Lewa Marathon: Lopekana hoi nusu marathon

Saturday June 30 2018

 

By Fadhili Athumani

Isiolo, Kenya. Bingwa mtetezi wa mbio za hisani za Lewa marathon, kilomita 21 kwa wanawake, Perendis Lopekana ameshindwa kutetea ubingwa wake katika makala ya 19 ya mbio hizo zinazofanyika kila mwaka katika hifadhi ya wanyama ya Lewa, iliyoko mjini Isiolo, kaunti ya Meru.

Lopekana alikimbia mbio hizo akitumia muda wa saa 1:16:34, dakika moja na sekunde 20, nyuma ya mshindi wa kwanza Mary Ngendo, aliyevuka utepe, akikimbia kwa muda wa saa 1:15:14 huku nafasi ya tatu ikienda kwa Esther Waweru Wangui (1:20:01).

Kufuatia matokeo hayo, Lopekana aliyekuwa anapigiwa upatu kuibuka mshindi alisema kilichomponza ni kuanguka, baada ya mzunguko wa kilomita 39, hali iliyopelekea mpinzani wake (Mary Ngendo), kumpita na kuongoza mbio hizo.

“Imeniuma sana kushindwa kutetea ubingwa wangu, niliyumba kidogo baada ya kujigegedua, tukiwa pale kilimani, mwenzangu alitumia nafasi hiyo kuongoza mbio, mwisho wa siku ikawa kama ilivyotokea. Nitarudi upya mwakani,” alisema Lopekana.

Kwa upande wa wanaume, mwanariadha Maurice Munene, aliibuka mshindi, akitumia muda wa saa 1:05:39, akimpiku mshindani wake wa muda mrefu, Kiprono Kipkemboi, aliyevuka utepe, akitumia saa 1:06:07, sekunde 18 mbele ya Silas Kimutai (1:06:23).

Tangu mwaka 2000, ambapo mbio za kwanza zilizpofanyika, Lewa Marathon, imekuwa ikifahamika kote duniani kutokana na ugumu wake, hasa hali ya hewa isiyotabirika, njia zisizoeleweka na washiriki wakubwa katika medani ya riadha.

Advertisement

Baadhi ya majina makubwa kuwahi kushiriki mbio hizi ni mshindi wa fedha katika michezo ya Olimpiki, mwaka 2004, Catherine Ndereba na Rais wa Kamati ya Olimpiki (NOCK), Paul Tergat.

 

Advertisement