Muguna atua Stars kuivaa Equitorial Guinea

Monday May 28 2018

 

By Fadhili Athumani

Nairobi. Kiungo wa KF Tirana ya Albania, Kenneth Muguna atakuwemo katika kikosi Harambee Stars kinachoshuka uwanjani leo, kukabiliana na Equatorial Guinea, kwenye mchezo wa kirafiki wa kimataifa, utakaopigwa ugani Kenyatta, mjini Machakos kuanzia saa 10 alasiri.
Uwepo wa Muguna ni habari njema kwa kocha Sebastien Migne baada ya maproo wake kadhaa, kujiengua kikosini na hivyo kusalia na wachezaji wa ndani huku maproo pekee wakiwa ni Musa Mohammed na Eric Ouma (hawana timu kwa sasa).
Muguna licha ya kuwa kiungo ni fundi wa kufumania nyavu ataongeza morali katika kikosi cha Stars, kuelekea mchezo huo ambao mtihani wa pili kwa Kocha Migne tangu akabidhiwe mikoba ya kuinoa Harambee Stars. Mechi ya kwanza Stars ililala 1-0 dhidi ya Swaziland.
Akizungumzia mchezo huo na maandalizi ya jeshi lake, kocha Migne alisema wamejifunza kutokana na makosa yaliyojitokeza dhidi ya Swaziland na kuongeza kuwa, vijana wake wako tayari kukabiliana na Equatorial Guinea.
"Tulishindwa kutumia nafasi tulizopata dhidi ya Swaziland, katika siku hizi mbili tumejikita katika kuyafanyia kazi baadhi ya makosa yaliyojitokeza, vijana wako vizuri na Wakenya wategemee matokeo chanya", alisema Migne.
Mfaransa huyo, anayesaidiwa na wakufunzi wa U19 na U20, Francis Kimanzi na Stanley Okumbi, anatumia mechi hizo mbili za kirafiki kama sehemu ya maandalizi kabla ya kukutana na Ghana katika mchezo wa kusaka tiketi ya kufuzu michuano ya mataifa huru barani Afrika 2019.
Kabla ya mechi hiyo itakayopigwa katika uwanja wa Moi Kasarani, Septemba, Harambee Stars, itaelekea nchini India kwa ajili ya michuano ya mabara (Intercontinental Cup), inayohusisha timu nne za New Zealand, Kenya, Taipei ya China na wenyeji India.
Wachezaji walioko kambini ni pamoja na Kipa namba moja wa Gor Mahia aliyehusika kwenye mchezo dhidi ya Swaziland, Boniface Oluoch, Nahodha Joackins Atudo, kiungo mchezeshaji Francis Kahata na Kenneth Muguna.
Wengine ni Patrick Matasi na Timothy Odhiambo (makipa), Erick Ouma, Michael Kibwage, Joash Onyango, Duncan Otieno, Patillah Omotto, Philemon Otieno, Whyvonne Isuza, Ovella Ochieng, Humphrey Mieno, Marvin Nabwire, Chrispin Oduor, Jaffary Owiti, Mutamba Pistone, Musa Mohamed, Wasambo Vincent, Timothy Otieno, Shakava Harun na Bolton Omwenga

Advertisement