Ulaya.

MAN UNITED

Inaowasaka: Kipa, beki wa kulia, winga, straika

Wanaoondoka: David de Gea, Antonio Valencia, Matteo Darmian, Eric Bailly, Ander Herrera, Juan Mata, Paul Pogba, Alexis Sanchez, Romelu Lukaku

Bajeti: Pauni 200 milioni

Mipango: Kocha Ole Gunnar Solskjaer anataka kusajili wachezaji wenye umri wa miaka 24 kushuka chini akitaka kuwa na kundi bora kabisa kwenye kikosi chake ili kuwa na timu itakayokuwa ikisilikiza maelekezo yake na yale ya msaidizi wake Mike Phelan.

Anafahamu wazi kuna baadhi ya wachezaji wenye majina wataondoka na watatumia kipindi hicho kuleta damu changa zenye uchu. Mchezaji ambaye mwenye umri mkubwa atakayesajiliwa basi ni yule atakayekuja kuleta kitu cha tofauti kwenye timu na ndio maana anatajwa Gareth Bale kwenye mpango huo.

Makinda inaowasaka ni Dan James wa Swansea City, Aaron Wan-Bissaka wa Crystal Palace. Ole anataka pia mshambuliaji na viungo wawili huku Youri Tielemans akiwekwa kwenye orodha.

Kuna mashaka makubwa kuhusu Sanchez na Lukaku huenda wakaondoka mwishoni mwa msimu huu huku Anthony Martial akipewa muda hadi Januari kuthibitisha uwezo wake. Kinachoshangaza, Ole hataki beki wa kati.

Advertisement