Sofapaka yaifanyia unyama Sportive

Tuesday July 17 2018

 

By JOHN KIMWERE, NAIROBI

SOFAPAKA Youth FC imeinyuka Salem Sportive FC mabao 3-1 nayo Mbotela Youth iliidunga Black Mamba FC 2-1 kwenye mechi za Ligi ya Kaunti ya FKF Tawi la Nairobi East msimu huu. Sofapaka Youth inayoendelea kutikisa mahasimu wao ikiwamo Uprising FC ilizoa ufanisi huo baada ya kuchoma Kiambiu Warriors mabao 3-1 wiki iliyopita.

Mbotela Youth FC chini ya Kocha  Dennis Arori ilitia kapuni alama tatu kutokana juhudi zake Kelvin Wambua na Caleb Ondimu. ''Sina budi kuwapongeza wachezaji wangu kwa kutwaa pointi tatu muhimu wiki moja baada ya kudondosha alama sita,'' Arori alisema na kuongeza kuwa wamo mbioni kupigana kwa udi na uvumba kuhakikisha wameibuka miongoni mwa nafasi bora mwaka huu.

Naye Lucas Maina aliifungia Kiambiu Warriors bao moja na kuibeba kuchuna ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Madiwa City FC kabla ya kukung'utwa mabao 8-0 na Kariobangi South United.  Kwenye patashika nyingine kipute hicho, Umoja Rhinos FC ilipiga hatua ilipovuna ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Country Bus FC.

 

Advertisement