Paul Pogba kuvaa namba 8 Monaco

Muktasari:
- Staa huyo Mfaransa amesaini mkataba wa miaka miwili katika klabu hiyo, ambapo atapata nafasi ya kurudi uwanjani kuonyesha makali yake baada ya kutokea kwenye adhabu ya kufungiwa karibu miaka miwili.
MONACO, UFARANSA: KIUNGO supastaa, Paul Pogba amekamilisha uhamisho wake wa kujiunga na AS Monaco, ambako atavaa jezi yenye Namba 8 mgongoni, imeelezwa.
Staa huyo Mfaransa amesaini mkataba wa miaka miwili katika klabu hiyo, ambapo atapata nafasi ya kurudi uwanjani kuonyesha makali yake baada ya kutokea kwenye adhabu ya kufungiwa karibu miaka miwili.
Pogba, 32, aliondoka Juventus mwishoni mwa 2024, lakini hakuwa na uwezo wa kujiunga na klabu yoyote hadi mwishoni wa msimu. Na sasa, amejiunga na klabu hiyo ya Ufaransa ili kukipiga kwenye Ligue 1 na Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Monaco na Pogba walithibitisha dili hilo Jumamosi iliyopita, hivyo atakuwa kwenye kikosi hicho ambacho kilimaliza nafasi ya tatu kwenye Ligue 1 msimu uliopita, hivyo kukamatia tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Kwa kitendo hicho, Pogba anakwenda kuungana na wakali wengine kadhaa wa zamani waliowahi kukipiga kwenye Ligi Kuu England, wakiwamo mastraika wa Arsenal, Flo Balogun na Mika Biereth.
Hata hivyo, kuna muunganiko mwingine wa Ligi Kuu England ukibainisha namba ya jezi ambayo atavaa kiungo huyo wa zamani wa Manchester United.
Pogba amekabidhiwa jezi Namba 8, ambayo imeachwa wazi na Al-Musrati baada ya mkopo wake kuondoka. Namba hiyo pia iliwahi kuvaliwa na staa wa Real Madrid na Ufaransa, Aurelien Tchouameni na wachezaji wengine kibao kama vile Youri Djorkaeff, Sylvain Legwinski na Jean Tigana.
Wengine ni Ali Benarbia, Joao Moutinho, Youri Tielemens na Adrien Silva. Kwenye kikosi cha Monaco, mastaa wengine wapya ambao wanaweza kunaswa na timu hiyo ni pamoja na beki Eric Dier.